Wabunge:Wauza mafuta wafutiwe leseni
WASEMA NI WAHUJUMU WA UCHUMI
Festo Polea
WAKATI tatizo la upungufu wa mafuta likionekana kutopata ufumbuzi, wabunge wameitaka serikali kuchukua hatua kali, ikiwa ni pamoja na kuwanyang'anya leseni wamiliki wa vituo vya mafuta waliodiriki kuficha nishati hiyo muhimu na kusababisha usumbufu mkubwa.
Katika hali isiyo ya kawaida, vituo vingi vya mafuta vilikuwa havina mafuta aina ya petroli kwa takriban siku nne, ikiwa ni siku chache baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Mafuta (Ewura) kutangaza bei mpya za bidhaa hiyo, ambayo ilipingwa vikali na wauzaji.
Vituo vingi vilikuwa vimebandika bei ya mafuta iliyotangazwa na Ewura, lakini ni dizeli pekee iliyopatikana katika vituo hivyo na kusababisha misululu mirefu kwenye vituo vichache vilivyokuwa vikiuza mafuta.
Hali hiyo iliifanya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kushangazwa na jinsi wafanyabiashara hao walivyoamua kuonyesha kiburi na kuisumbua serikali inayowaongoza kwa kufanya mgomo baridi.
Wakiwa katika ziara ya kutembelea miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), wajumbe wa kamati hiyo waliwaambia waandishi wa habari kuwa serikali inatakiwa kuchukua jukumu la juu kwa kuwa wafanyabiashara hao hawana huruma na uchumi wa nchi.
Akizungumzia sakata hilo, mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli alisema wauzaji hao wanastahili kuitwa wezi na mafisadi kwa kuwa wamejipatia fedha nyingi kutokana na kuficha mafuta na baadaye kuyauza kwa bei ya juu katika siku hizo mbili, tofauti na ilivyokusudiwa.
"Wauzaji wa mafuta ni wezi na mafisadi, angalia leo serikali inafanya jitihada za kushusha bei wao wanaficha mafuta... wana sababu gani ya kuendelea kuwepo... wafutiwe tu leseni zao hawana faida kwa taifa zaidi ya kuuua uchumi," alisema Lembeli.
Lembeli aliitaka serikali kufanya jitihada za kupata wafanyabiashara wazalendo kujitokeza katika umiliki na uendeshaji wa biashara hiyo ili kusaidia ufichaji wa mafuta kama huo usiendelee kujitokeza.
"Serikali ndiyo ya kulaumiwa kwa sababu ndiyo iliyotengeneza mazingira kwa wauzaji hao kuwa na kauli ya kujipangia watakavyo, kitu ambacho ni hatari kwa uchumi wa nchi," alisema Lembeli.
Mbunge wa Viti Maalum (CUF, Tabora), Magdalena Sakaya alisema ufichaji wa mafuta uliofanywa na wafanyabiashara hao unatokana na jeuri waliyonayo kwa serikali.
"Kuficha mafuta ni hujuma kwa uchumi, taifa na kwa wanajamii wote walio katika nchi hiyo kwani hutegemea mafuta, hivyo katika harakati za kuokoa hali hiyo, ni muhimu kufungia vituo vyote vinavyoficha mafuta na kuwapokonya leseni wamiliki wa vituo hivyo," alisema Sakaya.
"Hawa wafanyabisahara ni wahujumu wa nchi kwa kuwa katika biashara wanayoifanya wanataka kupata faida ya asilimia 100 na kuacha nchi tupu," alisema Sakaya.
Mbunge wa Nzega, Lukas Seleli alisema tatizo la kukosekana kwa mafuta linatokana na serikali kutojua kiwango kamili cha mafuta yanayoingizwa na kubaki katika akiba iliyobaki kwa ajili ya siku zijazo.
"Serikali haipo makini na masuala hayo muhimu kwani hadi leo Ewura, ambacho ndiyo chombo cha serikali katika kushughulikia mafuta, haina mitandao katika mikoa... walikimbilia biashara huria ndio maana inawapa shida," alisema.
"Hivi mafuta wanasema hawana kweli inaingia akilini wameuza wapi wakati kulikuwa na akiba ya siku nyingi... ndiyo maana nasema serikali haijawa makini katika mambo hayo," alisema Seleli ambaye aliitaka serikali kuchunguza kwa kina kama mafuta hayo yapo ama hakuna ndipo wafanye utaratibu wa kufungia.
Mbunge wa Kongwa, Job Ndungai alisema endapo serikali inataka kumaliza tatizo hilo, haina budi kuiwezeshe kampuni ya TPDF iweze kuingiza mafuta mengi na kuyauza kwa bei nafuu.
Wakati huo huo waandishi Tumsifu Sanga na James Magai wanaripoti kuwa makampuni ya mafuta yanatarajia kuingiza shehena kubwa mafuta nchini ambayo itaondoa uhaba wa mafuta ulioikumba nchi kwa takribani siku nne sasa.
Akijibu maswali ya waandishi wa habri jana kwenye mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na Ewura, mkurugenzi Mtendaji wa makampuni ya uagizaji wa mafuta nchini (Taomac), Salum Bisarara alisema tayari kuna meli za mafuta ambazo zitaingia na kushusha mafuta bandarini wakati wowote.
Bisarara alisema kampuni ya mafuta ya Gapco imeingiza nchini lita milioni 10 na kampuni ya BP inatarajia kuingiza shehena ya mafuta tani 1,000 ifikapo Januari 18, wakati Januari 25 Oryx inatarajia kuingiza tani 8,000 pamoja na GP ambayo inatarajia kuingiza tani 3,000 ambapo zote kwa jumla zitakuwa zimeshusha tani milioni .
Bisarara alitumia nafasi hiyo kukanusha taarifa kuwa wafanyabiashara wa mafuta wanaihujumu serikali kwa kugoma kuuza mafuta kama njia ya kupinga bei elekezi zinazotolewa na Ewura kwa madai kuwa wanapata hasara.
Awali Kaimu Mkurugenzi wa Ewura, Anastas Mbawala, akielezea hali halisi ya uhaba wa mafuta ulioikumba nchi tangu Jumamosi, alisema hali hiyo imetokana na makampuni ya mafuta kuogopa kuagiza mafuta mengi wakihofia kupata hasara kufuatia hatua ya Ewura kutangaza bei elekezi kila wiki.
"Wenye vituo vya mafuta wamekuwa na hisia kuwa Ewura itakapobadilisha bei inaweza kushuka na hivyo kupata hasara. Hivyo kuna wale ambao waliacha kufanya manunuzi makubwa ili kutosheleza siku za mwisho wa wiki pamoja na sikukuu ya Mapinduzi," alifafanua Mbawala.
Hata hivyo Mbawala alisema walipofanya ukaguzi katika katika vituo na maghala mbalimbali ya makampuni ya mafuta walibaini kuwa kulikuwa na mafuta ya kutosha kwa matumizi ya matumizi ya siku 10.
Source:
Mwananchi Read News