Mentor
JF-Expert Member
- Oct 14, 2008
- 20,328
- 23,909
Au ni Wivu tu?
Ghafla kwa mbali nikaona gari linakuja nyuma huku limewasha taa za dharura (sirens). Sikuwa na haraka sana kulipisha kwani kama mita 100 mbele yangu kulikuwa na kizuizi cha Polisi. Nilijua hakika lazima watapunguza mwendo. Lakini pia akili yangu ilishtuka nilipokumbuka kuwa eneo lile palikuwa na kiashiria cha mwendo kikionesha mwendo usizidi km 50 kwa saa. Hapo ndipo nilipogundua kuwa dereva huyu hakuwa na nia ya kupunguza mwendo wala kusimama.
Nilisogeza gari langu pembeni huku nikiwaza sana kwa nini gari lile lenye namba za kiraia lilikuwa na taa za dharura. Kama sijaondoka kwenye wimbi la mawazo hayo niliona mbele yangu dereva yule alivyomkwepa kwa ustadi askari aliyekuwa barabarani akikagua magari mengine. Niliogopa maana hakika alionesha umahiri binafsi. Nilimsifu kuwa lazima atakuwa dereva mzoefu maana kwa hali ilivyokuwa, hakukuwa na njia ya kumkwepa yule askari.
Tukio hili limenikumbusha ambavyo siku za karibuni kumeibuka wimbi kubwa la magari ya kiraia (au yanayoonekana ya kiraia) kuweka taa za dharura (siren). Nikaelekea kwenye sheria inayoelezea magari ya dharura, Sheria ya Usalama Barabarani (CAP 168, The Road Traffic Act) kifungu cha 54. Nikasoma na kurudia lakini sikuona mahali ambapo magari haya yenye namba za kiraia yanaruhusiwa kuweka taa hizo. Na kinachokwaza zaidi ni pale ambapo wanavunja sheria waziwazi na hata kusababisha ajali kwa magari mengine kwa kisingizio cha ‘taa za dharura’.
Eeh Waziri husika, maana sheria imesema 54(5) kuwa magari haya ya dharura yanaweza kuongezwa na Waziri kupitia gazeti, naomba nijulishwe gazeti lililotoa kibali cha magari ya kiraia kuweka taa za dharura.
Afande IGP, ni mpaka siku askari wako agongwe na haya magari au mbaya zaidi, magari haya yatumike kwenye uhalifu ndipo labda tutaamka? Maana katika magari yasiyotii sheria za barabarani haya yanaongoza. Na askari wengi huwa hawayasimamishi hata yakiwa yamevunja sheria kwa kuogopa ‘taa za dharura’.
Lakini pia kuna kasauti kanakuja kichwani kikiniambia, "au ni wivu wangu tu...kwa kuwa sina gari la kuweka taa za dharura?????"