Vipi iliundwa TANU na nani waliunda TANU 1954?

Vipi iliundwa TANU na nani waliunda TANU 1954?

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
VIPI ILIUNDWA TANU NA NANI WALIUNDA TANU 1954?

Nimeulizwa swali hilo hapo juu katika group moja.

Swali nimelifanyia uhariri kidogo ili mada ikae vyema.

Jibu la swali hili ni hili hapa chini:

Nitakupa jibu kwa muhktasari.

Kuna waraka wa Kleist Sykes Secreatary African Association wa mwaka wa 1933 akimwandikia Mzee bin Sudi aliyekuwa President wake.

Katika waraka ule Kleist alianza kuandika kwa maneno haya: "Bismillah Rahman Rahim."

Katika maneno mengi aliyosema mwisho aliandika kuwa juhudi hizi wanazofanya lazima wazifikishe mwisho na kama wao hawatafanikiwa basi hao watakaokuja baadae wafanikishe kuitoa Tanganyika kwenye mikono ya wakoloni.

Waraka huu upo katika mswada wa kitabu alichoandika Kleist Sykes kabla hajafariki mwaka wa 1949 na alimwachia mwanae Abdul kwake ukawa kama usia.

Abdul Sykes alipokuwa Burma WWII (1939 - 1945) aliwakusanya askari wenzake katika 6th Battalion kutoka Tanganyika na kuwaambia wao ndiyo watakuwa msingi wa kuunda TANU wadai uhuru wa nchi yao.

Waliporudi Tanganyika mwaka wa 1945 wakaikuta African Association iko mikononi mwa wazee na hapakuwa na dalili ya mabadiliko.

Mwaka wa 1950 Abdul Sykes na Hamza Mwapachu wakaupindua uongozi wa Thomas Plantan akiwa TAA President na Clement Mtamila Secretary.

Waingereza hawakukubali hili wakatoa amri uitishwe uchaguzi.

Uchaguzi ukafanyika mwaka wa 1950 Dr. Vedasto Kyaruzi akawa President na Abdul Sykes Secretary nafasi ile ile iliyokuwa ikishikwa na baba yake kwa miaka mingi.

Mwaka huo wa 1950 Abdul akaunda Political Subcommittee ndani ya TAA kazi kubwa ikiwa kutayarisha mipango ya kuigeuza TAA kuwa chama kamili cha siasa kudai uhuru.

Pamoja na haya wakafanikisha safari ya Japhet Kirilo na Earle Seaton kwenda UNO mwaka wa 1952 katika madai ya mgogoro wa ardhi ya Wameru.

Wajumbe wa kamati hii walikuwa Vedasto Kyaruzi, Abdul, Hamza Mwapachu, Mufti Sheikh Hassan bin Ameir, Sheikh Abdallah Chaurembo, Steven Mhando na John Rupia.

Waingereza waliona mwelekeo huu mpya wa TAA wakatishika wakatoa onyo kupitia Government Circular kadhaa kuhusu TAA kujiingiza katika siasa na wakawahamisha Dar es Salaam Mwapachu, Dr. Kyaruzi na wazalendo wengine wengi.

Baada ya kuondoka Dr. Kyaruzi Abdul akawa Act. President na Secretary na akaanza mazungumzo na Chief David Kidaha Makwaia amlete TAA wamchague kuwa President waunde TANU na Chief Kidaha aongoze harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.

Mazungumzo haya hayakufanikiwa.

Chief Kidaha alikuwa msomi wa Oxford, Mwapachu University of Wales na alikuwapo Dr. Wilbard Mwanjisi aliyehitimu udaktari Makerere.

Kwa miaka kama mitatu Abdul akawa amekwama katika azma ya kuunda TANU lakini alikuwa na mshauri hodari na rafiki yake Earle Seaton mtu mweusi kutoka Bermuda na mwanasheria aliyemsaidia sana katika kusukuma mambo serikalini kwa Gavana Edward Twining na UNO.

Hiki ndicho kipindi Abdul alipojaribu kuunganisha harakati za TAA na KAU kwa kukutana na Jomo Kenyatta na wenzake akina Bildad Kaggia, Achieng Oneko, James Mbiu Koinange na Kung'u Karumba, Nairobi katika mkutano wa siri.

Lakini Hamza Mwapachu yeye akijuana na Julius Nyerere toka Makerere na walikuwa pamoja katika uongozi wa TAA Tabora mwaka wa 1948.

Nyerere alipokutana na Abdul Dar es Salaam mwaka wa 1952 ikawa Abdul kapata mwenzake waliokubaliana katika fikra zao.

Hamza Mwapachu na alimweleza Abdul kuwa Nyerere angefaa sana kutiwa katika uongozi wa juu wa TAA.

Uchaguzi wa TAA ulikuwa unakaribia mwezi April 1953. Abdul na Ali Mwinyi Tambwe Secretary wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika) wakaenda Nansio Ukerewe ambako Mwapachu alikuwa amehamishiwa, kupata kauli yake ya mwisho kuhusu kumuingiza Julius Nyerere katika uongozi wa TAA kama President katika uchaguzi uliokuwa mbele yao.

Hamza alielekeza kuwa Nyerere aingizwe katika uongozi na Abdul amsaidie kupata nafasi ile.

Mbali na sifa na uwezo ambao Hamza akiujua aliokuwanao Nyerere, Hamza alisisitiza kuwa Nyerere kama Mkristo katika kudai uhuru ataondoa hofu ya kuwa hizi ni harakati za Waislam peke yao.

Tarehe 17 April 1953 Nyerere alipambana na Abdul Sykes katika uchaguzi wa TAA Ukumbi wa Arnautoglo Hall.

Julius Nyerere akachaguliwa kuwa President na Abdulwahid Sykes Vice President.

Mwaka wa 1954 TANU ikaundwa.

Ni bahati mbaya sana kuwa katika uhai wake wote Nyerere hakupata kueleza historia yake vipi alipokelewa na Abdul Sykes na nduguye Ally na vipi kupitia kwa Abdul akajuana na wote waliokuwa katika harakati za kudai uhuru mfano wa Dossa Aziz, Mufti Sheikh Hassan bin Ameir, Sheikh Suleiman Takadir, Mshume Kiyate, John Rupia na wengine wengi na vipi ikapangwa mipango ya safari ya UNO mwaka wa 1955 mwaka wa pili tu baada ya kundwa kwa TANU nk. nk
 
Angalia picha:

Abdul na Ally Sykes Burma Infantry 6th Battalion, Jomo Kenyatta na Abdul Sykes, Julius Nyerere na Dossa Aziz.
Screenshot_20200531-082641.jpg
IMG-20200515-WA0145.jpg
Screenshot_20200510-090328.jpg
Screenshot_20200520-063442.jpg
 
Back
Top Bottom