SoC02 Vikwazo vya kupata elimu bora vijijini

SoC02 Vikwazo vya kupata elimu bora vijijini

Stories of Change - 2022 Competition

Muhcienn Jr

Member
Joined
Aug 3, 2022
Posts
5
Reaction score
3
Ikisiri
Lengo la makala haya ni kudhihirisha kwa uwazi vikwazo mbalimbali ambazo hukabiliana nazo wanafunzi hususani wa maeneo ya vijijini katika kupata elimu iliyo bora. Wapo waandishi wengi tofautitofauti ambao wametoa machapisho mbalimbali yanayojadili swala hili, vilevile wapo wadau wa elimu pia wamepaza sauti kuhusiana na swala la elimu na changamoto zake. Lakini wengi wao huzungumzia changamoto hizo kwa ujumla, yaani mijini na vijijini ambapo hupelekea kutotoa changamoto kwa undani zaidi. Ila makala haya yatajitika kutoa changamoto zinazowakabili wanafunzi wa vijijini pekee na kujaribu kutoa ushauri nini kifanyike ili kutatua changamoto hizo. Mbinu ya ushuhudiaji imetumika katika kupata data mbalimbali za makala haya.

UTANGULIZI
Elimu
kwa maana pana ni tendo au uzoefu wenye athari ya kujenga akili, tabia ama uwezo wa kimaumbile wa mtu binafsi. Katika dhana ya kiufundi, elimu ni njia ambayo hutumiwa makusudi na jamii kupitisha maarifa, ujuzi na maadili kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine. Hivyo elimu bora kwa ujumla ni ile inayozingatia hali ya wanafunzi, mazingira ya kujifunzia, mambo yanayofundishwa darasani, ubora wa walimu na ufundishaji mzuri.

Nchini Tanzania hasa maeneo ya vijijini hukumbwa na vikwazo mbalimbali kwenye swala la kupata elimu bora. Wanafunzi wengi hushindwa kufikia malengo yao kutokana na sababu mbalimbali ambazo kwa namna moja au nyingine huwa ngumu kukabiliana nazo pindi wanapotafuta elimu. Makala haya yatabainisha kwa ujumla changamoto ambazo hukumbwa nazo wanafunzi wa maeneo ya vijijini katika kupata elimu bora. Vilevile tutapemdekeza njia mbalimbali ambazo pindi zitakapochukuliwa zinaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto hizo.

Malengo ya Makala
Sehemu hii itahusisha malengo ya makala haya kama ifuatavyo;
(i) Kudhihirisha vikwazo vya kupata elimu bora vijijini.
(ii) Kubainisha njia mbalimbali zinazoweza kutatua vikwazo hivyo

VIKWAZO VYA KUPATA ELIMU BORA VIJIJINI
Makala haya yatajadili kwa undani vikwazo mbalimbali ambazo hukabiliana nazo wanafunzi hususani wa maeneo ya vijijini katika kupata elimu iliyo bora. Vikwazo hivyo kama vifuatavyo;

Uchache wa Watumishi (Walimu)
Licha ya serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Ofisi ya Waziri ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutoa ajira za watumishi wa elimu zipatazo 9800 mwaka huu wa 2022 na kuwatawanya watumishi hao mikoa na wilaya zote Tanzania nzima, lakini kiuhalisia idadi ya watumishi hao imekuwa finyu kwa sababu ya kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi mashuleni. Na ukizingatia watumishi wengi hupendelea kufanya kazi mijini kuliko vijijini licha ya serikali kufanya juhudi kuwapeleka vijijini lakini walimu hao uhamia mijini na kupelekea kuwa na walimu wachache katika shule za vijijini, kwa mantiki hiyo wanafunzi wa shule za vijijini hukosa elimu iliyo bora. Kwa mfano, katika shule ya msingi Mkamba iliyopo wilayani Mkuranga mkoa wa Pwani, shule nzima haizidi walimu 8 hivyo elimu inayotolewa haiwezi kuwa bora kwa idadi ya walimu hao kwa shule nzima. Ambapo baadhi ya watumishi wa shule hiyo hiyo kuwapeleka watoto wao shule za mijini zenye idadi nzuri ya watumishi ili kupata elimu iliyo bora.

Uelewa Duni Juu ya Umuhimu wa Elimu
Wizara ya elimu ikishirikiana maafisa elimu mkoa, wilaya na kata zinajitahidi kwa kiasi kikubwa kuelimisha jamii juu ya swala zima la elimu. Lakini katika maeneo ya vijijini bado kuna shida kubwa kwa wazazi, walezi na hata watoto wenyewe kuelewa manufaa ya elimu licha ya waelimishaji kutoa elimu. Hii inapelekea kukosa kiunganishi kizuri kati ya wazazi na walimu shuleni ambapo hupelekea wanafunzi kutofanya vizuri katika masomo yao. Kwa mfano, katika maeneo mengi ya vijijini katika siku za shule wazazi au walezi huwazuia watoto kwenda shuleni ili kwenda kushiriki kazi za kilimo, uchungaji na kazi nyingine mbalimbali. Hii humdidimiza mwanafunzi kielimu na kupelekea kukosa elimu iliyo bora.

Umbali Mrefu Zinapopatikana Shule Ikiambatana na Usafiri Duni
Licha ya serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa na mpango wa kujenga shule kwenye kila kata, hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwenye ngazi ya shule za msingi ambazo zipo kwenye kila kata. Japokuwa hazijajitosha kwa asilimia mia moja lakini mpango huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Lakini kwa upande wa shule za sekondari, hapo ndipo kuna changamoto kubwa sana kwenye maeneo ya vijijini kwa sababu ya uchache wa shule ambapo hupelekea wanafunzi kutoka kijiji kimoja kupita vijiji kadhaa ili kufika shuleni. Yapo maeneo mengi ya vijijini nchini Tanzania yanakumbwa na kadhia hiyo mfano katika wilaya ya Mkuranga kata ya Mkamba, wapo wanafunzi wanatembea zaidi ya kilomita 10 kutoka kijiji cha Chamgoi kwenda kijiji cha Kizomla ambapo shule ya sekondari ndipo ilipo. Wanafunzi wanalazimika kutembea kwa miguu kwa sababu hakuna usafiri wenye kueleweka, hivyo mara kwa mara hupelekea kuchelewa vipindi vya asubuhi. Kwa kadhia hii wanafunzi lazima wasipate elimu iliyo bora kutokana na ugumu wa mazingira yaliyopo.

Unyanyasaji wa Kijinsia
Unyanyasaji wa kijinsia upo Tanzania nzima lakini mijini sio kwa kiasi kikubwa kama vijijini kwenye swala la elimu. Wanafunzi wengi huko vijijini hasa wa jinsia ya kike hukumbwa na unyanyasaji wa kijinsia katika sura tofauti tofauti. Kwanza, bado wapo wazazi na walezi ambao huona ni hasara kubwa kuwasomesha watoto wa kike kwa sababu wanahofia kupoteza gharama zao. Wazazi au walezi wanaamini watoto wao wa kike hawana haki ya kupata elimu ya juu zaidi kulingana na mrejesho wanaoupata kutoka kwa watoto wengine wa kike walioendelea. Hii hupelekea mzazi au mlezi kumkatia tamaa mtoto wa kike na kuweka nguvu zaidi kwa mtoto wa kiume, huu ni unyanyasaji. Pili, vishawishi vimekuwa vingi kwa wanafunzi wa kike ambavyo hupelekea kukatishwa masomo yao kwa kupata ujauzito. Unyanyasaji unakuja pale ambapo wanaowapa mimba kutochukuliwa hatua. Wanafunzi wa kike wanapopata ujauzito wazazi na walezi hawamchukulii hatua aliyempa ujauzito na badala yake wazazi wa pande zote mbili hukaa na kuelewana kifamilia na sio kisheria. Kwa hakika hii hudidimiza ubora wa elimu kwa kiasi kikubwa.

Umasikini
Kwa kuliona hilo, serikali imekuja na TASAF mpango wa kuinua kaya masikini kiuchumi. Na mpango huu kwa kiasi kikubwa unawahusu wananchi walio katika hali ya chini kiuchumi waishio vijijini. Pia serikali ilianzisha utaratibu wa elimu bila malipo ili kuwawezesha wanafunzi wote wa hali ya juu na ya chini kupata elimu. Lakini mipango yote ya serikali ya TASAF na elimu bila malipo haikusaidia kwa asilimia mia moja kwa wanafunzi wanaotoka kwenye kaya masikini kupata elimu bora na sio bora elimu. Wanafunzi wanaenda shule na kurudi bila ya kutia kitu chochote mdomoni, hii inapunguza kasi ya uelewa wa mtoto kwa sababu ya njaa.

Na shule nyingi za vijijini hazina utaratibu wa chakula shuleni kwa wanafunzi kwa sababu wazazi au walezi wanashindwa kuchangia kutokana na hali ngumu ya maisha. Vilevile umasikini huu hupelekea wanafunzi kutofanya vizuri kwenye mitihani yao kwa kuhofia pindi atakapofaulu nani atamsomesha na ukizingatia nyuma ya mwaka huu wa 2022 elimu ya sekondari ya kidato cha tano na sita ilikuwa na malipo. Niliwahi kumsikia binti mmoja jina lake na shule aliyosoma sitotaja hadharani. Binti huyo alisema, "mama kanambia nisifaulu hana uwezo wa kunisomesha". Na matokeo yalivyotoka hakufaulu kweli. Binti huyo alikuwa anaishi na mama yake tu kwenye mazingira magumu. Hivyo ilipelekea kukatisha ndoto zake kutokana na umasikini.

NJIA MBALIMBALI ZINAZOWEZA KUTATUA VIKWAZO HIVYO
Makala haya pia yataangazia na kubainisha njia stahiki ambazo pindi zitakapochukuliwa vikwazo hivyo ambavyo hukabiliana navyo wanafunzi hususani wa maeneo ya vijijini zitapungua kwa kiasi kikubwa kama sio kuisha kabisa. Njia hizo ni kama zifuatazo;

Kuongeza Idadi ya Walimu Ili Kwenda Sambamba na Uwingi wa Wanafunzi.
Uwingi wa wanafunzi sio mijini tu pia hata vijijini wapo wanafunzi wengi sana. Na ukizingatia watumishi wengi hawapendi kufanya kazi maeneo ya vijijini na kupendelea mijini pekee, hii huchangia kwa kiasi kikubwa kuwa na idadi ndogo sana ya walimu vijijini. Endapo serikali itakuja na mpango mzuri wa kuajiri walimu wa kutosha na kuwasambasa Tanzania nzima hasa vijijini, sina shaka kila somo litapata walimu wa kutosha watakaokuwa na uwezo wa kufundisha na kufuatilia uelewa wa wanafunzi kwa ukaribu zaidi. Walimu wakiwa wa kutosha watatoa elimu iliyo bora kwa manufaa ya wanafunzi.

Kuelimisha Jamii Juu ya Faida ya Elimu kwa Watoto
Semina na warsha mbalimbali zinazohusu faida ya elimu zinahitajika sana maeneo ya vijijini. Licha ya wadau wa elimu kuelimisha lakini bado wanahitajika kutoa elimu zaidi kwa wanajamii kuhusu faida ya elimu. Bado wananchi wa vijijini ambao wapo kwenye giza zito la kutofahamu faida ya elimu, hao ndio humzuia mtoto kwenda shule ili kushiriki kazi za uzalishaji ikiwemo kilimo, uchungaji wa mifugo na kazi nyinginezo. Ikiwa elimu itatolewa vizuri kwa watu wa aina hiyo basi itachangia kwa kiasi kikubwa watoto kuhudhuria shule bila kukosa.

Kusisitiza Juu ya Kufata Sheria Pindi Tatizo Linapotokea
Jamii nyingi za vijijini hazifuati sheria pindi panapotokea tatizo kwa wanafunzi, hususani wanafunzi wa kike wanapopata ujauzito. Hatua kubwa wanayoifanya ni kukaa na kuzungumza kifamilia. Jambo hili huwa halimalizi tatizo kwa sababu hakuna hatua yoyote ya kisheria inayochukuliwa, hupelekea wanafunzi wengi kupata ujauzito na kukatishwa masomo yao. Serikali yapaswa kuwasisitiza wananchi kufuata sheria pindi tatizo linapotokea ili kukomesha tatizo hilo.

Kuandaa Mpango Kazi Kabambe Utaoweza Kuwasaidia Wanafunzi Wanaotoka Katika Kaya Masikini Kutokatisha Ndoto Zao.

Mpango wa elimu bila malipo pamoja na TASAF bado haitoshi katika kuwasaidia wanafunzi wanaotoka katika familia masikini kupata elimu bora na kutokatisha ndoto zao. Licha ya kuwepo elimu bure lakini shule zilizo nyingi bado ipo michango mingi sana ambayo kwa namna moja au nyingine wanaotoka kwenye kaya masikini watashindwa tu.

Serikali ikishirikiana na wadau wa elimu ni vyema wakaanzisha mpango mzuri kama uliopo katika vyuo vikuu. Vyuoni kuna mikopo ambayo inamwezesha mwanafunzi kujikimu kwa kila kitu ikiwemo ada, chakula na malazi. Hii inapelekea kuwa rahisi kwenye usomaji wa mwanafunzi husika. Lakini kuanzia shule za msingi mpaka sekondari bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuwasaidia wanafunzi wanaotoka kwenye kaya masikini kuziishi ndoto zao.

Kusogeza Huduma Karibu Ili Kupunguza Wanafunzi Kutembea kwa Muda Mrefu
Ili kupata elimu iliyo bora, wanafunzi lazima wapate utulivu wa kila kitu. Wapate utulivu wa akili na wa mwili. Endapo mwanafunzi atatembea kwa umbali mrefu kwenda shule hapo kitu kimoja atakikosa ambacho ni utulivu wa mwili. Kwanza hatofika shule muda sahihi kwa maana atachelewa baadhi ya vipindi vya asubuhi, na pindi anapofika shule mwili utakuwa na uchovu kutokana na kutembea na hapo hupelekea kukosa utulivu wa akili. Kwa mantiki hii mwanafunzi hawezi kupata elimu iliyo bora. Sekta ya elimu yapaswa kuwaangalia wanafunzi hawa kwa kuwasogezea karibu huduma kwa maana shule zijengwe karibu na wanafunzi ili waweze kupata utulivu wa akili na mwili ili waweze kupata elimu iliyo bora.

HITIMISHO
Licha ya swala la elimu nchini Tanzania kuwa na vikwazo vingi lakini ufaulu wa wanafunzi kutoka ngazi moja kwenda ngazi nyingine pia umeongezeka kwa kiasi kikubwa. Idadi ya wanafunzi wanaotoka shule ya msingi kwenda sekondari inaongezeka na kutoka sekondari kwenda vyuoni pia inaongezeka, hili kama nchi ni jambo la kujivunia sana. Kutokana na ufaulu huo kuna wimbi kubwa la wahitimu wapo mitaani wakiwa hawana ajira yoyote, hivyo serikali inatakiwa kutathmini na kufanya mabadiliko ya mtaala wa zamani na kuanzisha mtaala mpya wenye kuendana na mazingira yaliyopo ili wanafunzi wakishahitimu iwe rahisi kujiajiri na sio kusubiri kuajiriwa.

Mwandishi; Omary Muhsini (0677301368/0621614300)
 
Upvote 1
Back
Top Bottom