SoC02 Wakati wako ndio leo!

Stories of Change - 2022 Competition
Joined
Sep 6, 2022
Posts
3
Reaction score
2
Mwanangu, tazama mzazi wako nimeshakuwa mzee, umri umenitupa mkono. Meno yangu yote yamebongonyoka, siwezi hata kutafuna mnofu. Nguvu za mwili nazo zimeniisha, siwezi tena kusimama na kutembea vizuri kama kipindi cha ujana wangu. Ubaya, nimekuwa mzee masikini, uzee wangu umekuwa wa majuto na kutaabika sababu ya makosa niliyofanya pindi nilipokuwa kijana mdogo.

Natamani kurudisha masaa nyuma, ila, ndo hivo tena muda huwa haurudi nyuma. Natamani niingie tumboni mwa mama yangu nizaliwe upya lakini nimechunguza na kugundua huwa haiwezekani. Nayoyatamani kama yangewezekana, basi, wakati ambapo ningerejeshewa upya nguvu za mwili wangu na kuwa kijana, ningejitahidi kurekebisha makosa niliyoyafanya nyuma ambayo yamefanya uzee wangu uwe wa majuto na kutaabika.

Kuna vitu nimewiwa kukueleza sababu sitaki nawe ukizeeka utaabike. Tambua wewe bado ni kijana mdogo, na huo ndio mtaji mkubwa unaopaswa kujivunia. Ujana ulionao ukichanganya na nguvu, akili, maono na imani ambayo mwenyezi Mungu amekubarikia unaweza jenga kesho yako yenye kuvutia na kuacha historia pindi utakapoondoka duniani.

Jambo muhimu unalopaswa kujiuliza leo ni hili: “Mimi ni nani???” Najua jina lako unalitambua vyema, nalo huna haja kulitaja hapa. Nachotaka ujibu ni hivi: “Mimi ni … .” Unaweza jaza nafasi wazi kwa kazi yoyote unayoipenda, kama vile mwanasiasa, mkulima, mfanyabiashara, msanii na mwanamitindo, daktari, mwalimu, n.k. Kama bado hujajijua, basi, angalia kitu unachopenda kufanya sana ukiwa peke yako; usipokijua hata hicho basi naomba uwaulize watu wako wa karibu, wanaokujua vizuri, kuwa wewe unafaa kuwa nani.

Ukishajua hili, kamwe usiichezee bahati yako. Cha kufanya; ongeza imani, bidii, utulivu na uvumilivu sababu Nia huvuta Mambo! Kamwe usigeuke nyuma kusikiliza marafiki, wazazi, ndugu au walimwengu wanasemaje? Kumbuka wewe ndiye mbeba maono, na, si kila mtu anaweza ielewa safari inayoelekea kwenye hatima ya maisha yako, saa nyingine ni wewe tu unaweza kuwa unaiona. Hivyo, daima nenda mbele usigeuke nyuma.

Wakati ukipambana kutimiza maono yako, usiogope changamoto pamoja na watu watakaokukatisha tamaa; jivike moyo wa ujasiri sababu hakuna changamoto na kelele zinazodumu milele. Ukiweza kutuliza akili yako kumaliza changamoto utakazokumbana nazo na si kuzikimbia, amini kesho au keshokutwa yako itakuwa ya kuvutia zaidi na nakuahidi kuwa utasahau changamoto zote ulizopitia. Mwanzo ni mgumu siku zote, hivyo, pambana kwa kila namna uende mbele na si kurudi nyuma.

Daima usimwache elimu katika safari inayoelekea kutimiza maono yako. Elimu atafanyika kama upepo kwenye gurudumu la gari ili ufike bila kuyumbishwa-yumbishwa ovyo. Nakumbuka mzazi wako nilimdharau sana elimu kwa kuamini pesa ni muhimu zaidi. Kwa kukosa elimu, mambo yangu mengi niliyafanya kwa pupa nisitake kuyajua vizuri. Baadhi ya mambo yaliponiendea kombo nilijutia ujinga wangu, niliwalaani hata marafiki walionishauri niachane na shule nikatafute pesa mtaani.

Kama utachagua kuwa mwanasiasa, niwe na ombi moja kwako. Siku ukipewa nafasi hii naomba usiichezee. Ni muhimu ukatambua nchi yetu ni maskini licha ya kuwa tumebarikiwa rasilimali nyingi kama madini ya thamani, ardhi yenye rutuba, vivutio vya watalii, misitu, vyanzo vya maji, samaki, pamoja na rasilimali watu.

Macho yangu yameona kuwepo kwa rushwa katika sekta nyingi za umma, ubadhilifu, bajeti mbovu, teknolojia duni, pamoja na ukoloni mamboleo ndio kikwazo kikubwa tusiendelee. Hivi vyote kavipige vita vikali, sababu, umaskini huu tuliojitakia umesababisha kwenye shule nyingi za umma kuwe na miundombinu chakavu pamoja na vitabu vichache, huduma za afya mbovu, uhaba wa maji safi na salama, miundombinu ya usafiri mibovu, viwanda duni, umeme usio wa uhakika pamoja na uhaba wa umeme katika maeneo mengi ya vijijini. Matatizo haya yote ukiwa na moyo wa kuipenda kweli nchi yetu pamoja na nidhamu ya ufuatiliaji unaweza kuyamaliza.

Endapo utachagua kuwa mkulima, niwe na ombi moja pia. Ombi langu kwako ni kwamba: Nenda kafanye kilimo chenye tija na cha kiushindani zaidi ili kujipatia maendeleo mazuri yanayoweza kukutoa kwenye hali ya umaskini uliyonayo sasa na kuwa tajiri. Unaweza kulima mazao mbalimbali ya nafaka, mbogamboga, matunda, vitunguu na viungo vingine na hata kufuga wanyama na ndege.

Tambua tunayo ardhi ya kutosha yenye rutuba lakini wakulima wetu bado ni maskini wa kutupwa. Kilimo chetu bado ni cha kutegemea sana jembe la mkono na mvua isiyotabirika. Nakutuma ukalete mapinduzi; nenda kafanye kilimo cha umwagiliaji ili ulime kipindi chote cha mwaka, tumia plau au trekta na mashine nyingine ili ulime eneo kubwa. Pia zingatia mbegu na mbolea utakazopanda na kutia shambani; vyote viwe bora ili ujipatie mavuno ya uhakika. Kabla ya kipindi cha mavuno hakikisha umetafuta soko zuri na la uhakika kwa ajili ya kuuza mazao.

Kama utachagua kuwa mfanyabiashara, naomba ujitahidi kupambanua fursa. Kamwe usichezee fursa yoyote itakayojitokeza mbele yako na hakikisha unakuwa na nidhamu ya ufuatiliaji mpaka utakapoona matunda yake. Mbele yako zipo fursa nyingi sana ambazo zinaweza kukupatia fedha na kutanua uchumi wako ili uwekeze katika miradi mingine. Acha kuwaza juu ya kupata mtaji mkubwa ili ufanye biashara kubwa; unachotakiwa kufanya ni kuamua kufanya hata kile kidogo kinachoweza kukupatia fedha kidogo kisha utumie fedha kidogo utakayopata kufanya kitu kingine chenye kukuingizia pesa zaidi ili kesho uweze kufikia uwezo wa kuwekeza katika miradi mikubwa.

Wakati unaanzisha biashara hakikisha umeyajua mazingira ya kufanyia biashara yako na kujua nini watu wanahitaji kukipata na kupendelea, kwa wakati gani na kwa thamani gani. Ukishajua hilo, wewe kama mbeba maono inakupasa uamue kuanzisha biashara hiyo na kutafuta kila njia kuhakikisha unaweza kukabiri changamoto mbalimbali za biashara yako na kuona inakua zaidi. Katika biashara yoyote, watu kwako ni mtaji wa kwanza hivyo hakikisha unajenga mahusiano mazuri na kila mtu unayekutana naye. Usiogope na kutishwa na wale walioshindwa, sababu, wewe ni wa kipekee na wakati wako wa kufanikiwa na kutimiza maono yako bado haujafika.

Endapo pia kama utapenda kuwa msanii na mwanamitindo ili uwaburudishe na kuwanogesha watu kwa lengo la kujipatia pesa, hakikisha unajituma na kufanya kazi zako kwa ubunifu mkubwa. Tambua watu wengi wapo kwenye sekta ya burudani, hivyo hakikisha kazi zako zinakuwa za kitofauti na kiufundi zaidi ili upate kuaminika kwa watu.

Kwa kazi nyingine yoyote ikiwa ni pamoja na walimu, udaktari na Kadhalika; tafuta kujua nini unakihitaji ili ufanikiwe na namna ya kukabiliana na changamoto zake. Ni matumaini yangu nuru ya mafanikio nimekwisha iangaza. Yote yanawezekana ukiamini! Nguvu unazo! Uwezo unao! Wakati wako ndio leo, usingoje kesho! Nikutakie tafakari na siku njema, kwaheri!

Imeandikwa na Romward Johnny
Mawasiliano: 0716541844
Chanzo cha picha: iStockphoto

 
Upvote 6
Umetisha mkuu
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…