Akizungumza wakati wa tukio hilo, Agapinus Tax, Mkurugenzi wa `Viatarishi na Uzingatiaji wa Sheria kutoka Vodacom Tanzania, alieleza kuwa msafara wa mwaka huu utapita katika mikoa 11 na utahusisha waendesha baiskeli wa kimataifa kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Botswana, DRC, Zambia, Malawi, Afrika Kusini, Marekani, Uholanzi na Nigeria.
“Zaidi ya waendesha baiskeli 200 watashiriki safari hii kutoka Dar es Salaam hadi Butiama. Kati yao, 50 watarudia njiani huku 150 wakitarajiwa kufika hadi mwisho wa safari,” alisema.
Msafara wa mwaka huu umekusanya washiriki kutoka kila kona ya Tanzania ikiwemo Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Lindi, Mbeya, Kagera, Dodoma, Pwani na Tabora, pamoja na wale wa kimataifa kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Botswana, DRC, Zambia, Malawi, Afrika Kusini, Marekani, Uholanzi na Nigeria.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, msafara wa Twende Butiama umetoa mafanikio makubwa ikiwemo kupanda miti zaidi ya 100,000, kufikia watu 23,000 kupitia huduma za afya kwa njia ya kliniki tembezi, kugawa madawati 1,900 kwa shule 32 za umma, na kutoa baiskeli 50 kwa wanafunzi waishio mbali na shule.
Mwaka huu, waandaaji wanalenga kufikia shule 10 zaidi, kupanda miti 50,000, na kuwafikia Watanzania zaidi ya 700,000 wakiwemo watoto, vijana na wazee.
Akizindua rasmi tukio hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alisema kuwa msafara huu si tu kwa ajili ya kumuenzi Mwalimu Nyerere, bali pia ni chombo muhimu cha kuhamasisha afya na maendeleo ya jamii:
“Msafara huu ni kumbusho la umoja na uzalendo. Washiriki wanapata fursa ya kujifunza historia kwa njia ya vitendo. Serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwa sekta za michezo, utamaduni na jitihada za kulinda mazingira,” alisema.
Naye Mwanzilishi Mwenzake wa msafara huo, Gabriel Landa, alieleza kuwa safari hiyo itaambatana na shughuli mbalimbali za kijamii zenye kugusa maisha ya wananchi, zikiongozwa na maono ya Mwalimu ya kupambana na ujinga, maradhi na umasikini.
“Waendesha baiskeli watashiriki katika shughuli za utunzaji wa mazingira ikiwemo upandaji miti kwenye maeneo ya Mlima Kilimanjaro na chanzo cha Mto Pangani ili kusaidia kuhifadhi mazingira,” alibainisha.