Wadau: Elimu iwe ni kipaumbele cha taifa

Wadau: Elimu iwe ni kipaumbele cha taifa

kbm

JF-Expert Member
Joined
Oct 5, 2012
Posts
5,224
Reaction score
1,677
Janeth Idrissa (siyo jina lake halisi), amehitimu kidato cha nne akiwa na cheti daraja la nne chenye alama 27.
Kwa kuwa sifa hizo zinakidhi vigezovya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, anajiunga na ualimu kozi inayomchukua miaka miwili kabla ya kwenda kufundisha.
Mwalimu huyo ni mmoja kati ya maelfu ambao wanaomba na kuchukua kozi ya ualimu, baada ya Serikali kupunguza kiwango cha alama za ufaulu kwa wahitimu wa kidato cha nne na sita wanaotaka kuchukua fani ya ualimu iwe katika ngazi ya cheti au stashahada.
Mpango huo na vivutio vingine vimewekwa ili kuwavutia watu wengi zaidi kujiunga na fani hiyo, ili kupunguza tatizo la uhaba wa walimu nchini ambao kwa takwimu za karibuni wamekuwa wakiongezeka, licha ya ukweli kuwa kiwango cha elimu nacho kinazidi kuporomoka.
Kulingana na takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, jumla ya walimu 26,537 wameajiriwa katika mwaka wa fedha wa 2012/2013.
Idadi hiyo ni ongezeko la walimu 2,630 sawa na asilimia 11 kulinganishwa na walimu 23,907 wa mwaka uliopita wa 2011/2012.
Kuporomoka kwa kiwango cha elimu nchini pamoja na mambo mengine, kunapimwa na mfululizo wa kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika mitihani ya taifa.
Licha ya sababu nyingi kutajwa, weledi mdogo wa maarifa kwa walimu, nao unaelezwa kuchangia anguko hilo la elimu.
Sababu za anguko la elimu
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mkoba anasema matokeo mabaya yanachangiwa na sababu nyingi, ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji duni wa wadau kila yanapofanyika mabadiliko kuhusu elimu.
Kwa mfano, anasema Serikali imefanya makosa makubwa kupunguza alama za ufaulu kwa waombaji wa nafasi za ualimu, bila kuwashirikisha wadau wengine na matokeo yake ndio hicho kinachoitwa mgogoro wa elimu.
Anaeleza kuwa ni jambo la hatari kuruhusu mtu aliyepata daraja la nne kwenda kuwa mwalimu shuleni, kama anavyofafanua:
“Mtu mwenye akili hafifu, anakwenda kufundisha akili changa. Ni wazi kuwa mtu huyo ameshindwa kabla hajaanza. Mfumo wa namna hiyo unaua vipaji vya wanafunzi ambavyo vinahitaji kuendelezwa, lakini vinakosa wa kufanya hivyo.’’
Kwa upande mwingine, anahusianisha kinachotokea sasa na walimu kukata tamaa, kwa kuwa wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mengi huku kilio chao kikishindwa kusikilizwa na hata kuminywa na Mahakama.
“Siwezi kuwa mtabiri wa kiama au nini ambacho kitatokea iwapo kila wanapojaribu kupumua Mahakama inawaziba pumzi” anasema na kuongeza kuwa ualimu unakabiliwa na changamoto nyingi zinazohitaji kufanyiwa kazi.
Profesa Herme Mosha ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), anasema sekta ya elimu inakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu bora katika ngazi zote na kibaya zaidi mafunzo hayawapi nafasi ya kufanya rejea ya masomo waliyofeli.
“Anapopelekwa kusoma ualimu miaka miwili mtu ambaye ana alama 30 ni kuwa tayari mtu huyo ana upungufu wa maarifa kwa asilimia sabini, hivyo bila maandalizi ya ziada tusitarajie atuzalishie ‘A’ “ anasema.
Aidha, anaeleza kuwa kumekuwa na kawaida ya kumchukulia mwalimu kama mtu anayeweza kufundisha masomo yote hata yale aliyofeli.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar esSalaam katika Shule ya Elimu, Profesa Agnes Njabili pamoja na kukosoa utaratibu wa kuwapandisha madarasa wanafunzihata wale wanaofeli, anasikitishwa na tabia iliyopo ya kuingiza ama kutoa vitu katika elimu kwa kufuatamatakwa ya wahisani.
Anasema utegemezi wa Serikali kwa wafadhili na wahisani wengineunaligharimu Taifa, kwani wageni hao wamekuwa wakishinikiza kuongezwa au kupunguzwa kwa mambo katika mitalaa ya elimu.
“Wafadhili tumewapokea kama miungu na ndiyo maana tumeingia katika kitu ambacho kinadharia tunaweza kuiita Kill education (ua elimu), kill the nation (ua taifa)” anasema.
Kwa upande mwingine, Profesa Njabili anawashukia wazazi ambao wengi wao wanashindwa kukagua kazi za watoto wao, kwa kuwa waowenyewe ni mbumbumbu.
Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi katika chuo hicho hicho, Dk Kitila Mkumbo anasema tatizo kubwa ni Taifa kukosa vipaumbele vikuu.
Anatoa mfano wa Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa ambaye alisema wazi kuwa kipaumbele chake katika uongozi wake kilikuwa ni uchumi.
“Mkapa alipoulizwa vipaumbele vyake alisema uchumi, uchumi, uchumi, lakini kwa sasa hakuna ambaye anajua vipaumbele vikuu vya Serikali...” anasema.
Anasema kuporomoka kwa elimu kumeanza tangu mwaka 2007 na hali ilikuwa mbaya zaidi mwaka 2010 na 2012. Anaeleza kwa hali ilivyo kutakuwa na shida kujaza nafasi za vyuo vikuu ifikapo mwaka 2015.
Aidha, Dk Mkumbo anasema Tanzania inatajwa kuchangia asilimia 32 katika elimu wakati nchizingine zinachangia hadi asilimia 48.
Kimsingi sekta ya elimu inahitaji mkakati wa kitaifa kuweza kuinusuru. Changamoto ni nyingi, jamii, Serikali na wadau wa elimu kwa jumla wanapaswa kukaa mezamoja kutafuta namna ya kuinusuru Tanzania kielimu.
Njia moja thabiti ya kupambana na hali ya sasa ni kuifanya elimu kuwa kipaumbele cha taifa. Kwa kufanya hivyo, Serikali itawekeza vilivyo katika sekta hii mama kwa maendeleo ya taifa.

CHANZO: MWANANCHI
 
Back
Top Bottom