Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,771
- 41,027
Mungu ni Mungu wa wote. Hana upendeleo na hajali sura, hali, au mahali pa mtu. Wema wake na uaminifu wake ni wa milele. Niandikapo hili nimejawa na huzuni kwani siku chache zilizopita nimepokea taarifa ya kifo cha Padre Pierluigi Dell’Amico kilichotokea huko Trento, Italy Machi 15, 2020 baada ya kuambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona – Covid – 19.
Fr. Angelico alikuwa ni mtawa wa Shirika la Ndugu Wadogo Wafransiskani Wakapuchini (OFM Cap.) lililoanzishwa na Mt. Fransisco wa Assisi mwaka 1525. Alipoanza kazi yake ya umisionari Tanzania Pd. De’ll Amico alijulikana kwa jina moja tu la Fr. Angelico. Ilikuwa rahisi kutamkika na rahisi kuandikika kwa sisi wengine.
Fr. Angelico alikuja Tanzania miaka ya sabini na alifanya kazi mbalimbali za kimisionari lakini sehemu kubwa ya maisha yake akihudumu huko Dodoma – Mpwapwa na Kongwa na sehemu nyingine kama alivyotakiwa na wakuu wake wa shirika.
Nilimfahamu Fr. Angelico miaka thelathini iliyopita huko Bigwa, Morogoro kwenye kituo cha kiroho ambapo yeye na wengine waliandaa semina ya vijana ya kwanza ya vijana wa kikarismatiki. Wakati huo “Uamsho wa Roho Mtakatifu” kama ulivyokuwa ukijulikana ulikuwa haujapata kukubalika au kuungwa mkono sehemu nyingi nchini. Baadhi ya vijana wa enzi hizo ambao tulikuwa tunajiuliza maswali mengi kuhusu ukatoliki na upentekoste. Vijana kutoka karibu mikoa yote tukakutana pale Bigwa kwa wiki moja na kujifunza kuhusu huu uamsho wa kiroho. Fr. Angelico, Fr. Theo Van Schack, Sr. Sophia (Mcongo huyu) na walei wengine kama Mama Bulemela na wengine walitupa nafasi ya kujifunza.
Hata hivyo, ilikuwa Fr. Angelico ambaye aligusa kwa namna ya pekee mioyo ya vijana. Alikuwa ni mnyenyekevu kupitiliza, alimsikiliza kila mtu, na alikuwa anatutia moyo katika safari ya kiroho. Kwa mara ya kwanza wengi wetu tulimuona Padre kama mwenzetu na mtumishi. Fr. Angelico alishiriki kufanya shughuli mbalimbali za usafi kama sisi wengine, na mwenyewe alikuwa anatembea na makubazi yake. Kwa baadhi yetu iliacha alama kubwa sana. Huo kwangu ulikuwa ni mwanzo wa kumfahamu Fr. Angelico na miaka mingi baadaye niliweza kushiriki naye semina mbalimbali na hata kunialika pamoja na vijana wengine kwenda kufanya semina kwenye parokia yake.
Miaka miwili iliyopita akiwa anaelekea kustaafu nilipata nafasi ya kuonana naye uso kwa uso akiwa njiani kuelekea Italy. Ilikuwa ni mara ya mwisho kuonana naye. Taarifa ya msiba wake ilichapishwa na gazeti la huko Trento Italy. Kumbe Fr. Angelico hakugusa maisha ya Watanzania tu bali hata Waitalia wenzake. Haijulikana aliambukizwa lini lakini kwa wanaomkumbuka wanajua jinsi alivyopenda kusalimu kwa kukumbatia (Waitalia wengi wana utamaduni huu) na hili inawezekana ndio sababu ya kuambukizwa na hata yeye kuambukiza wengine kabla ya mauti kumfika.
Hata katika kustaafu kwake Fr. Angelico alikuwa anakusanya mahujaji kutoka sehemu mbalimbali za Italia ambao walikuwa wanaenda Assisi kwa Hija. Na safari hii ya Februari ilikuwa ni safari yake ya mwisho kwani alianza kujisikia kuugua lakini alitaka aendelee na safari yake. Hali yake ilipozidi kuwa mbaya ndipo vipimo vikaonesha kuwa ameambukizwa Covid-19. Alikuwa ni mtu wa imani na mcha Mungu kweli kweli, lakini hilo halikuwa sababu ya yeye kutokuambukizwa au kuambukiza wengine (kwani kundi aliloliongoza kwenye hija 42 walikuwa wameambukizwa).
Binafsi namkumbuka kwa ucheshi wake, furaha yake, na imani yake katika Kristo Mfufuka. Nina uhakika kama angekuwa amejua ameambukizwa au anambukiza wengine sidhani kama angeendelea. Kwani alidhania ni mafua ya kawaida tu. Na kama alijua kabla ya mauti atakuwa amesikitika sana. Kifo chake kimeacha pigo kubwa kwa Wanakarismatiki Watanzania na Wakatoliki wote kwa ujumla kwani alikuwa ni mtumishi mwema na mwaminifu. Hata katika kustaafu alikuwa bado anafanya ziara Tanzania akileta misaada kutoka kwa waumini wa Italia (nakumbuka hata semina kadhaa alisaidia kuchangisha fedha Italia kusaidia mafanikio yake).
Hata sasa tunapoendelea kupambana na gonjwa hili, hatua mbalimbali zilizochukuliwa hadi hivi sasa ni za kupongezwa na kuungwa mkono. Ni kweli tungependa zichukuliwe zaidi lakini pia ni sahihi kutokuwafanya watu waishi katika taharuki. Ugonjwa huu unaweza kumuambukiza yeyote. Awe mwenye imani au asiye na imani, awe tajiri au maskini, awe mtu mkubwa serikalini au mtu mdogo kabisa kijijini; wote mbele ya virusi hivi wako sawa. Virusi vya corona havijui cheo cha mtu, mipaka ya nchi au bendera ya taifa.
Na kama ugonjwa huu umeshambulia watu wenye kumuamini Kristo (imetokea hivyo Korea ya Kusini) au wenye imani nyingine (Iran umeshambulia mahujaji walioenda mji wa hija wa Qom). Na watu hawa wa imani wamekuwa chanzo cha kueneza ugonjwa huo kwa watu wengine katika jamii zao – bila wao wenyewe kujua au kupenda. Imani zao, dua zao kwa Mungu hazikuzuia wao kuambukizwa au kuambukiza; hili ni kweli hata kwa rafiki yangu na muungamishi (confessor) Fr. Angelico.
Tunapoendelea kujikinga na ugonjwa huu na kufuata maelekezo yote tunayopewa na watu sahihi serikalini au matibabu ni lazima pia tujiandae zaidi. Kunawa mikono kwa sabuni, kujitenga kijamii (social distancing) ni namna nzuri zaidi ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo. Kitu ambacho kinaweza kutokea kwetu ni endapo kwenye katika mikuanyiko ya dini na imani (ambayo bado hatujazuia) anatokea mtu mmoja ambaye ni muambukizaji mkuu (super spreader) tunaweza kujikuta tunashindwa maana itakuwa vigumu sana kumfuatilia kila mtu aliyeenda ibadani au kwenye sala. Sitashangaa hata hivyo, hekima ya serikali itawalazimisha kuzuia mikusanyiko mikubwa angalau kwa wiki mbili ili kuzuia maambukizi ya mlipuko. Hii si kwa sababu hatumuamini Mungu au si kwa sababu Mungu hatujali bali ni kwa sababu Mungu ametupa nafasi ya kujiandaa – tusije mbeleni tukamlilia Mungu na kupiga mayowe kama wale wanawali watano wajinga ambao hawakuwa na mafuta kwenye taa zao (Mathayo 25:1-13).
Fr. Angelico na wengine wengi wameshakufa kwa ugonjwa huu na maelfu wengine wameambukizwa. Siyo wote wataumwa vibaya, siyo wote wanadalili. Tusisubiri hadi tupate wagonjwa wengi ndio tuchukue hatua kali zaidi. Mungu tunayemwomba ametupa nafasi ya kujiandaa mapema. Kama alivyosema Rais, tunaweza kukabiliana na ugonjwa huu na tusisalimu amri mbele yake; lakini tutaweza kufanya hivyo tu kama tutafuata kanuni ile ya “defense is the best offense”. Tujikinge kama wahenga walivyosema “heri nusu shari, kuliko shari kamili”.
Mungu ampumzishe Fr. Angelico katika raha ya milele, na amvishe lile taji waliloahidiwa wateule; hadi tutakapokutana tena Sayuni. Fr. Angelico alikuwa na miaka 85.
Taarifa ya kifo chake: Contagiati in gita ad Assisi, è morto padre Angelico
MMM