JESHI la Magereza, limeingia katika kashfa nzito baada ya nyapara mkuu wa wafungwa katika Gereza la Butimba mkoani hapa kuuawa kwa kuchomwa visu na wafungwa wenzake juzi mchana.
Nyampara huyo aliyetajwa kwa jina moja la Kishiwa, aliuawa chumbani kwake wakati akila chakula cha mchana, baada ya wafungwa wenzake kumfuata na kufunga mlango, kisha kumkaba na kumchoma visu sita shingoni, ubavuni na kifuani.
Imedaiwa kuwa wafungwa wengine walishuhudia watuhumiwa hao wakiingia ndani mwake, kabla ya kusikia tafrani kubwa iliyowafanya wavamie chumba hicho na kukuta mkuu wao kauawa.
Watuhumiwa hao walishambuliwa vibaya kwa kipigo na wafungwa wenzao pamoja na baadhi ya askari magereza kiasi cha kulazimika kupelekwa hospitali kupata matibabu.
Habari za kina kutoka ndani ya gereza hilo zilizothibitishwa na Kamishna Mkuu wa Magereza nchini (CGP), Augustine Nanyaro na viongozi wengine waandamizi, zilisema chanzo cha mauaji hayo ni hali ya kutoelewana baina ya wafungwa wanaotumikia vifungo virefu.
Hata hivyo, kuna madai kwamba mauaji hayo yamechangiwa na uzembe wa uongozi wa gereza hilo wa kushindwa kuyafanyia kazi malalamiko ya siku nyingi ya wafungwa, yakiwemo ya ukatili, ingawa Mkuu wa Gereza, Kamishna Masidizi (ACP), Edson Yalimo, alikwepa kukwepa kutaja kiini halisi.
Baadhi ya askari magereza ambao waliomba kuhifadhiwa majina yao, walisema kwa muda mrefu wafungwa wamekuwa wakimtuhumu nyapara huyo kuwa ana uongozi wa kibabe ambao unakumbatiwa na viongozi wakuu wa gereza.
Nyapara huyo alikuwa ni kama mkuu wa gereza, chochote ambacho alikuwa akisema ndicho kilichokuwa kikifuatwa na uongozi wa gereza, alisema askari mwingine.
Kwamba hata kwa nyakati tofauti walipokuja viongozi wa Makao Makuu, Naibu Kamishana wa Magereza (DCP), John Minja, na Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Magereza (SACP) Mkoa wa Mwanza, RPO Raphael Mollel, wafungwa walitoa malalamiko yao kuhusu nyapara huyo, lakini waliishia kupigwa na kuandikishwa maelezo.
Habari zinasema wafungwa hao walimwambia Kamanda Minja kwamba kama hawamwondoi nyapara huyo, watafanya tukio kubwa lisilokuwa la kawaida, ikiwemo kuua askari au nyapara mwenyewe.
Sisi askari tunajua ni mwiko kupuuzia taarifa yoyote ya kialifu, tunashangaa ni kwanini mkuu wa gereza na viongozi wengine walipuuzia taarifa hizi, alisema askari mwingine.
Mkuu wa Magereza nchini, Nanyaro, alikiri kutokea kwa tukio hilo, lakini akasema kuwa alikuwa safarini mkoani Mbeya na hivyo ameagiza apatiwe taarifa kamili ndipo aweze kutoa taarifa.
|
|