SoC02 Wabunge hamtutendei haki Wananchi

SoC02 Wabunge hamtutendei haki Wananchi

Stories of Change - 2022 Competition

Abeida

Member
Joined
Jul 14, 2022
Posts
13
Reaction score
7
Abeid Abubakar
Katiba yetu ya Tanzania ya mwaka 1977 inatambua uwepo wa wawakilishi wa wananchi maarufu kama wabunge na kule visiwani Zanzibar wakijulikana kama wawakilishi.

Kwa mujibu wa Katiba hiyo ambayo ndiyo msingi mama wa sheria na mwenendo wa uongozi na uendeshaji wa nchi, sehemu ya tatu ibara ya 6 kipengele namba 1 hadi 3 wabunge, wanaelezwa kuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba.

Kutekeleza hilo, Katiba yetu ikaendelea kueleza kuwa wabunge watakuwa na majukumu haya yafuatayo:

(a) Kumuuliza waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake;

(b) Kujadili utekelezaji wa kila wizara wakati wa mkutano
wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti;

(c) Kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano, na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo;

(d) Kutunga sheria pale ambapo utekelezaji unahitaji kuwapo sheria;

(e) Kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Jamhuri ya Muungano na ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa

Hata hivyo, uzoefu wangu wa kufuatilia mwenendo wa Bunge letu kwa muda mrefu, umebaini kuwa wabunge wengi kama sio wote, achilia mbali ya madai kama vile kuutaka ubunge kwa maslahi binafsi ya kiuchumi na umaarufu, wamekuwa si wawakilishi halisi wa wananchi.

Ajenda zao aghalabu sio zinazotokana na wananchi bali mtazamo binafsi au ajenda za kivyama. Ni kwa sababu hii utaona wabunge wakishupalia sana hoja za kitaifa zaidi hasa zenye mrengo wa kivyama kuliko kuzungunza kile wanachotumwa na wananchi.

Ndio maana haishangazi kuona mbunge wa jimbo lililopo kusini mwa nchi akizungumza hadi kutokwa povu masuala ya kaskazini, huku akiacha masuala muhimu ya jimbo lake huko kusini au mambo yanayohusu watu wa Kusini.

Sipingi mbunge kuzungumzia hoja za kitaifa hasa zinapoibuka bungeni, lakini najiuliza hoja wanazotoa ndizo walizopewa na wananchi wao? Katiba imeweka bayana kuwa wabunge ni wawakilishi wa wananchi, hawajiwakilishi, hivyo wanachotaka wananchi ndicho kinachopaswa kusemwa bungeni vinginevyo mbunge anyamaze.

Najaribu kukumbuka kwa mfano wakati wa mchakato wa Katiba mpya, hivi kuna mbunge aliyeitisha kikao na wananchi wake akawaambia nakwenda bungeni nikaseme nini?

Sidhani na naamini hivyo kwa sababu uzoefu wangu unaonyesha kuwa wabunge si ' visemeo'vya wananchi.

Kwa hili la Katiba mpya, lazima nisisitize kuwa wananchi wana nafasi kubwa na ndio wanaopaswa kuwapa wabunge mwelekeo, mitazamo na misimamo.

Lakini naomba msomaji wangu wewe na mimi tujiulize hivi kura zile zilizopigwa na wabunge wetu wakati wa Bunge lile maalumu, zilitokana na maelekezo ya wananchi? Je, kuna mbunge aliyekusanya maoni ya wananchi wake akayapima uzito na kuona wengi wana mtazamo upi ili auchukue na kwenda nao bungeni kupiga kura ile?

Sidhani kama hilo lilitokea. Naamini kwa asilimia nyingi mno wabunge walipiga kura kwa mitazamo yao na ya vyama vyao, badala ya walichotumwa na wananchi.

Uzoefu hapa nchini unaonyesha kuwa mtu akishakuwa mbunge anajiona kuwa ana weledi wa kila kitu, ni mtu wa kusikilizwa na wananchi badala ya kuwasikiliza, ndio maana hata wanapoitisha mikutano ya hadhara, wao huwa wazungumzaji zaidi; ndio wamwaga sera na ajenda badala ya kuwapa nafasi wananchi waseme wanachotaka na kisha wao wafikishe bungeni tena kwa namna wanavyotaka wananchi na sio kwa mipasho kama tunavyoona ikifanyika kule Dodoma!

Nakumbuka kusoma tawasifu ya rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama kuna eneo katika kitabu chake anasema wakati fulani aliitisha mkutano na wananchi ili wamweleze nini cha kwenda kusema katika seneti.

Tujiulize sisi hapa kwetu, misimu ya Bunge inapofika mfano Bunge la bajeti, kuna mbunge anayekaa na wananchi wake na kuwaomba nini akakiseme atakapokuwa Bungeni?

Leo tunaona mkutano mzima wa bajeti, mbunge anaweza kuchangia hoja za wizara kadhaa, je michango katika wizara hizo anaitoa kwa maelekezo ya wananchi wake? Je, wananchi ndio wanaowatuma wabunge au wanajituma?

Tunahitaji demokrasia ya kweli ya wananchi

Nadhani tunapotafuta namna ya kuboresha demokrasia yetu, hili linapaswa kupewa nafasi ya pekee. Wabunge wawe wawakilishi wa kweli wa wananchi.

Hata neno lenyewe kuwakilisha linamaanisha kufanya kitu au kusema kitu kwa niaba ya... Wabunge wetu walijue hilo na sasa wabadilike. Kwa kuanzia ningewashauri vikao vinapokaribia bungeni kwa kuwa wanajua nini wanaenda kufanya huko, wajenge utaratibu wa kuzungumza na wananchi wao kuchukua maoni na kwenda kuyazungumza na hapa ndipo unapokuja umuhimu wa kila mbunge kuwa mkazi wa eneo analowakilisha.

Aidha, njia kama mikutano ya hadhara, mikutano ya ndani, mitandao ya kijamii kama whasapp, telegram na mingineyo inaweza kutumika kuchukua mawazo na maoni ya wananchi.

Kama ni bunge la kupitisha sheria fulani, mbunge awaulize wananchi wake wanachotaka kuhusu sheria hiyo, kwa sababu kuna uwezekano wananchi wakawa na mawazo bora zaidi kuliko aliyonayo mbunge.

Kama kuna mjadala wa kitaifa unaotarajiwa kujadiliw bungeni, aombe mawazo yao, wakumbuke wao ni wawakilishi wa wananchi.

Tukijenga tabia ya kila mbunge kukumbuka kuwa ametumwa hapo na wananchi ili kuwa msemaji wao, kwanza itapunguza hata wabunge kujiingiza katika mijadala isiyo na maana na mipasho binafsi ambayo baadhi ya nyakati huchukua sehemu kubwa katika chombo hicho.

Kama tumechagua demokrasia ya uwakilishi wa watu, hivi ndivyo inavyopaswa kuwa demokrasia hiyo. Wananchi kwanza kuliko chochote kile. Vinginevyo tukubali kuwa na hata demokrasia ya wabunge binafsi kama inawezekana.

Mwandishi ni mkazi wa Dar es Salaam. Anapatikana kwa simu barua pepe: abeidothman@gmail.com
 
Upvote 0
Back
Top Bottom