Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefanya ziara ya kikazi nchini Comoro kwa mwaliko wa Jeshi la Comoro, ikiwa ni hatua ya awali ya kuanzisha ushirikiano wa kimkakati katika kuboresha huduma za afya visiwani humo, hususan hospitali ya jeshi.
Ziara hiyo iliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Dkt. Delilah Charles Kimambo, ambapo ujumbe huo ulifanya mikutano ya kitaalam, kutembelea miundombinu ya hospitali ya jeshi na kukagua hali ya utoaji wa huduma za afya pamoja na maeneo yanayohitaji kuboreshwa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Kimambo ameelezea utayari wa hospitali hiyo kushirikiana na Hospitali ya Jeshi la Comoro katika kuboresha mifumo ya uendeshaji wa hospitali, kuimarisha rasilimali watu kupitia mafunzo pamoja na kusaidia katika uanzishaji wa huduma za kibingwa ambazo kwa sasa hazipatikani nchini humo.
Soma pia:
Kampuni za Tanzania zahimizwa kuchangamkia zabuni Comoro
Ziara hiyo imeratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro huku ikitarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa sekta ya afya na kuimarisha uhusiano wa kindugu na kimkakati kati ya Tanzania na Comoro.