Novemba 3, 2023, Ukurasa unaopatikana kwenye mtandao wa X unaofahamika kwa jina la
Tanzania Abroad TV ulichapisha habari inayoonesha idadi ya visa vya maambukizi ya UKIMWI kwenye baadhi ya vyuo nchini.
Chapisho hilo lilisema:
“Tumia kinga uwa leo vyuo hivi….UDSM Ina wanafunzi wa UKIMWI 16,000. UDOM Ina wanafunzi wa UKIMWI 8,682. IFM Ina wanafunzi wa UKIMWI 4,526. SOKOINE Ina wanafunzi wa UKIMWI 3,521. Mzumbe wenye UKIMWI ni 3,236”
Hadi kufikia Novemba 6, 2023,
chapisho hili lilikuwa limesomwa na zaidi ya watu 163,00, watu 1329 walilipenda huku wengine 126 wakishirikisha wengine. Aidha, watu 76 walihifadhi chapisho hili (Bookmark) kwa ajili ya kumbukumbu na matumizi ya baadae.
Ukweli wa takwimu hizi upoje?
Baada ya kusambaa kwa taarifa hizi, JamiiCheck ilifanya jitihada kadhaa, ikiwemo kufuatilia hotuba za Waziri wa Afya
Ummy Mwalimu na Naibu wake
Dkt. Mollel pamoja na kurejea nyaraka za taarifa rasmi za kiserikali zenye kufafanua na kutoa taswira ya maambukizi ya VVU nchini.
Katika ufuatiliaji huu, JamiiCheck haikupata chanzo chochote cha kuaminika kilichotoa taarifa hizi. Aidha, takwimu tajwa hazipatikani sehemu zingine isipokuwa kwenye ukurasa wa
Tanzania Abroad TV jambo linalotia shaka ukweli wake.
Kanusho la Mamlaka
Novemba 3, 2023, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu
alikanusha taarifa hii kupitia mtandao wa X.
Pia, Novemba 4, 2023, Ukurasa rasmi wa Wizara ya Afya kwenye mtandao wa X
ulikanusha taarifa hii kwa kuiita kuwa ni "Uzushi" na kuwataka wananchi waipuuze.
Kanusho la Wizara ya Afya kwenye mtandao wa X
Kwa mujibu wa
Utafiti wa mwaka 2022/23 uliofanywa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (
TACAIDS), Tume ya Kudhibiti UKIMWI Zanzibar (
Zanzibar AIDS Commission- ZAC), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (
NBS) pamoja na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar, Tanzania imepata matokeo chanya katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI na kwamba idadi ya maambukizi mapya inaendelea kupungua ikilinganishwa na matokeo ya utafiti wa mwaka 2026/17.
Kushiriki tendo la ndoa, kupokea damu na mazao yake, uchangiaji wa vifaa vyenye ncha kali pamoja na maambukizi ya mama kwa mtoto wakati wa ujauzito na (au) wakati wa kujifungua ni
baadhi ya njia zilizothibitishwa kuwa na uwezekano usiotia shaka katika kusababisha maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) ambapo ikiwa
tiba sahihi haitatolewa, mtu huyu hupata Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI) ambayo ni hatua kubwa zaidi ya maambukizi.
Tangu kugunduliwa kwake zaidi ya miaka 40 iliyopita, zaidi ya watu milioni 85.6 wameambukizwa ugonjwa huu huku takriban watu milioni 40.4 wakipoteza maisha. Hii ni kwa mujibu wa
Shirika la Afya Duniani (WHO).
Aidha, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2022, takriban
watu milioni 39 walikuwa wanaishi na maambukizi ya ugonjwa huu duniani.