SoC01 Wakati wa kushamiri kwa maovu ni wakati kwa wenye akili timamu na uzalendo wa kweli kupitia magumu

Stories of Change - 2021 Competition
Joined
Jul 22, 2021
Posts
7
Reaction score
5
Na Nkuruma wa Karne ya 21.

KATIKA Namna zote za kutafuta suluhu ya changamoto za watu, maridhiano na amani, mbinu iliyofeli ni Vita/ matumizi ya nguvu na ubabe.

Wengi huamini hili pindi wawapo katika jamii halisi lakini waingiapo katika fursa za uongozi hasa wa kisiasa huipoteza imani hii hasa pale wanapojikuta wanaulinzi wa watu wenye silaha na wenye mamlaka mbalimbali za mamzi katika jamii zao.

Taratibu hujikuta wanaona wanao uwezo wa kuamua lolote likawa, wanauwezo wa kuamua Nani limtokee lipi na ikawa na hujikuta wanajiona ndio wanaostahili kuwa watu katika watu na kwamba yeyote anayefikiri kama wafikirivyo wao Basi ndiye Mwenye akili na anayefaa kuishi kwa amani lakini afikiriaye tofauti na wanapoishia wao basi hajitambui na pengine hastahili kuishi.

Nelson Mandela, aliyekuwa Mpigania Uhuru wa Taifa la Jamhuri ya Afrika Kusini na baadaye kuwa Rais wa Kwanza mweusi wa Taifa hilo aliamini kuwa Mashauri ya jamii yanapaswa kuamriwa kwa njia za mazungumzo ya amani na si ubabe ama kubeza wale wanaolalamika iwe kwa kuwashambulia kwa nguvu ama kuwalazimisha waamini watakavyo watu fulani pekee.

"Wale watumiao nguvu za vyombo vya dola katika kukabiliana na wale wanaodai haki zao kamwe huwa hawawezi kuzima madai hayo, Bali japo kwa kupitia maumivu makali Sana huwaandaa Wanyonge hao nao kutumia nguvu inayofanana na hiyo ili kudai haki zao" Ni maneno aliyoyasema Mzee Mandela pale watawala dhalimu wa kikoloni walipoonekana kutokuthamini madai ya haki kwa Waafrika.

Mandela aliamini kuwa wale wanaopuuza madai ya haki na maridhiano ya amani huku wakitumia maguvu na mamlaka waliyipewa na wananchi kukanyaga katiba ndio wachafuzi wa amani kwani kwa kufanya hivyo hulazimisha matumizi ya nguvu na mapambano yasiepukike.

Naye Mwanaharakati wa zamani wa Taifa la Uchina, Mao Tse Dung aliamini kuwa silaha humaliza mgogoro unaotumia silaha.

"Vita humalizwa na Vita, Vita ya bunduki humalizwa kwa bunduki" Ni moja ya kauli alizowahi kuzitoa Mara kadhaa katika hatakati zake za kijamii na kisiasa huko Uchina.

Falsafa hii nayo inatujuza kuwa kumbe ili amani, utu, upendo na mshikamano vidumu katika jamii, masuala yenye utata na migogoro yahusianayo na jamii hiyo Ni sharti yatatuliwe kwa njia za amani na maridhiano na si ubabe huku makundi mengine yakipuuzwa ama kushambuliwa kwa silaha za Moto.

"Utii wa uoga ndio msingi mkubwa uletao mateso na manyanyaso" Ni maneno aliyowahi kuyanena Mwanafasihi Maarufu wa Uingireza, Shake Spear kupitia moja ya kazi zake za fasihi.

Shake Spear anatufunda kuwa watu wakiwa katika utii uliojengwa katika unafiki na uoga ndio huweza kufanyiwa lolote, kupuuzwa, kuonewa na kuumizwa kwa namna mbalimbali na wale wenye maguvu, Bali jamii ikijitambua na ikasimama katika kudia haki kwa mujibu wa Sheria zilizopo hata wale wenye maguvu huishi sawasawa na Wanyonge.

Mwana wa Lufunga nasisitiza, tunaitana Wanyonge na wenye nguvu kwakuwa Kuna ukiukwaji wa Sheria na aidha Sheria zetu Ni mbivu kiasi kwamba ndizo zinakuwa chanzo Cha haya yote, kwa Maana katika jamii yenye kujitambua, hakuna mtu anayo nafasi ya kumpangia mwingine afanye kipi na asifanye kipi na wala haipaswi kuwa na tembo wa kumtisha mwingine Wala sisimizi wa kumnyenyekea mwingine. Uwepo wa haya katika jamii zetu Ni ithibitisho wa ukiukwaji wa haki za binadamu na aidha kwa uwepo wa katiba mbovu zisizoendana na wakati na mustakhabali wa jamii halisi.

Katika jamii mbalimbali, watu makini wenye akili sawasawa na uzalendo wa dhati wameteseka tangu enzi na hata Zama, historia inafichua. Haya yote yanatokea tu ikiwa wenye nguvu wanaelekea kuunga mkono maovu ya ukanyagaji wa katiba, matumizi ya nguvu kushinikiza matakwa ya wenye mamlaka na vitisho kwa wanaodai haki.

Historia inaonesha waafrika wengi zaidi wenye akili timamu walionja maisha ya jehanam wakati wa utawala wa wakoloni ikiwemo magereza, vipigo, mateso, kupuuzwa, kupangiwa maisha yao, kumiminiwa risasi na hata kunyongwa Hadi kufa.

Vitendo vya majeshi ya polisi kutumia vitisho na kauli Tata kwa wananchi wanapodai haki zao, kukamata viongozi wa kisiasa wanaokosoa serikali na kuwatia misukosuko Siku zote huleta sura mbaya katika mchakato wa kisiasa katika Taifa na hii huchafua sura ya nchi katika masuala ya utawala bora, Demokrasia na amani ya nchi husika.

Amani Ni tunda la haki na haki huinua Taifa, Ni vema mamlaka zote zikajua na kuishi katika falsafa hii kwa kuiona amani kama bidhaa adimu inayopaswa kulindwa kwa wivu mkubwa Sana

Na mbinu pekee za kuilinda amani ya nchi Ni maridhiano mema ya makundi yote ya kijamii, kuimarisha utawala wa haki, kuweka Sheria nzuri na kuzitii viongozi kuheshimu haki za watu na kuongoza kwa matakwa ya watu kuliko kushinikiza watu watii matakwa ya wachache waliopo madarakani.

Inasikitisha Sana pale wachache waliopo madarakani wanapotaka kulazimisha maamuzi yao pekee ndiyo yaonekana ya watu makini na kwamba anayewaza tofauti nao Basi Hana akili, hii si sawasawa kabisa kwani hufanya viongozi kujiona Miungu watu, huanza kudharau na kupuuzapuuza watu, kuonea watu na kufanya maamzi ya hovyo na kutumia polisi na magereza kuyashinikiza.

0689990248.
 
Upvote 1
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…