SoC01 Vijana tukijitambua jamii itatuheshimu na kutuwezesha

SoC01 Vijana tukijitambua jamii itatuheshimu na kutuwezesha

Stories of Change - 2021 Competition

Gnyaisa

Member
Joined
Jul 13, 2021
Posts
23
Reaction score
24
Katika kitabu kitakatifu cha Biblia kuna simulizi maarufu ya safari ya wana wa Israeli kutoka uhamishoni Misri kuelekea katika nchi waliyoahidiwa na Mwenyezi Mungu. Nchi iliyokuwa na kila aina ya neema na furaha, yenye kutirirsha maziwa na asali masaa yote! Simulizi ile inaelezea jinsi wana wale wakiongozwa na Nabii Musa walivyojikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuzungukwa na majeshi ya Farao huku mbele yao wakitazamana na bahari ya Shamu. Wote kwa pamoja walianza kumnung’unikia Musa kwa kuwatoa utumwani kwa lengo la kuwaua pale Jagwani kwani ni dhahiri wangeuawa na majeshi ya Farao. Musa, pamoja na kuwatia moyo wenzake naye hakujua afanye nini na kujikuta akianza kulia na kumnung’unikia Mungu! Kisa hicho kinaendelea kwa Mungu kumshangaa Musa ilhali alikuwa na jawabu la mtihani ule mkononi mwake. Alimuamuru anyooshe fimbo yake na kupiga bahari na baada ya kufanya hivyo maji ya bahari yaligawanyika katikati na wao kupita.

Nikiitazama jamii ya vijana katika taifa letu sioni tofauti yao na kisa hiki cha wana wa Israeli. Ni jamii inayoishi katika nchi yenye kila sifa ya kuwa taifa la ahadi lakini imedumaa katika lindi la umaskini. Tuna misitu tele na maua mazuri yenye kuvutia nyuki wa kila aina lakini tumeshindwa kutiririsha asali, tuna mifugo mingi inayotufanya kuwa taifa la pili barani Afrika kwa wingi wa mifugo hiyo baada ya Ethiopia lakini tumeshindwa kuwa na mabomba ya kutiririsha maziwa. Tumezungukwa na maji kila kona ya taifa letu lakini tunakufa kwa kiu. Tuna nguvukazi kubwa inayofikia Zaidi ya asilimia 65 ya watu wote lakini jirani zetu wanakumbwa na baa la njaa kila kukicha. Tanzania ni taifa la maajabu!

Wana wale walimnung’unikia Musa kwa sababu ni Musa ndiye aliyekiri kuijua njia na kwamba Mungu alimtokea na kuahidi kumuongoza. Kitendo cha wao kujikuta ufukweni mwa bahari huku kukiwa hakuna matumaini yoyote ya kusonga mbele kilizua wasiwasi kwa umati ule wa watu. Hata hivyo, Musa alidhihirisha unabii wake kwa kuwawezesha wana wale kuvuka na hatimaye jeshi la Farao kuangamia.

Musa wa zama hizi anayepaswa kuwakomboa watanzania kutoka katika utumwa wa ujinga, umaskini na maradhi ni MSOMI. Huyu ni mtu aliyepewa “unabii” wa kusomea na kujengewa uwezo madhubuti wa kupambana na changamoto mbalimbali za maisha. Amepewa fimbo (ELIMU) yenye uwezo wa ajabu. Fimbo hii imepewa uwezo wa kugawanya maji ya bahari yoyote ya umaskini. Bahati mbaya jamii imelazimishwa katika kuamini kwamba Musa wao ni serikali! Tofauti kubwa kati ya Musa wa kwenye Biblia na Musa tuliyenae Tanzania ni kwamba huyu wa pili amekwepa majukumu yake na kuishia kuinung’unikia serikali bila kuchukua hatua zozote za mapambano. Ameishia kushikilia fimbo na kushindwa kuyapiga maji licha ya kuamriwa kufanya hivyo!

Ni mara ngapi tunawaona wasomi wetu wakiilalamikia serikali kutowatengea maeneo maalum ya kilimo ilhali wote wamejazana mijini? Si kwamba vijana hawa wangerudi kwanza vijijini ndipo wailalamikie serikali kutowafuata? Hivi wasomi hawa wanajua kuwa kila halmashauri inapaswa kutenga asilimia 5 ya mapato yake kwa ajili ya maendeleo ya vijana na kwamba asilimia hiyo haitengwi kwa sababu vijana katika halmashauri hizo wamekosa Musa (Msomi) wa kuwaongoza na kuwapigania? Ni mara ngapi tunawasikia wasomi hawa wakiilalamikia serikali kutowapa mitaji ya kujiajiri ilhali marafiki zao waliomaliza vyuo na kubahatika kupata ajira wakiishia kuchukua mikopo ya magari na kushinda baa wakitumbua mishahara? Haiwezekani wasomi hawa kutumia “fimbo” yao kuwashawishi wenzao hawa kuchukua mikopo ya biashara na kuitumia kama mitaji kwa makubaliano maalum ya ubia? Wakala wa Umeme vijijini (REA) wanaendelea kusimika nguzo za umeme maeneo mbalimbali ya vijiji vya Tanzania na tayari vijiji kadhaa vimeshaanza kunufaika na umeme huo. Ni dhahiri kwamba asilimia 90 ya matumizi ya umeme huo yataishia katika kuwashia taa na kusikiliza muziki badala ya kuwa chanzo cha mapinduzi ya viwanda vidogovidogo vya kusindika mazao na vyakula. Wasomi wetu wako wapi katika kuchangamkia fursa hii na kusaidia mazao ya wakulima wetu yasiozee mashambani? Ni dhahiri kwamba akina Musa hawa wamejifungia majumbani kwao wakiisubiri serikali ijenge viwanda kisha wajitokeze na vyeti vyao vyenye kuonesha ufaulu mkubwa darasani!

Lengo la Makala haya si kuwashambulia vijana wenzangu au kuitetea serikali kwa namna yoyote ile bali kuwahimiza kuhusu kujitambulia na kuachana na lawama zisizokwisha. Haiingii akilini kwa kijana mwenye uwezo wa kufikiri vema na anaeishi katika taifa lililojaa fursa tele na utulivu mkubwa wa kisiasa kuwa na kilio kinachofanana na vijana wenzake wa mataifa ya mashariki ya kati wanaoogelea katika dimbwi la vita kila kukicha. Vijana tukijitambua jamii itatuheshimu na kutuwezesha.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom