Hongera kwa kufikiria kufanya biashara lakini kwa sasa huna tofauti sana na hao wenzio waliokopa na kununua magari. Walionunua viwanja hawajapotea sana labda kama wamenunua bonde la mpunga. Wakifulia wanaweza kuviuza au kuvitumia kama rehani kukopa. Mpaka sasa nadhani aliyekukopesha keshaanza kukata hela yake na riba wakati hela uliyochukua imekaa tu ikizidi kushuka thamani kama magari ya wale wafanyakazi wengine.
Kuhusu hiyo biashara unayotaka kufanya wengi wameshasema mengi na kuhoji maswali ya msingi sana. Mi nachojua hakuna kanuni maalum ya kuanza biashara ila kuna mambo ya msingi yasipozingatiwa biashara inakufa. Mi nilipata wazo la kufanya biashara baada ya kuona msingi wa fremu unachimbwa. Kwa kutambua uzuri wa eneo lile kwa maana ya idadi ya watu (wateja watarajiwa) nikaenda kuwahi fremu bila kujua nitafanya biashara gani. Baada ya kulipia hela ya kushika fremu ndo nikaanza kufikiri cha kufanya. Nilipopata wazo nikaenda kukopa. Mwaka wa kwanza na wa pili biashara ilikuwa tamu mno. Hela niliyokopa ilirudi ndani ya mwaka wa kwanza. Mwaka wa pili waswahili kama kawaida wakaona nafaidi wakaanza kufanya biashara kama yangu. Akaanza wa kwanza, wa pili...mi nikaendelea tu bila kuchukua tahadhari yoyote ya kukabiliana na ule ushindani. Baadae wakafika kama 6 hivi. Tukajikuta kila mtu anapata wateja "wawili wawili", maisha ya kibiashara yakaanza kuwa magumu, nikafikia mahali pa kuhudumia biashara kwa hela ya mshahara. Mwishowe nikaamua kuifungia mbali na hela za mtaji nikazipeleka benki ili nijipange upya. Loh!
Kwa tahadhari tu fanya kama walivyokushauri wale waliosema hiyo hela weka kwenye akaunti yenye riba mpaka utakapokuwa tayari, au baada ya kuwaona washauri wa biashara wekeza kwenye biashara ambayo imeshaanza we uwe unakula faida japo itakuwa ndogo (mi naitaka hii na nitaomba mawazo zaidi) kwani mojawapo ya mambo niliyojifunza kama mfanyabiashara ambaye ni mwajiriwa na sijataka kuachia ajira ni ugumu wa kuwatumikia mabwana wawili. Biashara nyingi zinahitaji usimamizi wa karibu sana hasa mwanzoni; utaweza kujigawa au utakuwa kama walimu wa shule kama benjamin mkapa wanapiga hata miezi miwili hawajakanyaga darasani? Kuna mwenzangu alikopa m 10 akafungua biashara nzuri sana lakini ilimlipa miezi kama 5 wafanyakazi wakamzidi ujanja, ikafa kifo cha mende. Alipouza kilichokuwa kimebaki aliambulia m 2 tu.
Mwingine aliyekopa kama wewe kabla ya kujua anachotaka kufanya, alijikuta ameanza kuchomoa hapo kidogo kidogo. Alichofanya ni kuzibadilisha zikawa dola ili kuepuka vishawishi vya kuzivuta kwa simu toka akaunti ya akiba ya madafu, lakini pia sijui uchumi ila nadhani zikiwa dola ni salama kuliko madafu kwa maana ya ile hatari ya kushuka thamani.
Kila la heri.