Wafanyakazi 600 wa Ticts wagoma Dar es SalaamNa Sadick Mtulya
WAFANYAKAZI 600 wa Kampuni ya Kupakia na Kupakua Makontena Bandarini (Ticts), jana waligoma kufanya kazi kwa lengo la kuushinikiza uongozi wa kampuni hiyo kutimiza makubaliano sita waliyoafikiana katika mikataba yao ya hiari.
Pia, walishinikiza kuondolewa kwa Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Neville Bisset na Meneja Utumishi, James Rhombo kwa madai kuwa ndio kikwazo katika kumaliza matatizo yao.
Wafanyakazi hao walidai kuwa Ticts imeshindwa kutekeleza ahadi ya kuwapandishia ngazi ya mishahara kwa zaidi ya miaka tisa, kuwanyima hisa zao za asilimia tano na kwamba, madereva wa matrekta kufanya kazi kwa zaidi ya saa tisa bila kupata muda wa kula.
Pia wanapinga kitendo cha wazungu kulipwa fedha nyingi tofauti na wao, kupewa kati ya Sh 5,000 na Sh10,000 kama posho ya ufanyaji kazi katika mazingira magumu kinyume cha makubaliano katika mkataba ambapo walikubaliana kulipwa Sh35,000 na zaidi kwa siku.
Mbali na posho pia walipinga hatua ya kulipwa Sh75,000 tu badala ya Sh 150,000, inayotokana na upakuaji na upakiaji kwa wastani wa makontena 16 hadi 22 kwa mwezi.
Mgomo huo ulisababisha taharuki kubwa kwa mawakala na madereva waliokuwa wamejaa nje ya ofisi za Ticts na zaidi ya malori 300 yalishindwa kuondoka bandarini hapo kwa kukosa huduma za upakiaji makontena ya mizigo.
Wakizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wafanyakazi hao walisema mgomo huo hautamalizika hadi hapo uongozi waTicts utakapokubali kutimiza makubaliano hayo ambayo ni ya muda mrefu.
Tulikuwa katika kikao, lakini hadi muda huu (saa 4.00 mchana) hatujaafikiana chochote, wao wanataka tuendelee na kazi sisi tumewaambia hatuko tayari kufanya kazi hadi makubaliano yetu yatekelezwe, alisema mmoja wa wafanyakazi hao ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na afisa kutoka wizara ya Miundombinu kilishindwa kufikiwa muafaka kutokana na kutokuwepo kwa Mkurugenzi Mkuu ambaye anadaiwa kuwa safarini Hong Kong, China.
Wafanyakazi hao walisema wamefikia uamuzi huo, baada ya kuchoshwa na kauli tata za vingozi wao kuwa Ticts haina pesa za kuwalipa.
Mambo yakizidi tutatoa orodha kuonyesha Wazungu wanavyolipwa na kuishi maisha ya kifahari, huku sisi wafanyakazi tukinyimwa haki zetu kwa kisingizio kampuni haina pesa.
Ni mwaka jana tu Mkurugenzi Mkuu aliyeondoka David Cotty alikuwa akilipwa Sh28 milioni kwa mwezi huyu wa sasa itakuwaje?, alisema na kuhoji.
Wafanyakazi hao ambao wanaingia kwa awamu mbili (usiku na mchana), walisema pamoja na mgomo wao huo, ambao ni wa tatu wataendelea kufika kazini kama kawaida, lakini hawatafanya kazi na kwamba wako tayari kuachishwa kazi.
Uongozi wa Ticts haukuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari waliofika ofisini hapo ili kupata ufafanuzi wa madai ya wafanyakazi hao.
Wakala wa kampuni ya Sure Freight, Erasto Mduma alisema mgomo huo umeongeza gharama kwao kutokana na kuongezeka kwa siku za mizigo kukaa bandarini hapo.
Taratibu za hapa ni kuwa zikizidi siku 7 bila kutoa mzigo wako kwa kontena lenye futi 20 unalipishwa dola 20 na la futi 40 unalipishwa dola 40. Sasa mtu una makontena zaidi ya 40 unaingia gharama pasipo sababu yoyote, maana haijulikani mgomo huu utaisha lini, alisema Mduma.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Bandarini hapo, Nasson Sengo alisema zaidi ya magari 150 yanayokwenda nje na ndani ya Tanzania yameshindwa kupakia makontena ya mizigo kutokana na mgomo huo.
Kwa upande wetu tumeathirika na muda na hadi sasa mashine zote za block b, c, d na e zimezimwa na hakuna kinachofanyika. Kawaida kuanzia asubuhi hadi jioni zaidi ya magari 150 huondoka hapa yakiwa yamepakia makontena ya mizigo na hivyo hivyo usiku, alisema Sengo.
Sengo aliongeza kuwa kwa kawaida wafanyakazi hao hupakia mizigo katika gari moja kwa muda usiozidi dakika 10. Uchunguzi uliofanywa na Mwanachi uligundua kuwa mgomo huo ulianza wiki iliyopita kwa wafanyakazi kupunguza kiwango cha utendaji kazi tofauti na awali.