Tatizo kenya kila kabila lina chombo cha habari
Unakuta ukabila unakuzwa na vyombo hivyo
Hilo pia jana limewekwa wazi hapa
Vyombo vya habari vya lugha asili vyadaiwa kupalilia ukabila
VUGUVUGU la uhamasisho mashinani (Kengo) Jumanne limesema kuwa vyombo vya habari vinavyotangaza kwa lugha asili ni “vizalishaji vya utengano wa kijamii.”
Mshirikishi wa kundi hilo Mlima Kenya Bi Bernice Wandia akiongea Mjini Thika alisema kuwa “vyombo hivyo vinafaa kumulikwa kwa undani na mikakati iwekwe ya kudhibiti jinsi vituo hivyo husajili msikilizaji na mtazamaji wao katika makundi haramu ya ukabila.”
Bi Wandia alisema kuwa vyombo hivyo huwa na programu za kisiasa ambapo waalikwa huwa ni wa jamii yenye lugha ya kituo hicho “na ambapo katika usiri wa kinyumba huwa wanatoa matamshi hatari kwa utaifa.”
Alisema kuwa “mimi kama wa kutoka Jamii ya Agikuyu najua waziwazi kuhusu baadhi ya watangazaji wa vipindi kadha ambao kila uchao
wanachochea hisia za kikabila, kudunisha makabila mengine na pia vyama vinavyodhaniwa kuwa hasimu kisiasa.”
Alisema kuwa baadhi ya vipindi hivyo hushirikishwa na wanasiasa wabishi ambao “hawaogopi lolote katika usiri wa unyumba kurushia
makabila mengine cheche za matusi, kuwaangazia wapiga kura kutoka jamii zingine kama wasiojielewa na wanaofaa kukaliwa kisiasa kupitia
kukosa kuchagua wagombezi wao wa urais.”
Alisema kuwa jitihada zote za serikali za kuunganisha Wakenya hazitafua dafu iwapo “vyombo ambavyo vinatumika kuwasilisha jumbe hizo
za umoja ni vilevile ambavyo vina vipindi vya kutenganisha taifa.”
Bi Wandia alisema kuwa katika siku za hivi majuzi ambapo mrengo wa Cord umekuwa ukiandamana dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kumekuwa na “harakati za kina za kuangazia Cord kama muungano wa wasioaminika kisiasa na ambao hawafai kuwa mamlakani.”
Kudumisha utengano
Alisema kuwa hali ni iyo hiyo katika jamii zingine ambapo kulingana na mrengo ambao watangazaji wa vipindi wanaunga mkono, matamshi ni ya kudunisha na kuwatenganisha Wakenya.
Bi Wandia alisema kuwa “wanasiasa hutumia lugha zao za mama kuwasilisha jumbe za kukera na ambapo Mkenya wa kawaida aliye
mashinani hukumbatia mwongozo huo wa kuchukia jamii zingine na vyama vyao.
“Kuna virusi angani na hilo ni kwa uhakika. Virusi hivyo vya ukabila na utengano vinasambazwa na vyombo vya habari kupitia mitambo kuwa
mikononi mwa wakabila, wasiojumuika katika uzalendo wa umoja na walio na mtazamo kuwa jamii zao zina haki ya kuwa mamlakani kuliko zingine,” akasema.
Alionya kuwa ikiwa hatari hiyo haitatafutiwa dawa yake kama suala la dharura, wanasiasa watachoma taifa hili mitamboni ya redio, Wakenya
watabakia kugawanyishwa kwa misingi ya kidini, kisiasa na kikabila na hatimaye harakati zote za kusaka umoja wa Wakenya vibakie kuwa ndoto tu.
Bi Wandia alisema kuwa mitambo iyo hiyo ya redio inatumiwa kwa kiwango kikuu katika kupendekeza wanasiasa ambao hawafai Wakenya kwa vigezo vya huduma bora.
“Wengine wa wanahabari hao ndio wanajipigia debe kuwa wanawania nyadhifa fulani na wanatumia fursa hiyo ya kuwa wamiliki wa mitambo ya matangazo kujipia debe huku wakidunisha wapinzani wao kinyume cha sheria. Wengine wanachapia kampeni wale wanasiasa ambao wamepoteza umaarufu ili wapiga kura waanze kuwaona kwa ufaafu,” akasema.
Alisema vyombo vya habari vikiwa havitawajibila pakuu katika kuwaleta Wakenya pamoja, kutekeleza la haki kwa wote bila ubaguzi na kuzingatia maelekezo ya kitaaluma, basgi vitabakia kuwa adui wa ustawi wa taifa.