SoC02 Vya walemavu waachie Walemavu

SoC02 Vya walemavu waachie Walemavu

Stories of Change - 2022 Competition

PCharahani

Member
Joined
Jul 27, 2022
Posts
7
Reaction score
4
Je, umewahi kupanda basi ukakaa kwenye siti ambayo ni maalumu kwaajili ya walemavu wakati wewe si mlemavu na wala haukuwa na ulazima wa kukaa kwenye siti hiyo? Au pengine umewahi kuona mtu asiye mlemavu akikaa kwenye siti maalumu za walemavu? Kama uliwahi kukaa ni nini kilifanya ukakaa? Au pengine hukuona nembo inayoashiria kuwa siti hiyo ni kwaajili ya walemavu? Fuatana nami.

Wengi wa wakazi wa miji mikubwa, kwa mfano Dar es salaam wasio walemavu wanaotumia magari ya mwendo kasi, wamekuwa na kawaida ya kuketi kwenye siti ambazo wanatakiwa kuketi walemavu. Wengi wao ukiwauliza ni kwanini wao hukaa kwenye siti hizo na wao si walemavu hujibu kuwa hawajaona mlemavu kwa wakati huo ndani ya basi. Sawa, ila je ni kweli na haki? Tutazame kwanza maana ya mlemavu na ulemavu kwa pamoja.

Ulemavu ni hali ya kuwa na dosari mwilini inayoathiri utendaji kazi wa sehemu au viungo tofauti vya mwili. Hali hiyo pia inaweza kuwa kizuizi cha mtu kushiriki katika masuala ya kawaida katika maisha kutokana na ugumu wa kutenda kama watu wengine. Ulemavu huweza kutokea wakati wowote katika maisha ya mtu; watu wengine huzaliwa wakiwa walemavu, wengine hupata ulemavu ukubwani au katika safari ya kukua. Ulemavu unaweza kuwa wa kudumu, wa muda mfupi au wa vipindi.

Kwa kutambua kuwa kuna walemavu katika jamii na kwamba utendaji wao huathiriwa na ulemavu wao kwa kiasi kikubwa, sehemu mbalimbali hutengwa ili kuwarahisishia maisha.

Sehemu mbalimbali, iwe ndani ya majengo, sehemu za wazi, vyoo na njia zinazojengwa kwaajili ya walemavu huwekwa alama maalumu (The International Symbol of Acces (ISA)/International wheelchair symbol) inayoonesha kuwa maeneo hayo ni kwaajili ya walemavu. Alama hiyo kwa kawaida huwa ni nembo nyeupe ya mtu aliyekaa kwenye kiti cha magurudumu.
1659452944802.png

Alama (ISA) ya jengo/eneo/gari linalofaa kwa walemavu (picha na Wikipedia)

Tujuavyo wengi ni kuwa alama hii huonesha kuwa eneo husika ni kwaajili ya walemavu wenye shida za kutembea.

Kikubwa ambacho wengi wetu hatujui ni kuwa nembo hii huonesha maeneo maalumu sio tu kwaajili ya walemavu wa viungo au wale wanaokaa kwenye viti vya magurudumu bali pia wote wenye changamoto za kiafya zinazoathiri kutembea au kujongea kwao. Changamoto hizo nyingi ni za ndani ambazo watu hawawezi kuziona kwa macho, kwa maana walionazo huonekana wakiwa kawaida tu na wasio na dosari.

Ionekanapo nembo katika matumizi huashiria kuwa eneo husika linatoa kipaumbele kwa watu wenye changamoto mbalimbali kama vile

-Watu ambao hawawezi kutembea

-Watu ambao hawawezi kufika mbali pindi wanapotembea

-Watu wenye ulemavu wa viungo

-Watu wenye matatizo ya akili, wanaohitaji kutumia maeneo hayo kila mara na wale wa vipindi

-Watu wenye tatizo la kutojizuia kurudiarudia tendo, kwa kiingereza Obsessive Compulsive Disorder (OCD).

-Ugojwa wa kushindwa kusahau matukio yanayotokana na kiwewe (trauma) linalojulikana kwa Kiingereza kama Post - Traumatic Stress Disorder (PTSD) na mengineyo.

Watu wenye magonjwa yanayoathiri utembeaji kama vile Pumu (asthma), matatizo ya neva, miguu iliyopinda (club feet), Usonji au kwa Kiingereza Autism Spectrum Disorder (ASD), ugonjwa wa mikano kuwa dhaifu yaani Ehlers-Danlos Syndrome (EDS), ugonjwa wa kutetemeka au kwa Kiingereza Parkinson Syndrome, kisukari (Diabetes), Ugojwa wa kushuka kwa sukari (Diabetic Hypoglycemia), wenye matatizo ya uti wa mgongo, wenye matatizo yanayoweza kuwafanya wasiweze kugeuka, pamoja na wale wanaopitia matibabu ya saratani ni walengwa wa matumizi ya sehemu za walemavu zenye alama hiyo ya ISA. Baadhi ya changamoto au magonjwa hayo huonekana kwa macho na baadhi hayawezi kuonekana.

Kwenye vyombo vya usafiri, walemavu wengi na watu wenye changamoto za kimwili zisizoonekana hukumbwa na tatizo la kukosa kukaa kutokana na watu wasio walemavu kukalia viti vya walemavu. wengi wa wanaokalia viti hivyo hawavihitaji na huwaacha wanaovihitaji wakiwa wamesimama kitu ambacho huwasababishia maumivu wahitaji hao. kwenye maegesho ya magari wasio walemavu huegesha na kuacha walemavu wakihangaika katika maegesho finyu na yaliyo mbali na huduma.

Katika nchi mbalimbali watu wenye ulemavu uliothibitishwa na madaktari huweza kukidhi vigezo vya kupewa kitambulisho cha walemavu ili wakitumie kuwasaidia kupewa kipaumbele katika huduma mbalimbali kulingana na hali zao, ikiwemo kupewa kipaumbele kwenye sehemu za maegesho ya magari. Wanaopewa huweza kutembea nacho na kukitumia kutumia maeneo tengefu kwa walemavu bila taabu. Kitambulisho hicho hujulikana kwa jina la “beji ya bluu” (blue badge) au disabled placard/handicap placard.
1659452469475.png

Kitambulisho cha mlemavu
picha na mtandao (Google Photos)
1659452346352.png

Eneo la maegesho ya magari kwa walemavu
Picha na mtandao (Google Photos)

Mambo muhimu mbalimbali yanayotakiwa kufanywa na makundi mbalimbali ili kuweza kusaidia watu wenye ulemavu au watu wenye changamoto zinazohusisha kutembea ni haya yafuatayo;


Mamlaka zinazohusika na ujenzi wa miundombinu kama; barabara, shule, hospitali, majengo ya umma na miundombinu ya usafiri zinatakiwa kuweka kipaumbele katika kujenga miundombinu inayotoa fursa kwa walemavu kupata huduma katika sehemu mbalimbali.

Miundombinu ambayo tayari imejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya walemavu isimamiwe ipasavyo ili kuhakikisha inatumiwa na walengwa.

Mamlaka husika zihakikishe kwenye miradi yote mikubwa ya nchi inayohudumia wananchi kunakuwa na sehemu maalumu kwaajili ya walemavu kama, kuwa na maeneo ya maegesho ya magari ya walemavu au watu wenye matatizo yanayowazuia kutembea au kutembea kwa umbali mrefu. Maeneo hayo yawekewe alama inaruhusu walemavu tu kuyatumia. Maeneo hayo yazingatie umbali kutoka yalipo hadi sehemu za huduma.

Mamlaka husika ziweke wazi vigezo vya mtu kukubalika kuwa mlemavu ili wanaokidhi waweze kupewa vitambulisho vya walemavu ambavyo vitawawezesha kutambulika kirahisi (kwa hiyari yao) na hivyo kuwapunguzia adha zinazotokana na kuonekana si walemavu kwa macho na hivyo kunyimwa haki zao.
1659452730831.png

Kitambulisho cha mlemavu cha kuweka kwenye gari ili aweze kuegesha eneo maalumu
Picha na mtandao (Google Photos)


Elimu itolewe kwa wanachi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii juu ya ulemavu, walemavu na haki zao ili kuwasaidia kupata haki zao bila taabu.

Kila mwanchi anatakiwa kujua kuwa ulemavu sio chaguo, ulemavu unaweza kuoneakana au kutoonekana kwa macho hasa ukiwa ndani ya mwili. Hakuna mwenye jukumu la kujieleza ni nini anachokipitia mwilini mwake na hivyo si vema kudhani kuwa kila mtu yuko sawa kimwili kwa kumtazama.

Ni hekima kutokaa au kutumia sehemu wanazotumia walemavu iwe ni sehemu za wazi za kukaa, maegesho ya magari, njia za kupita au vipandio. Ni hekima kuacha ubinafsi.

Ukiona walemavu wanafaidi ukatamani vilivyo vyao usisahau kuomba upate ulemavu wao kwanza.

Vya walemavu waachie walemavu.
 

Attachments

  • 1659452391462.png
    1659452391462.png
    33.7 KB · Views: 6
Upvote 3
Back
Top Bottom