Norbert Mporoto
Member
- Jul 18, 2020
- 14
- 12
“Mgeni Wa Mvua Hafukuzwi, Mwache Aweke Mzigo Wake”
Na; Norbert Mporoto
Tanzania.
28042021
Baruapepe: uhurunifikra9406@hotmail.com
Ilikuwa siku ya mwaka mpya kijijini Rani, katika mji wa King William mnamo mwaka 1942. Hii ndiyo siku ambayo nuru ya ukombozi iling'ara kuangazia bara hili la Afrika, hususani kwa wananchi wa Afrika ya Kusini ambao ndiyo wahanga wakubwa wa sekeseke la ukoloni kupitia mfumo wa ubaguzi wa rangi. Ni siku ambayo furaha ya mzee Wimot Goso na Bi Nobantu Ntebe ilizidi kifani kwani ndipo walipotuletea shujaa huyu, Victoria Nonyamelezo Mxenge. Mama aliyeuthibitishia umma wa bara la Afrika na dunia kwa ujumla ya kwamba nafasi ya mwanamke wa kiafrika inajitosheleza kuyamudu mapambano.
Mama huyu kupitia wazazi wake alifaidi sana thamani ya malezi ya kiafrika (ambayo kwa sasa ni nadra kuyapata kwa uzuri na ubora ule) kiasi cha kumpa chachu ya kuwa moja ya watu wanaochangia kwa hali na mali ukombozi wa jamii yake kufuatia historia na matatizo aliyoshuhudia ndani ya taifa lake.
Historia ya mama huyu ilizidi kukua kwa kasi kama moto wa kiangazi huku ikiwashangaza watu wengi. Kwa kuthamini nafasi ya maarifa na kukua kiuelewa, wazazi wake walimuanzishia vyema safari yake palepale kijijini Tamara ambako alipata elimu yake ya msingi, na baadae akajiunga katika shule ya sekondari Forbes Grant. Na mapema mwaka 1959 baada ya kuhitimu sekondari, alifanikiwa tena kuendelea na elimu yake ya sekondari katika shule ya Healdtown iliyoko Fort Beaufort, jimbo la Mashariki. Elimu yake Bi Victoria haikuishia hapo, na baada ya kuhitimu alipata nafasi ya kujiunga katika hospitali ya Victoria akisomea taaluma ya utabibu (ukunga), na hatimaye mwaka 1964 alifuzu mafunzo hayo.
Jitihada hizi za kuijenga taaluma yake, na kujiweka karibu na maarifa zilikuwa tayari kwa kuitumikia jamii yake. Sambamba na hilo, hicho ndicho kipindi ambacho Victoria alimpata mwenza sahihi ambaye alichagiza silka na utayari wa mama huyu kuzianza harakati za kupingana na mfumo dhalimu wa kibaguzi.
Yeye na mumewe Griffiths Mxenge, wakiwa ndani ya mapenzi motomoto ya maisha yao ya ndoa, walilazimika kuhama na kwenda kuishi KwaZulu-Natal. Hapa ndipo Bi Victoria alianza kuitumikia jamii yake kama tabibu (nurse) wa jamii ya wakazi wa Umlazi, lakini pia akihudumu kama mkunga katika hospitali ya King Edward. Sambamba na majukumu hayo, Bi. Victoria hakuacha kuitendea haki elimu kupitia kuongeza utaalamu mpya, na sasa alianza kusomea Sheria katika Chuo Kikuu cha Afrika ya Kusini (UNISA), huenda ilikuwa ni kutokana na ushawishi wa mumewe ambaye pia alikuwa Mwanasheria.
Waliitumikia jamii na kuyapa thamani maisha yao ambayo yaliacha alama ya uthamani wao ndani na nje ya jamii na taifa lao. Lakini kutokana na uthubutu, misimamo, na kukemea udhalimu wa tawala za kikoloni kupitia sera ya ubaguzi wa rangi, mumewe alijikuta matatani. Changamoto nyingi kati ya hizo zilikuwepo kuwekwa kizuizini, na kupewa marufuku na serikali ya kikaburu kutoendelea na harakati hizo.
Licha ya kashikashi hizo, Bi Victoria hakuacha kupigania haki za wanawake kutokana na sera kandamizi za kikoloni, pia haki za watoto ambao walikuwa wahanga wakubwa wa ukoloni. Haya yote yalimfanya mama huyu kutambulika kwa kasi na jamii zilizomzunguka, kiasi kwamba jamii ilizidi thamini mchango wake.
Familia yao haikupungukiwa vioja, ni mengi waliyapitia ikiwemo mumewe kufungwa katika gereza la Robben Island ambalo ni gereza mashuhuri sana lililotumiwa kuwafunga wanaharakati wengi wa kiafika. Mbali ya haya yote Novemba 1981, ambao ni mwaka wa kumi na tatu (13) wakiwa ndani ya ndoa; serikali ya kikaburu ilishindwa kuvumilia ukweli aliokuwa anaupigania Bwana Griffiths Mxenge kuhusiana na mateso na kubaguliwa kwa watu weusi, na hapo ndipo walipomuua.
Ni tukio lililowashtua watu wengi, hasa walioguswa na harakati za Griffiths Mxenge. Kwake Bi. Victoria pia lilikuwa ni jambo ambalo lilimuumiza sana, lakini kitu pekee ni kwamba alisimama kwa ujasiri kukabiliana na uongo ambao ulitungwa kwa makusudi kuhusu mauaji hayo. Tuhuma za mauaji hayo zilielekezwa kwa chama cha ANC, lakini mama huyu alipinga vikali na kuituhumu serikali ya kikaburu. Pingamizi lake lilikuja kuthibitika mwaka 1996 ambapo Jenerali Dirk Coetzee alikiri kuhusika.
Mbali na masaibu hayo, mama huyu hakuwahi kufikiria kuacha harakati zake. Kwa kiasi kikubwa baada ya kifo cha mumewe ndipo alipoongeza jitihada za kujishughulisha na masuala ya kisheria kwa kutetea jamii za watu wengi waliokosa msaada wa kisheria. Mwaka 1983 alifanikiwa kuwatetea wanafunzi ambao walidhurumiwa matokeo yao na Idara ya elimu kutokana na sababu za kibaguzi. Pia mchango wake wa kisheria ulionekana pale alipoingilia kati sakata la unyanyasaji wa watoto waliokuwa wamefungwa jela, na baadae kufanikiwa kutoa msaada wake kadri ya uhitaji.
Harakati zake zilizaa matunda na kuifanya nafasi yake kisheria kukua pia. Ndani ya chama cha United Democratic Front (UDF) ambacho mumewe alihudumu pia, Bi. Victoria aliongeza nguvu na kusimama thabiti akiwa Mhazini, na baadaye kuwa moja ya watu muhimu zaidi kwenye taasisi ya wanawake wa Natal yaani Natal Organisation of Women (NOW). Zaidi ya hapo, kwa kutambua thamani ya harakati zake, Victoria alipewa nafasi ya heshima kwa kuwa moja ya watu waliounda kamati ya kushinikiza Nelson Rholilala Madiba Mandela aachiwe huru kutoka gerezani yaani Release Nelson Mandela Committee (RMC).
Ukubwa na thamani ya harakati zake ulizidi shamiri, na kufanya awe kimbilio la watoto, wanawake, na watu wa jamii yake waliokosa faraja kutokana na matendo ya kikatili yaliyokuwa yakifanywa na serikali ya kikaburu. Hayo yote yalipelekea mnamo Julai, 1985 awe mmoja kati ya wazungumzaji wanaharakati kwenye mazishi ya vijana wanne (Matthew Goniwe, Fort Calata, Sparrow Mkhonto, na Sicelo Mhlauli) wa nchini Afrika ya Kusini maarufu kama "The Cradock Four" waliouawa na polisi wa ulinzi. Ndani ya hotuba yake mama huyu alielekeza tuhuma za mauaji kwa serikali ya kibaguzi na kuituhumu kuhusika na mauaji hayo, hakika hotuba yake ilimfungulia ukurasa mpya ambao uliacha alama isiyofutika milele.
Siku chache baada ya hotuba yake kuenea kwa kasi, mnamo tarehe Mosi, Agosti 1985 Bi. Victoria alivamiwa na kikundi cha wanaume wanne (watatu wenye asili ya kiafrika na mmoja mwenye asili ya kizungu, ambao wanadaiwa kuwa wanajeshi, na washirika wa mfumo wa kibaguzi) akiwa anarejea nyumbani. Hapo ndipo alipouawa kikatili mbele ya wanae, na hatimaye kuzikwa huko Rayi Cemetery pembezoni ya kaburi la mumewe.
Haikuwa rahisi kuaminika kama mama huyu kapotezwa napema kiasi kile, si kwa wananchi tu bali hata kwa wapigania uhuru wenzake akiwemo Nelson Rolihlahla Madiba Mandela na rafikiye Oliver Reginald Kaizana Tambo. Hakika kifo chake kiliacha simanzi kwa watoto, wanawake, wanafunzi, na jamii yote kwa ujumla nchini Afrika ya Kusini, na hata nje ya Afrika ambako harakati zake zilifika na kuwagusa watu. Kama ilivyokuwa kwa vifo vya wanaharakati wengi, kifo chake pia kiligubikwa na wimbi la upotoshaji wa sababu za kifo chake, mpaka mwaka 1987 ambapo Alias Bongi Raymond Malinga aliyekuwa askari wa ulinzi ndani ya serikali ya kikaburu kujitokeza hadharani na kukiri kutekeleza mauaji hayo.
Kufuatia heshima na mchango wa Bi. Victoria Mxenge nchini Afrika ya Kusini, mwaka 2006 yeye pamoja na mumewe walitunukiwa tuzo ya heshima ya Albert Luthuli ikiwa ni heshima ya mchango wao na jitihada za za kujitoa kwa manufaa na ukombozi wa nchi yao. Pia katika namna ya kuheshimu jitihada zake, Julai 2011 jijini Johannesburg kulianzishwa kundi la Mawakili na Wanasheria la Victoria Mxenge yaani The Victoria Mxenge Group of Advocates; lengo ikiwa ni kuheshimu jitihada za mama huyu ambaye naye pia alikuwa mwanasheria. Na kundi hili ndani ya katiba yao waliainisha kwamba wataziishi kanuni na misingi ya kiuanasheria kwa weledi mkubwa kama ambavyo BiVictoria alifanya. Lakini pia mwaka 2017 Agosti, 20 serikali ya KwaZulu-Natal kupitia manispaa ya eThekwini waliweka sanamu mbili za heshima, ikiwepo ya Griffiths Mxenge na Bi. Victoria Mxenge huko Umlazi, kusini mwa mji wa Durban ikiwa ni sehemu ya kuwakumbuka mashujaa hawa.
Afrika haina namna ya kueleza thamani na mchango wa shujaa huyu, isipokuwa kwa kuuishi ujasiri, utu, uzalendo, na uafrika wake uliothibitika kuleta jitihada za ukombozi wa bara letu. Nakupenda Victoria, Nakupenda Mama Afrika.
Picha kwa hisani ya Google.
#MakalazaHistoria #MashujaawaAfrika #NonyamelezoMxenge #Afrikanyumbani #Mporotowrites