SoC02 Vyakula hivi ni janga kwa watoto shuleni

SoC02 Vyakula hivi ni janga kwa watoto shuleni

Stories of Change - 2022 Competition

Abeida

Member
Joined
Jul 14, 2022
Posts
13
Reaction score
7
Abeid Abubakar

Umewahi kutembelea shule yoyote ya msingi au sekondari iwe mjini au kijijini?
Tuache shule zilizopo vijijini, tuzitupie jicho zile shule za mjini. Aghalabu hutokosa kukuta vibanda vya kila aina vimezunguka shule. Humo huuzwa kila aina ya vyakula.

Hata hivyo, vilivyo maarufu zaidi zaidi ni viazi vya kukaanga maarufu kama chips, soda, juisi za viwandani, keki, biskuti, pizza, mihogo ya kukaanga, maembe mabichi, ice cream, ubuyu, koni, bazoka, karanga na vitu vingine vingi ambavyo hujulikana kama vyakula vya haraka au kimombo Junk foods.

Ni vyakula vinavyokosolewa kwa kutokuwa na virutubisho muhimu kwa lishe ya binadamu. Na kibaya zaidi vinatajwa kuchangia katika matatizo ya kiafya kwa binadamu.

Katika shule hizi ni wanafunzi wachache utakaowakuta wakila vyakula kutoka kwenye migahawa au mama ntilie kama ugali, wali nk. Kimsingi, vyakula hivi vya haraka, vimetamalaki shuleni. Miaka saba mwanafunzi anatumia vyakulahivyo akiwa elimu ya msingi. Akibahatika kuingia sekondari, ana miaka mingine minne ya kula vyakula hivyo.

Nafuu kubwa ipo kwa wanafunzi wa bweni au hosteli ambao hula vyakula vya kawaida pengine chini ya usimamizi maalumu.

Ni hatari kiafya
Ukiangalaia asili ya vyakula hivi, sio siri kuwa havina manufaa kwa afya za wanafunzi, lakini ndivyo vyakula vinavyotegemewa na wanafunzi wengi.

Mwalimu mmoja wa Shule ya Msingi Kilimani iliyopo Kipunguni, wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, anasema kwa aina ya vyakula wanavyokula watoto hao, upo uwezekano mkubwa wa kuugua magonjwa kama vidonda vya tumbo.

Yeye anasema ameliona hilo na anaona namna watoto wanavyoathirika na ugonjwa huo. Anasema shuleni watoto wanakula vyakula vyenye chumvi nyingi anatoa mfano wa chips, mihogo au maembe ambayo ili kupata radha na vipite kooni kwa utamu, wanafunzi lazima watumie chumvi.

Sasa ikiwa hivi ndivyo maisha yalivyo siku tano kwa wiki, siki 20 kwa mwezi mara miezi zaidi ya nane ya mwaka wanapokuwa masomoni, kwa nini wanafunzi hawa wasiwe na matatizo ya kiafya? Na ilivyo hata yasipoonekana sasa, yanaweza kuja kuwadhuru ukubwani.

Wataalamu wa afya, lishe wanaonya kuwa vyakula aina hiyo vimekuwa kichocheo cha magonjwa kama vile kisukari, kiharusi, shinikizo la juu, unene uliopitiliza, vidonda vya tumbo, magojwa ya moyo na mishipa na mengineyo ambayo kwa sasa yanawatesa watu wengi kila kona ya dunia.

Kwa kuwa vyakula vingi ni vile vyenye wingi wa asidi kama chips na mihogo yenye kachumbari, chumvi na pilipili, lazima tuwazuie wanafunzi kwa kuwa wanajiweka katika mazingira ya kupata magonjwa kama nilivyotaja hapo juu.

Februari 2020, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa angalizo la namna watoto katika nchi mbalimbali duniani walivyo kwenye hatari ya kudhurika kutokana na matangazo ya ulaji wa vyakula vya haraka.



Vidonda vya tumbo
Licha ya maelezo mengi ya kitabibu kuhusianisha vidonda vya tumbo na watu wazima, lakini upo uwezekano hata watoto wadogo kuugua ugonjwa huo.

Taarifa iliyomo kwenye tovuti www.stanfordchilrens.org yenye kichwa cha habari: Stomach and Duodenal ulcers in children, inaweka bayana kuwa vitu kama vyakula vyenye asidi, uvutaji, kaffeine na pepsin ni vyanzo vizuri vya watoto kuugua vidonda vya tumbo.

Watoto wetu hawa wanaweza wasiwe wavutaji, lakini matumizi ya vyakula vyenye chumvi na pilipili nyingi kama mihogo na chips zenye kachumbari wanavyokula kila siku, vinatosha kuwaweka katika nafasi kubwa ya kuugua ugonjwa huu, ambao taarifa ya WHO ya mwaka 2020 inaeleza kuwa uliua Watanzania 462, sawa na asilimia 0.16 ya idadi ya vifo vyote nchini.

Si idadi ndogo, hii ni nguvu kazi inayoweza kuwa na mchango fulani kwa Taifa. Pengine katika vifo hivyo kuna wahandisi, walimu, wanasheria, wataalamu wa Tehama na wengineo.

kwa sura hiyo, kuna haja ya kudhibiti aina ya ulaji wa watoto wetu wakiwa shuleni, ili kuwaepusha na majanga ya maradhi yanayoweza kuwaweka kwenye hatari za kiafya maishani mwao

Njia za kudhibiti tatizo hili
Ifike hatua sasa mamlaka husika zione kuwa vyakula hivi ni sawa na janga kwa watoto na Taifa kwa ujumla.

Udhibiti wa nini wanafunzi wanapaswa kula, hauna budi kuzingatiwa, vinginevyo tunaandaa taifa la wagonjwa ambao watakuja kuathiri nguvu kazi ya ya Taifa.

Hili lituzindue ili sasa ule mpango wa lishe shuleni utiliwe maanani zaidi, kwa shule zote vijijini na mijini kuwa na utaratibu wa kutoa vyakula kwa wanafunzi. Na kisiwe tu chakula bali uwe mlo bora.

Inaposhindikana hilo, basi hawa hawa wauzaji wa vyakula binafsi wadhibitiwe. Walimu wakuu na kamati za shule kwa kushirikiana na maofisa afya ngazi ya mitaa, vijiji na kata, lazima wawe na utaratibu wa kuwasimamia wauzaji wa vyakula shuleni kwa kuwa na orodha yao, anuani na namna wanayopika.

Hilo litasaidia hata siku kukitokea tatizo iwe rahisi kujua wanafunzi walikula kwa nani na chakula gani. Tofauti na sasa ambapo uongozi wa shule unachojua ni kugawa mabanda na kuchukua kodi, huku kila muuzaji akijitengenezea chakula pasipo usimamizi.

Kwa baadhi ya shule, natambua kuwapo kwa programu za utoaji wa vyakula, hata hivyo bado uuzwaji wa ‘junk foods’ umekuwa ukiendelea shuleni.

Kwa hakika kama jamii tunapaswa kutupia jicho vyakula hivi, ambavyo athari yake inaweza isionekane sasa, lakini ikaja kuwatesa watoto miaka ijayo na hivyo kuathiri nguvu kazi ya Taifa.

Mwandishi ni mkazi wa Dar es Salaam. Anapatikana kwa barua pepe: abeidothman@gmail.com
 
Upvote 2
Asante sana, Mimi nilivyo sikia tu hivyo vibanda vya shule ya msingi wanavyo uza misosi hapa mate yamenitoka, umenikumbusha kwa mama bonge nilikuwa nawahi mihogo yangu ya shilingi mia mbili na juisi ya mia nilikuwa naenjoy sana.


Unajua wengi wao wanao uza vyakula kwenye vibanda ni wazazi wetu wa watoto wa shule unazani wazazi wasipo fanya biashara watakula nini pamoja na familia zao zinazo wategemea.

Mimi ndiyo maisha niliyo pitia hayo hata mama angu alikuwa anauza maji ya mifuko shuleni.


Nimeona kuna kipengele unazungumzia kuhusu vyakula vya hotelini kwamba hivyo ni salama kwa kusema hivyo unakosea sana. Hats hivyo vyakula vya hotelini navyo vinakasoro.


Lakini inaonekana wewe ulisoma shule za kishua sana unafiatwa na gari unarudishwa na gari lakini sisi umaskini tulikuwa tunatembea umbali mrefu kwa miguu kwenda kusoma na tulikuwa hatuna ngarama za kununua hivyo vyakula vya hotelini kama ulivyo kuwa unakula wewe sisi ni miogo ya mia tu.


Kwahiyo vyakula vya kwenye mabanda ni vya wazazi wetu kama vitakuwa na kasoro basi ni Mara chache sana vyakula vya kwenye mabanda siyo kwamba ni vibaya hivyo ndiyo vimenikuza Mimi mpaka Leo hii nipo hapa.

Nime kupigia kura
 
Asante. sana. Hata mimi kwa hakika background yangu sikusoma shule za kishua, nimekula sana hivyo vyakula na ule ulaji ndio unaonisukuma leo nikiwa ukubwani kuona kuwa japo nimekula sana bado havikuwa salama
 
Asante. sana. Hata mimi kwa hakika background yangu sikusoma shule za kishua, nimekula sana hivyo vyakula na ule ulaji ndio unaonisukuma leo nikiwa ukubwani kuona kuwa japo nimekula sana bado havikuwa salama
Asante sana pitia na kwangu utie baraka
 
Back
Top Bottom