Rare Sapphire
JF-Expert Member
- Jul 24, 2021
- 590
- 1,648
Babati. Wimbi la wadudu waharibifu wa mazao maarufu kama “mbirizi” limevamia mashamba ya mahindi ya wakulima katika kata ya Kiru na vijiji vya jirani wilayani Babati mkoani Manyara.
Mkulima wa mahindi kutoka kijiji cha Kiru, Six Salao akizungumza leo Jumanne Desemba 27, 2022, amesema makundi makubwa ya mbirizi hao wanashambulia mazao ya mahindi.
Salao amesema wadudu hao ni wengi na wamejazana kwenye mashamba yao kama nzi mara baada ya msimu huu wa mvua kuanza kunyesha.
Mbunge wa zamani wa jimbo la Babati Vijijini, Vrajlal Jituson amesema wadudu hao wamevamia mashamba ya mahindi katika bonde la Kiru, hivyo wananchi wanapata hofu ya kuharibiwa kwa mazao yao.
“Wakulima wameanza kupiga dawa, hawajaisubiri serikaili ila kuna haja mamlaka husika za serikali zikajua na kuanza kutafuta mbinu za kuwatokomeza wadudu hao,” amesema Jituson.
Mkazi wa Babati, Theodora Hams amesema miaka iliyopita wazee wa eneo hilo waliwaeleza kuwa endapo wadudu hao wakivamia mashamba, ni ishara nzuri kuwa msimu huo utakuwa na mavuno mengi.
Kwa upande wake, kaimu ofisa kilimo wa mkoa wa Manyara, Samwel Dahaye amesema wadudu hao viwavijeshi vamizi waliozoea kuitwa mbirizi, hivi sasa wamejazana kwenye kata hiyo na vijiji jirani.
Dahaye amesema njia pekee ya kuwaondoa wadudu hao ni wakulima kuchukua hatua za haraka za kupiga dawa ambazo wameshauriwa na wataalamu wa pembejeo za kilimo.
“Njia nyingine ni wakulima wakague mashamba yao mara kwa mara na kuhakikisha wanaweka dawa kwenye kiini cha mche ili kuendeza ustawi,” amesema Dahaye.
Mwananchi