SoC04 Vyombo vya Habari na nguvu ya kulinda maadili, mila na desturi za taifa

SoC04 Vyombo vya Habari na nguvu ya kulinda maadili, mila na desturi za taifa

Tanzania Tuitakayo competition threads

Muharram wa Pili

New Member
Joined
Jun 2, 2024
Posts
3
Reaction score
0
Ulimwengu umekuwa kijiji kwasababu ya ukuaji wa sayansi na teknolojia. Kupata habari na matukio ya ulimwengu ni rahisi sana kuliko hata kuipata shilingi. Hii inatokana na maendeleo na hatua kubwa zilizopigwa katika sekta ya sayansi uvumbuzi na teknolojia Duniani. Upatikanaji wa intaneti, mitandao ya kijamii, vyombo ya kupasha habari kama luninga na redio vimekuwako kila kona. Utakubaliana nami kuwa kwa hali hiyo sekta ya habari ulimwenguni ina nguvu kubwa katika ushawishi na kuleta matokeo ya aina yoyote ile. Ndio sekta ya habari ikitumika vyema huleta matokeo chanya vivyo hivyo ikitumika vibaya huwenda ikaleta matokeo hasi.

Propaganda ni wazo jipya ama geni linaloundwa kwa lengo la kuzoeleka kwenye jamii ambayo haikuwa na mazoea nalo, kwa ajili ya maslahi ya waliounda wazo hilo, aidha kibiashara, kisiasa, kimfumo ama kimkakati. Na mara zote ili propaganda iweze kuenea kwa kasi basi vyombo vya habari hutumika sana kueneza kutokana na nguvu iliyonayo.

Kwenye sekta ya habari kuna vyombo vya habari vya kitaifa, kimataifa, vya binafsi na hata kurasa za mitandao ya kijamii lengo lao likiwa ni kupasha habari za ndani ya nchi na kwengineko ulimwenguni. Hoja yangu hapa je ni kwa namna gani vyombo hivi vinazingatia maudhui yao kwa wigo mpana wa kulinda maadili, mila, desturi na kudumisha utamaduni wa kizazi cha taifa kwa maslahi mapana ya Taifa?

Maslahi ni faida aipatayo mtu baada ya kufanya kazi ama jambo kwa lengo la kunufaika, yaweza kuwa fedha, wadhifa ama sifa. Maslahi ndio yamekuwa kipaumbele katika kila jambo lifanywalo katika ulimwengu wa sasa. Tena kwa wale ambao wana uchu wa mafanikio wamekuwa hawajali misingi wala mipaka ya kiutu, asili hata tamaduni za jamii za watu kwa sababu tu ya maslahi.

Uhuru wa vyombo vya habari katika kupasha habari
, ni haki yao kisheria kutafuta, kukusanya na kuzitaarifu habari hizo kisheria kupitia vyombo hivyo. Lakini je kama habari hizo ni propaganda za kimfumo wa kilimwengu zenye lengo la watu ama mataifa makubwa yenye nguvu kiuchumi kueneza mikakati yao kwa maslahi yao dhidi ya mataifa madogo kiuchumi. Ni kwa namna gani vyombo vyetu vya ndani vya kitaifa na binafsi vina utayari wa kizalendo kuzuia propaganda hizo kisheria kwa lengo la kulinda maadili, mila na desturi za Utaifa wetu na kizazi chetu.?

Uzalendo ni mapenzi makubwa kwa nchi, taifa kwa kuheshimu katiba na kutekeleza wajibu wa kiraia bila kuvunja sheria na kwa maslahi ya ustawi wa Taifa na kizazi chake. Hapa tutakosoa, tutahoji, tutatoa maoni na kudai mabadiliko ya kimifumo kulingana na nyakati bila ya kuvunja sheria za nchi. Kwa nguvu ya vyombo vya habari zitataarifu habari hizo ili kusaidia kwenye ujenzi wa taifa bila kupendelea itikadi za makundi ya watu ama taasisi ndani ya nchi. Tukiyatekeleza haya tutakuwa Wazalendo kwa Taifa letu.

Ukinzani wa kimaslahi na Uzalendo kwa Taifa.
Kama ambavyo nimetangulia kufafanua awali juu ya maslahi na uzalendo, kumekuwa na ukinzani wa kipi ni kipaumbele kati ya maslahi na uzalendo. Vyombo vingi vya habari vipo kibiashara maana yake wao wapo kimaslahi zaidi na ndio kipaumbele chao. Je zinapokuja propaganda zenye lengo baya kwa uhai wa maadili, mila na desturi zinazokinzana na utamaduni wa Taifa wanazizuia vipi.? Watachagua maslahi ama Uzalendo?

Sheria za kimataifa na mikataba ambazo zimeazimiwa kwenye mabaraza ya umoja wa matifa, nyingi zikiwa zimeshinikizwa na mataifa yenye nguvu kiuchumi duniani ambazo nyingi zinakizana maadili, mila, desturi na utamaduni wa mataifa mdogo kiuchumi. Mwanzo sheria hizo huanza kama propaganda na baadae wanashinikiza zikubalike bila kuheshimu tamaduni za watu. Sheria ya haki za binaadam ni mfano wa hizo nyingi. Ni wazi kuwa binaadam ana Haki lakini ipo na mipaka kulingana na asili ya kuumbwa kwake. Haki ya uhuru wa vyombo vya habari kimataifa inawataka kuarifu kila aina ya matukio. Vyombo vya habari vingi vinaheshimu sheria za kimataifa kuliko za sheria za nchi na wanajifichia huko bila kuwa Wazalendo.

Tanzania tuitakayo ni yenye kuwa na sheria kali ya kulinda maadili, mila na tamaduni za watu wake. Vyombo vya habari viwe nguzo muhimu ya kupinga, kukataa aina yoyote ya uenezwaji wa propaganda zenye lengo la kuharibu tamaduni za taifa letu. Vielimishe na kuelezea kinaga ubaga athari za propaganda hizo kwa taifa, zitangaze kwa ufahari tamaduni, mila na desturi kwa maadili yetu wenyewe. Na huo ndio utakuwa uzalendo wa kweli kwa maslahi ya Taifa na kukilinda kizazi cha Taifa hili dhidi ya propaganda zenye lengo la kumomonyoa utamaduni wao.

Rai yangu kwa vyombo vya habari ni kushirikiana na serikali na asasi za kiraia kuwa Wazalendo wa kweli kwa Taifa lao na kutanguliza maslahi ya Taifa kwanza kuliko fedha na sifa za kilimwengu ilhali Taifa linaangamia kwa kuwa na kizazi kisichojitambua.
Ndimi wenu 𝙈𝙪𝙝𝙖𝙧𝙧𝙖𝙢 𝙬𝙖 𝙋𝙞𝙡𝙞
 
Upvote 0
Back
Top Bottom