Vishazi katika lugha ya Kiswahili

Vishazi katika lugha ya Kiswahili

Suley2019

JF-Expert Member
Joined
Oct 7, 2019
Posts
2,203
Reaction score
5,610
Salaam Wakuu,

Leo tuendelee kujikumbushia masuala mbalimbali yanayohusu lugha. Baada ya kuangalia maana ya Virai na aina zake katika somo lililopita (Soma: Fahamu zaidi kuhusu Virai, muundo na aina zake) leo tutatazama kwa kina kidogo kuhusu vishazi. Katika somo hili tutatazama maana ya Vishazi, aina zake na mifano mbalimbali kama ifuatavyo:

1. KISHAZI
Ni aina ya tungo ambayo huwa na kitenzi ndani yake, kitenzi hicho kinaweza kikawa kinakamilisha maana au kisiwe kinajikamilisha kimaana. Kitenzi ambacho huwa kinakamilisha maana huwa ni kitenzi kikuu (T), na kile kisichokuwa kinatoa taarifa kamili huwa ni kitenzi kisaidizi (TS). Kwa mujibu huo tunapata aina mbili za kishazi yaani kishazi huru na kishazi tegemezi.

A. Kishazi huru (K/Hr)
Aina hii ya kishazi huwa na tabia ya kutoa taarifa ambayo huwa ni kamili katika tungo, hubeba kitenzi kikuu au kishirikishi ndani yake. Kishazi hiki huwa hakihitaji maelezo ya ziada ili kukamilisha maana au taarifa kusudiwa na pia huweza kujitegemea kama sentensi kamili na huwa na muundo wa kiima na kiarifu.

1627458230346.png


B. Kishazi tegemezi (K/ Tg)
Aina hii ya kishazi huwa haitoi taarifa iliyokamili badala yake hutegemea kishazi huru ili kukamilisha taarifa iliyokusudiwa na msemaji. Kishazi hiki hutawaliwa na kitenzi kisaidizi. Kishazi tegemezi kwa upekee wake hakiwezi kutoa taarifa iliyokusudiwa. Vishazi tegemezi hushuka hadhi na kuwa na hadhi ya kikundi cha maneno (kirai).

Mfano; Mtoto unayemjua
Mwanafunzi anayesoma
Mahali alipoingia
Mama alipomchapa
Kaka aliporudi

Vishazi hivyo hapo juu havitoi taarifa iliyokamili ila tunapoviweka pamoja na vishazi huru taarifa iliyokusudiwa hukamilika. Tazama hapa chini:

Mfano; Mtoto unayemjua ameondoka
Mwanafunzi anayesoma atafaulu
Mahali alipoingia ni pachafu
Mama alipomchapa aliondoka
Kaka aliporudi alinifurahisha

Sifa za kishazi tegemezi
i. Hakikamilishi taarifa pasipokuwepo na kishazi huru
Mfano; Mtoto anayecheza mpira ameumia
Mvulana aliyefaulu mtihani amefurahi
Mama alipomkaribisha aliingia ndani

ii. Kinaweza kuondolewa katika tungo bila kuathiri taarifa kusudiwa.
Mfano; mtoto aliyeugua amepona
Mtoto amepona
Mama uliyemsalimia pale ameondoka jana.
Mama ameondoka jana

iii. Hutambulishwa na vitambulishi vya urejeshi vinavyopachikwa katika vitenzi.
Mfano; Anayesoma, Alichookota, Uliokatika, Iliyoibiwa, Alipoingia n.k.

iv. Vilevile kashazi tegemezi hutambulishwa na viunganishi tegemezi kwamba, ili, ili kwamba, kwa sababu, mzizi wa amba na kiambishi cha masharti.
Mfano; Mama alisema kwamba motto ameumia
Mvulana ambaye ni kaka yangu amerejea nyumbani
Akijua atanichapa

Vishazi tegemezi vipo vya aina mbili kutokana na majukumu yake kimuundo
A. Kishazi tegemezi kivumishi (bV)
Kishazi tegemezi kivumishi hufanya kazi ya kuvumisha nomino katika tungo.
Mfano; Baba anayenijali
Mbwa aliyepotea
Mwanafunzi aliyefariki
Uliyemuona pale
Aliyempenda sana

B. Kishazi tegemezi kielezi (bE)
Kishazi hiki hufanya kazi ya kueleza tendo katika tungo na hujitokeza kueleza dhima tofauti tofauti kama ifuatavyo:
  • Kueleza mahali tendo linapofanyika. Mfano; Alipoingia (mahali dhahiri), Alimochungulia (ndani ya kitu Fulani), Alikoelekea (mahali pasipo dhahiri)
  • Kueleza wakati wa tendo. Mfano; Tulipotoka, Alipomchapa, Walipomsema n.k.
  • Kueleza masharti katika tendo. Mfano; Akirudi, Angekuja, Angelimpiga, Angalijua n.k.
  • Kueleza namna tendo linavyofanyika. Mfano; Alivyoimba, Walivyopendeza, Tulivyomsifu.
  • Kueleza kasoro katika kukamilisha tendo. Mfano; Ingawa amesoma, Licha ya kufaulu, Japokua amependekezwa.
  • Kueleza sababu ya kufanyika kwa tendo. Mfano; Kwa sababu alipendeza, Kwa kuwa hujafaulu, Kwa vile umenisomesha.
 
Back
Top Bottom