SoC02 Vijana na Connections; Mahusiano na Uchumi

SoC02 Vijana na Connections; Mahusiano na Uchumi

Stories of Change - 2022 Competition

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Joined
Mar 24, 2018
Posts
28,297
Reaction score
68,017
MAHUSIANO NA UCHUMI.​

Imekuwa ni kiitikio cha taifa katika ule wimbo wa ukosefu wa ajira; “Connection! Connection! Hatuna connection” hiyo ni sehemu katika kiitikio cha taifa kwa vijana wa leo. Nani atawafuta vijana machozi? Nani atasikia kilio chao? Au machozi yao ni kama samaki majini! Na kilio chao ni kama kilio cha kinda mkiwa aliyeachwa na mamaye! Hakuna anayepinga kuwa bila ya connection hakuna kutoboa; uchumi imara unategemea zaidi mtu awe na connection lakini mtu atawezaje kupata connection pasipo kuwa na Mahusiano na mtoa connection? Robert ameingizwa kwenye ajira na Mjomba wake, Ahmed amepewa zabuni na Baba yake mdogo, Khadija ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya kisa ni mkwe wa Rais. Alex amepata kazi kwa sababu anaufaulu kwa mkubwa na ujuzi wa hali ya juu. Connection zote hizo hujengwa na mahusiano baina ya mtu na mtu, au mtu na kitu au jambo Fulani.

Mahusiano ndio uchumi wenyewe. Hakuna uchumi bila ya mahusiano kwani Uchumi unahusu zaidi uzalishaji, usambazaji, utumiaji na udhibiti wa rasilimali. Kuboresha mahusiano ni kuboresha uchumi wa eneo husika au mtu husika. Mahusiano ni namna ya muunganiko(Connection) kati ya mtu mmoja au kundi la watu na mtu mwingine au kundi au makundi mengine; Au muunganiko baina ya mtu na vitu au mambo Fulani.

Mahusiano mazuri huleta uchumi mzuri na imara. Mahusiano mazuri katika maeneo ya huduma mathalani huduma za kifedha kama Benki, huduma za mawasilianao, huduma za elimu kama shule huleta matokeo chanya, Mfano; Waalimu kama hawana mahusiano mazuri na wanafunzi wanaowafundisha huweza kuleta matokeo mabaya kama watoto kufeli masomo, wanafunzi kuathirika kisaikolojia, wakati mwingine wanafunzi kuichukia shule na kutoroka kama sio kucha kabisa shule. Makampuni na kwenye biashara mahusiano huzingatiwa kwa manufaa ya ukuaji na kupata wateja wengi katika biashara au kampuni husika.

Vijana wa sasa wanayohaja ya kuhakikisha wanajenga mahusiano mazuri maeneo waliyopo ili kupata connection ya fursa mbalimbali zilizopo ndani na nje ya nchi. Kwani kwa kujenga mahusiano mazuri kutawaimarisha zaidi uchumi. Kujenga Mahusiano hakuhitaji mtaji wa pesa bali kunahitaji nia na utayari wenye nidhamu na hekima ili kuleta matokeo bora.

Zifuatazo ni sehemu ya namna ya kujenga mahusiano bora;


Jenga, kuza na Safisha Jina lako

  • Jenga jina lako liwe bora na safi mbele ya jamii inayokuzunguka, jiepushe na sifa na tabia mbaya, jitahidi kadiri uwezavyo kuwa na tabia njema. Onyesha uwezo na ujuzi wako, jitangaze kadiri ya upatapo nafasi, hakikisha kila unachokifanya kinakuwa bora, kifanye kwa weledi wa hali ya juu. Kuza jina lako kwa kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii hapo mtaani, kanisani, msikitini. Kazi unayoifanya iwe ni yakujiajiri au kuajiriwa hakikisha unaifanya inakutambulisha jina lako. Hakikisha jina lako linakuwa kubwa kwa kufanya mambo chanya ndani ya jamii, Kadiri jina lako linavyokuwa na kuimarika ndivyo mahusiano yako na watu yanavyozidi kukua na kuimarika, hatimaye uchumi nao utajibu vyema. Huwezi pata connection kama watu hawakujui na kukutambua. Hili vijana wengi hawalijui.

Uaminifu na uadilifu
  • Mahusiano bora ambayo husababisha uchumi bora hujengwa na uaminifu na uadilifu. Makampuni na biashara nyingi huanguka kwa kukosa uaminifu na uadilifu, wafanyabiashara wote wakubwa wanaelewa kuwa uaminifu baina yao na wateja ndio msingi mkuu wa biashara. Watu wakishakujua wewe ni mwaminifu na muadilifu watakupa kazi kwani wanajua utafanya kadiri ya makubaliano yenu.
  • Watu wengi wanaogopa kuwapa watu mawazo ya biashara au connection za fursa kutokana na kutokuwa na imani na vijana. Heshimu watu, bila kujali mkubwa au mdogo, mwenye cheo au asiye na cheo. Usitumie Lugha chafu, vaa mavazi yenye heshima. Acha majivuno.

Shiriki shughuli za Kijamii.
  • Mahusiano hujengwa kwa watu kushirikiana, hata kama haushirikishwi wewe shiriki. Shughuli za kiserikali mfano siku za usafi jitokeze, shughuli za dini yako shiriki, sio uende kukaa au kutazama bali kuwa sehemu ya tukio, jipe kitengo hata kama ni kidogo, usikubali kukaa vivihivi, ukishiriki utashirikishwa wakati unaofuata. USIKUBALI KUKAA BUREBURE! Baada ya kujijenga jina lako ni muda sasa wa kuijenga jamii na nchi yako. Shiriki!

Penda kusaidia zaidi kuliko kusaidiwa!
  • Onyesha kwamba unakitu cha kusaidia jamii yako hata kama ni kidogo, hichohicho kitumie. Kadiri unavyosaidia ndivyo unavyoweza kujikomboa wewe na jamii yako. Usijidharau! Kujidharau kunaharibu mahusiano yako na wengine. Mtu anayejidharau hawezi kuwa na mahusiano bora. Kama huna mali basi saidia kwa nguvu na hali. Hiyo inajenga mahusiano. Zingatia mahusiano ndio uhcumi wenyewe.
  • Kadiri mtu anavyokosa mahusianao mazuri na watu ndivyo anajiweka katika hatari ya kuzorota kwa uchumi wake mwenyewe. Kila mtu anakitu ambacho anaweza kukitumia kusaidia wengine.

Heshimu maamuzi na uhuru wa wengine.
  • Kila mtu anauelewa na mtazamo wake kadiri na jinsi alivyo, Kama ilivyo kwa kila nchi ina sheria na tamaduni zake. Heshimu maamuzi na uhuru wa watu wengine hii itaboresha mahusiano yenu. Hii ni kusema usivuke mipaka yako ukaingilia mpaka wa mwenzako. Unaouwezo wa kushauri lakini sio kumuamulia mtu maisha! Huko kunaitwa kuheshimiana.
Unaweza anzisha mradi au biashara yoyote utakavyo lakini mahusiano yako na watu wanaokuzunguka ndio yataamua biashara hiyo idumu au ife. Unaweza kupata kazi nzuri yenye kipato kizuri lakini mahusiano yako na mwajiri au wafanyakazi wenzako ndio yataamua uendelee kubaki kwenye ajira au ufukuzwe kazi. Moja ya sababu kubwa za watu kufukuzwa kazi au biashara kufa ni mahusiano mabovu.

Mahusiano ya kiuchumi baina ya nchi na nchi ambapo yanahusu muunganiko na muingiliano wa baadhi ya shughuli kama biashara za bidhaa na huduma, mawazo(Ideas), sera, sayansi na teknolojia miongoni mwa mambo mengine huweza kuboresha maisha ya wananchi wa nchi husika. Kadiri nchi inavyokuwa na mahusiano mazuri na nchi zingine inajiweka katika nafasi nzuri ya kunufaika kimaendeleo.

Utawala bora, sera nzuri za kidiplomasia, kiuchumi na kifedha zenye mwelekeo wa kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji, uzingatiaji wa uhuru na haki za binadamu, ushirikiano wa nchi na jumuiya za kimataifa katika majanga yanayoikabili dunia, miongoni mwa mambo mengine hukuza Mahusiano bora baina ya nchi yetu na mataifa mengine ambapo taifa na watu wake hunufaika kiuchumi.

Ni wito wangu; Kwa vijana ambao ndio nguvu kazi ya nchi, kuhakikisha wanaimarisha mahusiano mazuri kwa ajili ya manufaa yao kiuchumi; kwani Mahusiano ndio Uchumi wenyewe. Hii itapunguza kama sio kuondoa kabisa tatizo la Ajira nchini.

Shukrani sana na niwakaribishe kwa Mjadala
 
Upvote 6
Back
Top Bottom