Wageni wetu kutoka SADC karibuni Tanzania

Wageni wetu kutoka SADC karibuni Tanzania

Joined
May 3, 2019
Posts
53
Reaction score
144
KARIBUNI TANZANIA WAGENI WETU KUTOKA SADC.

Leo 13:15pm,04/08/2019.

Karibuni Tanzania,ardhi ya Kilimanjaro,Zanzibar na Serengeti, ardhi yenye mbuga kubwa barani Afrika,Mbuga ya Selous,Taifa la watu wazuri wenye upendo mkubwa,undugu ni sehemu yetu ya maisha,Karibuni wageni wetu katika ardhi ya Ujamaa ulioanzishwa na Mwalimu Julius Nyerere.

Karibuni wageni wetu katika Taifa lililoasisiwa na Julius Nyerere na sasa linaongozwa na Rais John Magufuli,Taifa la Waafrika wote,Kuanzia wapigania uhuru Rais wa kwanza wa Namibia Samueli Shafiishuna Daniel Nujoma maarufu kama Sam Nujoma,Samora Machel,Edward Mondlane,Nelson Mandela,Kenneth Kaunda,Robert Mugabe wote walijifunza tamaduni mbalimbali walipopata bahati ya kuishi Tanzania.

Rais Sam Nujoma aliyepata kuishi Kongwa,Wilaya ya Dodoma,alipata pia kuishi Njombe na Iringa alijifunza kuongea kigogo akiwa Kongwa wakati Rais wa kwanza Msumbiji,Samora Machel alifanya kazi kama Mganga msaidizi,Wilayani Kongwa,Mkoani Dodoma huku baadhi ya askari wapigania Uhuru waliokuwa mafunzoni hapo Kongwa kutoka Angola,Zimbabwe,Afrika ya Kusini,Shelisheli,Comoro na Guinea Bissau wakifika vijijini na kunywa pombe za kienyeji na wenyeji wa Kongwa zikiwemo primisi inayotengenezwa kwa mchuzi wa Tangawizi na Choya inayotokana na juice ya tunda la Alover.

Karibuni ndugu zetu kutoka kusini mwa bara la Afrika,Afrika ni moja na sisi ni ndugu,Ndio,Tanzania ni alama ya tumaini na ukombozi katika bara la Afrika,Tanzania ilijitoa kwa hali, damu na mali nyingi kwa ajili ya Ukombozi wa nchi za SADC na nyingine nyingi.Tanzania haikuweza kukaa ikiwa huru huku sehemu kubwa ya Afrika ikiendelea kutawaliwa.

Baba wa Taifa alikuwa muumini wa ile imani kuwa huwezi kuwa huru majirani zako wakiwa hawapo huru au hawana amani,na hilo lipo tunaweza kulithibitisha na machafuko yaliyotokea Somalia ,Burundi na Rwanda si tuu yalileta wakimbizi bali pia yalileta wanajeshi waasi hadi ndani ya mipaka yetu.Hivyo basi ilikuwa ni muhimu kwa Afrika nzima kuwa huru ili bara la Afrika liweze kupiga hatua za kimaendeleo.

Katika mkutano wa OAU mnamo mwaka 1963 ,iliundwa kamati ya ukombozi ya iliyokua Umoja wa nchi huru za Afrika(OAU).Tanzania ikawa kituo cha wapigania uhuru na mafunzo ya kijeshi.Eneo la Kongwa(sasa ni wilaya) Wilaya ya Kongwa ikawa kituo cha mafunzo ya kijeshi kilichopokea wapigania Uhuru toka nchi za Msumbiji,Namibia,Zimbabwe,Angola,Afrika ya Kusini na nyinginezo zilizipo chini ya jangwa la Sahara.

-Upendo wa Watanzania kwa bara la Afrika.

Wakati nchi nyingine zikiona hakuna umuhimu wa kuwekeza nguvu nyingi kwenye ukombozi wa Afrika,kuwa bize katika kuimarisha Uchumi wao Julius Nyerere alikuwa bize kwenye "ukombozi wa Afrika" baadae Kenya ikapata Uhuru na vile vile Uganda.

Tuliitoa nchi yetu sadaka na kukubali nchi yetu kuwa hifadhi na maficho ya wapigania uhuru wa nchi nyingine. Vijana wetu wengi wakiwa jkt walijitolea kwenda kwenye vita ama uwanja wa mapambano kwa ajili ya ukombozi wa bara zima la Afrika. Vita ambavyo kihalisia havikua vyetu ila kwasababu sahihi ama zisizo sahihi lakini kwa Upendo mkubwa kwa bara letu la Afrika, tulitoa hifadhi, mafunzo ya kijeshi, fedha na kuweka takribani asilimia 30% ya budget yetu kwa ajili ya kusaidia juhudi za mapambano katika kulikomboa bara la Afrika.

-Bila ya Umoja,Afrika haitakuwa na mafanikio sasa na baadae - Julius Nyerere.

Kauli hii iliyotolewa na Rais Julius Nyerere miaka arobaini iliyopita ndiyo ilikuwa chachu ya uanzishwaji wa Jumuiya hii ya SADC,na kwa hakika kauli hiyo inaishi katika nchi 16 wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC).

SADC ambayo awali ilijulikana kama jukwaa la kuratibu harakati za maendeleo kusini mwa bara la Afrika (SADC) kikiwa chombo cha nchi za mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na utawala usiozingatia demokrasia kusini kulitokana na mchango wa Tanzania Kuziunga mkono nchi hizo,shukrani kwa Rais Julius Nyerere aliyekuwa chachu ya uanzishwaji wa Jumuiya ya SADC.

-Kuundwa kwa SADC.

Ushirikiano wa SADC ulianza kama kundi la mstari wa mbele pale Lusaka,Zambia mnamo Mwaka 1980.Viongozi wa nchi tisa walikutana wakiwamo Mwalimu Julius Nyerere,Samora Machel,Robert Mugabe na Mwenyekiti Kenneth Kaunda.

Mkutano wa pili mkubwa ulifanyika baada ya Namibia kupata Uhuru,Viongozi 16 wakakutana Windhoek, Namibia mnamo Agosti 17,1992 ambapo ikaundwa rasmi SADCC kama Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika ikiwa na malengo ya Kimaendeleo katika ukanda wa kusini mwa Afrika.

Baadae jina likabadilika kutoka SADCC nakuwa SADC ambayo makao makuu yake yakawa Gaborone,Botswana ikiwa na malengo ya kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi,mtangamano,siasa,ulinzi na Usalama na jumla ya nchi wanachama ni 16.

-Marais 16 wa Afrika,kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere.

Karibuni Tanzania,Marais 16 wa nchi wanachama wa Sadc,Karibuni wageni zaidi ya 1,000 watakaoambatana na ugeni wa Marais 16 katika jiji la Dar es Salaam wakati wa mkutano wa 39 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc).

Rais John Magufuli, ambaye sasa ni Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo atakabidhiwa rasmi Uenyekiti na kuongoza kwa mwaka mmoja mpaka Agosti mwakani.

Katika mkutano huo wa 39, Rais Magufuli atapokea kijiti cha Uenyekiti wa jumuiya hiyo kutoka kwa mtangulizi wake, Rais wa Namibia, Hage Geingob anayemaliza muda wake.

Wakuu wa nchi 16 watakaohudhuria mkutano huu wa 39 wameleta ombi maalumu kufanya kumbukizi ya Julius Nyerere watakapokuwa hapa nchini. Hii ni pamoja na kutambua mchango mkubwa wa Julius Nyerere toka kumpa Nelson Mandela kitambulisho cha kusafiria kilichoandikwa "Huyu ni Nelson Mandela,apatapo matatizo arudishwe Tanzania na si Afrika Kusini" chini kilisainia na Julius Nyerere,Rais wa Tanzania,pia kuwapa makazi Marais takribani sita waliokuwa wakitafutwa na Serikali za Wazungu na makaburu katika nchi zao,hii itaendana na kumbukumbu na ku-identify (kutambua) maeneo yote ambayo wapigania uhuru wa nchi mbalimbali waliishi huku wakipata mafunzo mbalimbali ya kijeshi kwa ajili ya kuzikomboa nchi zao.

Viongozi wengi wa nchi za kusini mwa Afrika wamewahi kuishi nchini na wengi walikuwa na ofisi katika jiji la Dar es Salaam.

Wakuu 16 wa Sadc wameomba kupitia nyumba zote walizokaa mfano Jacob Zuma (rais mstaafu wa Afrika Kusini) Sam Nujoma (rais mstaafu wa Namibia) na wengine wengi,ni kumbukumbu ya kusisimua na historia ya kishujaa kwa bara la Afrika.

Ahsante Mwenyezi Mungu kwa kumpa moyo wa Upendo,Rais Julius Nyerere hata kuifanya Tanzania kuwa nyumbani kwa kila Mwafrika,Ahsante Mwenyezi Mungu kwa Kuibariki Tanzania,Ahsante Mwenyezi Mungu kwa kumbariki Rais John Magufuli,Tupe neema ya kutumia vyema rasilimali zetu ili ziinufaishe Tanzania na watu wake wote.

Nikiishia hapa,Mimi ni,
Msemakweli Chakubanga.
Dar es Salaam.
0755078854.
 
Back
Top Bottom