Mengi asubiri misuli ya Masha
Na Ramadhan Semtawa
MFANYABIASHARA maarufu nchini, Reginald Mengi hajawasilisha uthibitisho wa madai yake aliyotoa hadharani kuwa waziri mmoja kijana anataka kumuhujumu biashara zake, na sasa zamu ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha kuchukua hatuia baada ya siku saba kuisha.
Masha, ambaye ni mwanasheria, alimpa Mengi siku saba kuwasilisha uthibitisho wa madai aliyoyatoa kwa waandishi wa habari kuwa kuna waziri kijana aliyewasilisha hoja katika kikao nyeti ya kutaka mfanyabiashara huyo abambikiwe kodi kwenye biashara zake ili ashindwe kuzilipa na hivyo kufilisiwa.
Siku hizo saba ziliisha jana huku mamlaka za usalama wa raia zikiwa hazijapokea uthibitisho wowote kutoka kwa mfanyabiashara huyo, wala maelekezo kutoka kwa Waziri Masha, ambaye ameripotiwa kuwa safarini nje ya nchi na ambaye alionya kuwa iwapo mmiliki huyo wa makampuni ya IPP atashindwa kuwasilisha uthibitisho, atachukuliwa hatua za kisheria.
Lakini inaonekana Mengi ametunisha msuli kusubiri kuona waziri huyo akichukua hatua hizo.
Hadi jioni saa 11:30 jana, Mengi hakuwa amewasilisha uthibitisho huo, si wizarani wala makao makuu ya Jeshi la Polisi, huku waziri huyo akielezewa kuwa Geneva, Uswisi ambako yumo katika msafara wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuhudhuria mkutano wa wa kimataifa wa wakimbizi.
Mengi aliripotiwa kuwa mkoani Arusha kwa shughuli za kijamii.
Akiongea na Mwananchi, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Kamishna Robert Manumba aliweka bayana kwamba hadi jana hawakuwa wamepata maelekezo ya serikali kuhusu namna ya kushughulikia suala hilo.
Naye msemaji mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga alithitibisha kwamba hadi jana jioni Mengi hakuwa amewasilisha taarifa yoyote wizarani.
Alisema baada ya kuisha kwa siku saba alizopewa mfanyabiashara huyo, kinachosubiriwa ni kuona hatua ambazo zitachukuliwa kwa mujibu wa Waziri Masha.
"Kwa kuwa alipewa barua ya wiki moja na wiki imekwisha, tusubiri tuone hatua itakayofuata, nafikiri tusubiri waziri atakachosema hapo baadaye," alifafanua.
Msemaji huyo aliongeza kuwa hakukuwa na mawasiliano yoyote na Mengi na hakukuwa na haja ya kufanya hivyo kwani, tayari alipewa barua na waziri hivyo alichopaswa kufanya ni kujibu.
"Yeye alipewa barua, kwa hiyo hakukuwa na haja ya kufanya naye mawasiliano alichopaswa kufanya ni kujibu tu barua ya waziri," alisisitiza msemaji huyo mkuu huyo wa wizara.
Kutowasilishwa kwa ushahidi huo kunamaanisha kuwa Masha sasa anasubiriwa kuchukua hatua dhidi ya mfanyabiashara huyo, ambaye pia aliwahi kupambana na aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Utawala Bora, Wilson Masilingi, katika serikali ya awamu ya tatu.
Habari kutoka kwa watu walio karibu na mfanyabiashara huyo zinasema kuwa Mengi ameweka msimamo ambao haubadiliki kuhusu tuhuma hizo na kwamba badala ya kuwasilisha ushahidi, ni vema waziri huyo akaenda mahakamani.
Awali Mengi alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa kipindi hicho cha siku saba ni kirefu na kwamba ni vema hata angetoa siku moja.
Msemaji wa Mengi, Abdulhamin Njovu hakutaka kuzungumzia suala hilo baada ya Mwananchi kuwasiliana naye kwa njia ya simu.
Sakata hilo tayari limechukua sura na mwelekeo tofauti kutokana na maoni ya watu kugawanyika. Baadhi wanamtetea mfanyabiashara huyo na kuishushia lawama serikali, wakati wengine wanampinga mfanyabiashara huyo na kuitetea serikali.
Wiki iliyopita, Baraza la Wazee Mkoa wa Dar es Salaam, bila ya kutaja majina lilitoa tamko kali ambalo liligusa pande zote mbili kwenye mgogoro huo, likiweka bayana kuwa kauli zinazotolewa si fikra za Watanzania, bali ni utashi binafsi wa kibiashara na kisiasa.
Lakini viongozi wengi wa vyama vya siasa wamemtetea Mengi na kulaumu serikali kwa kufanya njama dhidi ya wafanyabiashara wazalendo.