Janeth Kahama: Sophia Simba alinirushia makonde
2008-09-16 11:46:43
Na Simon Mhina
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake ya Chama cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Dar es Salaam, Janeth Kahama, amedai kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba, alimrushia makonde kwenye kikao cha Kamati ya Siasa na kwamba haukuwa ugomvi mdogo wa maneno kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari jana.
Mwenyekiti huyo wa UWT Mkoa wa Dar es Salaam, amesema kutokana na kitendo hicho, amemshitaki Waziri Sophia Simba kwa Rais Kikwete pamoja na kwenye vikao vya Chama.
Akizungumza na Nipashe jana, Janeth alisema mbali na Sophia kumtamkia maneno makali yasiyo na idadi, alidiriki kumkunja na kumrushia makonde kadhaa kabla hajakamatwa na watu.
``Alitaka kunidhuru, nilikuwa katika wakati mgumu, maana hata wanaume na nguvu zao walipomshika asije kuniumiza, bado aliwasukumiza,`` alisema mwenyekiti huyo, ambaye anatarajia kuchuana na Waziri Simba katika kinyang\'anyiro cha uenyekiti wa Taifa wa UWT katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba.
Alipoulizwa kama anawakumbuka wajumbe waliomuokoa katika sakata hilo ni kina nani, Jeneth alisema haikuwa rahisi kuwakumbuka kwani kuna wakati aliserereka na kabla hajaanguka, hajui nani alimdaka.
``Katika hali hiyo huwezi kukumbuka jina wala sura ya mtu, nilichokumbuka mimi ni msalaba,`` alisema.
Alisema baada ya kuona mwenzake (Sophia) amezidi kuwaka hasira huku hali ikizidi kuwa mbaya ukumbini, alichokumbuka ni kukimbilia msalabani na kufanya maombi na kukemea roho ya ugomvi.
Alisema anamsgukuru Mungu, kwani hadi sasa anayo amani ya kutosha na kwamba hana kinyongo na mtu yoyote. ``Nampenda sana Sophia, sina kinyongo naye,`` alisema.
Hata hivyo alisema amekusudia kumfikisha mbele ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na kwenye vikao vya Chama.
``Siwezi kumlaumu wala kusema barabarani kama alivyosema, mimi nitamfikisha kwenye vikao vya maadili, ndivyo taratibu zetu zinavyosema,`` alisema.
``CCM hakuna jela, kwamba nikimpeleka huko atafungwa, lengo nikuhakikisha anapata nafasi ya kutoa madai yake,`` alisema. Hata hivyo, alikana kumhujumu Sophia kwa kutomwalika kwenye vikao vya UWT kama ilivyodaiwa.
Kwa upande wake, Waziri Sophia alililiambia Nipashe jana kuwa haogopi. ``Kama anakwenda kushitaki anayo haki ya kufanya hivyo, akashitaki tu,`` alisema.
Hata hivyo, Sophia alisema na yeye anayo malalamiko dhidi ya Janeth na atayafikisha kwenye Chama. ``Namimi pia nina malalamiko kwake, mengi sana tena mazito, hata mimi nitamshitaki,`` alisema.