WAFANYAKAZI wa kampuni ya Guardian Ltd wameandamana kupinga kuachishwa kwao kazi bila taratibu kufuatwa zinazositahili wakati wa kumuachisha kazi mfanyakazi yeyote yule.
Wafanyakazi hao walioandamana hadi katika ofisi za gazeti la Mwananchi walidai kuwa hawakuridhishwa na kitendo walichofanyiwa na mwajiri wao kuwaachisha kazi bila kufuata taratibu na kwamba walipewa notisi ya siku moja baada ya hapo waliambiwa kuwa siyo wafanyakazi wa kampuni hiyo hali ambayo iliwashangaza na kuwaweka katika wakati mgumu.
Aliwaachisha kazi jumla ya wafanyakazi 134 na kwamba walikuwa wamedhaminiwa na kampuni ( IPP) kuchukua mikopo benki na walikuwa wameishapewa mikopo hiyo, lakini walishangaa kwenda benki na kukuta hundi zao zimezuiliwa kwani walipewa taarifa kuwa mwajiri wao alituma barua benki kwamba wasipewe pesa tena.
"Nilikuwa nimepata mkopo benki lakini nilishangaa kwenda na kukuta taarifa za kwamba hundi yangu imesitishwa na bosi wangu, pia utaratibu alioutumia ni wa kuumizana maana tulifukuzwa kama mbuzi na wengine waliuopewa mafao yao ni ya kusikitisha,"alisema Edward Kabaye aliyefanya kazi miaka 18 na kupewa Sh milioni 2.
Waliendelea kudai kuwa kila wakidai madai yao wanaambiwa kuwa waende popote watakapotaka kwenda na kwamba kuna baadhi yao waliofanya kazi zaidi ya miaka kumi lakini waliondolewa bila kupewa malipo yao hali ambayo imewafanya washindwe kurudi kwao kwani wengi wao huku sio kwao.
Walidai pia kuwa wanachokitaka kwa mwajiri wao awaite na awapatie haki zao ingawa kwa sasa anajifanya kama hana habari na kilio cha wafanyakazi hao na huku wamemfanyia kazi kwa muda mrefu anashindwa kuwa na fadhila na kusahau umuhimu wao.
"Nilidhani wakati wa kufanya ukatili huu mtu kama mimi mlemavu asingenidhurumu haki yangu kama unavyoniona mguu wangu una matatizo, kwani nilikuwa nikiona tajiri yetu akitoa misaada kwa walemavu kumbe ni kuwazuga watu,"alisema Joseph Mshamu.
Katika kundi lililofika Mwananchi kulikuwepo walemavu wanne wote wakielezea matatizo wanayoyapata baada ya kufukuzwa na kwamba wanaishi maisha magumu na huku wamefanya kazi kwa muda mrefu lakini kutokana na unyama waliofanyiwa unawaweka katika wakati mgumu.
"Kweli naishi maisha ya taabu ukilinganisha na hali yangu ilivyo kama angekuwa anasaidia kweli walemavu siangenisaidia mimi kwa kunilipa madai yangu yote, lakini kanitelekeza hadi sasa sina mahali pakwenda sikutegemea kama Mengi angenifanyia hivi,"alisema Sultan Said mlemavu.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mkurugenzi Mtendaji Kiondo Mshana, alisema hakuwa na nafasi jana kulizungumzia suala hilo akaomba apewe muda kwa kuwa alikuwa akishungulikia masuala mengine ya kiofisi.