Lycaon pictus
JF-Expert Member
- Jan 31, 2021
- 9,189
- 16,128
Kitabu hiki kinapatikana BURE ndani ya app ya Maktaba Sauti. Ipo playstore.
Somo la kwanza
Kisa cha Vimbwenelehi
Somo la kwanza
Kisa cha Vimbwenelehi
Nilipokuwa bado mdogo nilipata kusikia habari za vijitu vya kutisha, vyenye matata sana, vinaitwa Vimbwenelehi. Kimo chao shubiri mbili, akisimama atakufikia gotini. Mimi sikuwahi kuona Kimbwenelehi wakati huo, lakini wanasema ni vijitu vyenye kupenda sana kusifiwa, na usipokisifia utaona cha mtema kuni. Ukikutana nacho kitakuuliza, "Umbwenelehi?" Maana yake, kwa lugha nyingi za kibantu, "Umenionea wapi?"
Haja ni kujitahidi kuthibitisha kwamba yeye siyo mfupi, na kwamba hata watu wengine wanaweza kumwona toka akiwa Imbali. Matarajio yake ni kwamba utamwambia, "Nimekuona mbali sana: tangu kulee-eee!" Hapo utakuwa rafiki wa Kimbwenelehi. Lakini ukisema kwamba umemwona pale pale karibu, hata kama si kwa sababu ya ufupi, basi Kimbwenelehi kitakuandama, utapigwa ngumi mpaka uzimie!
Basi zikavumishwa sana sifa hizo za Vimbwenelehi. Ikasemwa kwamba vinaweza kukufurusha ngumi, au kukupiga rungu. Havipigiki hivyo, Vimbwenelehi, kimo chao shubiri mbili! Hivi majuzi nilikuwa nikiwaza. Vipi vijitu hivi, urefu shubiri mbili, vitakavyoweza kuwapiga majitu ngumi hadi wakazimia; ngumi yenyewe itatoka wapi hasa?
Kumbe yote haya yalitokana na hofu ya kijinga. Hofu ile ile ya vibwengo, ya maruhani, ikaingia kwa Vimbwenelehi. Mtu kaona vijitu vya ajabu, akaanza kuviabudu. Kumbe kaona mbilikimo, binadamu kama sisi, isipokuwa mfupi sana tu. Kudai kujitukuza ndio mwenendo wao. Wanajitambua kuwa wafupi, kwa hiyo wanatamani kujikweza-kweza kidogo. Lakini ndio tuwaogope, tuwasifie sana, kwamba wanaweza kutufurusha kwa ngumi, au kwa magongo? Hivyo hiyo ndio sababu kuhofu kumwambia kweli, kama kweli inapaswa kusema. Tunampaka asali Kimbwenelehi, na kumwambia maneno ya kumpendeza wakati wote, tunaogopa asitupige gongo? Hiyo ni hofu au upumbavu?
Basi wako hata leo wananchi wanaowaogopa sana Vimbwenelehi. Wako Vimbwenelehi wa akili, wenye mawazo mafupi sana. Kwa bahati kapata cheo. Basi nao hawa hutamani sana kutukuzwa, kuvikwa vilemba vya ukoka; hawataki kuelekezwa wakikosa. Watu hawa matata sana, na kweli wanaweza sana kuchachamaa. Lakini shida yao kubwa ni umbwenelehi tu.
Sasa la ajabu ni kwamba na sisi wengine tunawaogopa. Mtu anaona dhahiri jambo linapotoka. Anaogopa kusema, maana Kimbwenelehi kikali, kitampiga ngumi! Wajibu wa mwana-TANU ni kusema kweli daima, bila ya chuki, wala kinyongo. Huenda wazo lako likamsaidia mtu, akajitambua kwamba yeye ni Kimbwenelehi.
Na kwa vyo vyote vile, hata kama Kimbwenelehi kweli akikupiga ngumi, ngumi hiyo itafika wapi mbele ya TANU?