Wakatoliki Tujifunze: Baadhi ya mavazi ya Askofu na maana yake

Wakatoliki Tujifunze: Baadhi ya mavazi ya Askofu na maana yake

Alfred

JF-Expert Member
Joined
Apr 13, 2008
Posts
2,093
Reaction score
2,843
Tumsifu Yesu Kristu!
Tumekuwa tukiwaona MaAskofu wetu wakiwa ndani ya Baadhi ya Mavazi ambayo mara Pengine wengine Hatuyafahamu, Basi Haya na Ndiyo Maelezo ya kila Vazi!


1. Pete ya Askofu (Episcopal ring)

1535550385265.png

Hii huvaliwa na Askofu katika “kidole cha pete cha mkono wa kulia” (kidole cha pili kutoka kushoto). Mtume Paulo katika waraka wake kwa Waefeso anatumia lugha ya picha kutoa ujumbe kwa wanandoa akisema “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa…” (Efe. 5:25). Hapa Mtume Paulo anamtazama Kristo kama mume wa Kanisa (Kanisa ni mke na Kristo ni mume). Lugha hii ya picha inaonesha aina fulani ya “muungano wa ndoa” uliopo kati ya Kristo na Kanisa lake kama ilivyo kwa mume na mke. Askofu anamwakilisha Kristo mbaye ni kuhani mkuu. Hivyo kama ambavyo Kristo kuhani mkuu “ameoana/funga ndoa” na Kanisa lake, kadhalika Askofu naye anavikwa pete kuonesha kuwa “amefunga ndoa na Kanisa lake”- ameunganishwa na Kanisa analolitumikia- yaani waamini wake/Jimbo lake). Kama ambavyo pete ni ishara ya uaminifu na mapendo, kadhalika Askofu naye anapaswa kulitumikia kanisa lake/waamini wake/Jimbo lake kwa uaminifu na mapendo.
Kwa nini tunabusu pete ya Askofu? Kitendo cha kubusu pete ya Askofu ni ishara ya kutambua na kuheshimu mamlaka yake ya kuongoza, kufundisha na kutakatifuza.


2. Msalaba wa kifuani (pectoral cross)
1535550366097.png

Msalaba huu humkumbusha Askofu mateso na msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo katika safari nzima ya ukombozi. Msalaba auvaao Askofu humkumbusha Askofu kuwa naye katika kutimiza wajibu wake wa kichungaji atakumbana na mateso na misalaba mingi ambayo atapaswa kuiibeba kwa moyo mkuu- hii ndiyo sababu ya msalaba huo kuvaliwa kifuani (wengi tunaamini moyo hukaa kifuani). Msalaba wa kiaskofu hufungwa ama kwa kamba au mkufu.

3. Fimbo ya kichungaji (Pastoral Staff/ Crosier)

1535550350377.png

Katika jamii ya wafugaji, wachungaji hubeba fimbo wanapokwenda kuchunga mifugo yao. Fimbo hiyo hutumika kuongozea kundi lake la mifugo na hutumika pia kama silaha ya kulilinda kundi la mifugo dhidi ya hatari zozote zitakazojitokeza. Kadhalika fimbo ya Askofu ni ishara ya mamlaka yake ya kichungaji na kiutawala: inaonesha kuwa Askofu amekabidhiwa kundi la kulichunga, kuliongoza na kulitawala. Kundi hilo ni waamini. Hivyo, fimbo ya kichungaji inaashiria kuwa Askofu anao wajibu wa kuwaongoza waamini wake na kuwalinda dhidi ya hatari zozote
za kiimani. Kisheria Askofu anayebeba fimbo ya kichungaji ni Askofu-Jimbo akiwa ndani ya Jimbo lake. Hata hivyo, Askofu asiye wa Jimbo husika anaweza kubeba fimbo ya kichungaji kwa ruhusa ya Askofu-Jimbo wa Jimbo husika. Maaskofu Wastaafu hawabebi fimbo ya kichungaji.


4. Mitra (Miter)

1535550332861.png

Hii ni kofia kubwa ya pembe tatu ambayo kwa nyuma ina tepe mbili. Kufafanua zaidi juu ya maana ya maumbo ya kofia hii tunahitaji muda mwingi. Itoshe kusema tu kwamba Mitra inaashiria “taji ya ushindi” endapo tutashinda mapambano ya Kikristo. Mtume Paulo anasema wazi: “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake” (2 Tim. 4:7-8). Hivyo, Mitra inamkumbusha Askofu kuwa anapaswa kuliongoza kundi lake katika mashindano ya mbio za hapa duniani kuelekea wokovu hadi tufikie ushindi wa mwisho mbinguni ambapo tutapewa taji ya ushindi inayoashiriwa na Mitra.

5. Zucchetto (kofia ndogo ama nyeupe, au nyekundu au zambarau)
1535550317534.png

Mwanzoni, zucchetto haikuwa sehemu ya mavazi ya liturujia. Miongoni mwa hatua za kuelekea upadre ilikuwa ni kunyolewa kipara cha utosini. Hatua hii iliitwa “tonsure”. Kutokana na baridi kali la nchi za ulaya, ililazimika kuvaa kofia ndogo eneo la kipara ili angalau kupata joto. Kofia hiyo ya kuhifadhi joto kwenye kipara cha utosini ndiyo iliitwa “zucchetto.” Kadiri miaka ilivyopita, zucchetto ikawa vazi la liturujia/ibada. Zucchetto ya rangi nyeupe huvaliwa na Baba Mtakatifu; Zucchetto ya rangi nyekundu huvaliwa na Makardinali na Zucchetto ya rangi ya zambarau huvaliwa na Maaskofu. Vyanzo mbalimbali huonesha kuwa zucchetto ni ishara ya Roho Mtakatifu kama vile Roho Mtakatifu alivyowashukia mitume kama ndimi za moto siku ya Pentekoste (rejea Mdo. 2:1-4). Hivyo, zucchetto huashiria nguvu na mapaji ya Roho Mtakatifu. Kwa kawaida Maaskofu huvua zucchetto zao wawapo mbele ya Baba Mtakatifu ikiwa ni ishara ya heshima na kutambua mamlaka na cheo cha Baba Mtakatifu.

6. Pallium
1535550284256.png

Hili ni vazi ambalo huvaliwa na Baba Mtakatifu, Maaskofu Wakuu na Patriaki wa Yerusalem tu. Ieleweke wazi kuwa siyo kila Askofu Mkuu huvaa Pallium. La hasha! Huvaliwa tu na Maaskofu Wakuu ambao ni Maaskofu-Jimbo (yaani wana majimbo wanayoyaongoza). Hata hivyo, huvaliwa tu na Askofu Mkuu awapo ndani ya majimbo yanayounda Jimbo Kuu lake. Mfano Jimbo Kuu la Mwanza linaundwa na majimbo ya Mwanza, Musoma, Shinyanga, Bunda, Geita, Kayanga, Bukoba na Rulenge-Ngara. Hivyo Askofu Mkuu wa Mwanza anaweza kuvaa Pallium awapo kwenye mojawapo ya majimbo hayo. Akienda Jimbo la Tanga, kwa mfano, hawezi kuvaa Pallium kwa sababu ni nje ya metropolitan yake (nje ya mipaka ya Jimbo Kuu la Mwanza).
Pallium hutokana na sufu (manyoya ya kondoo) yaliyokatwa kutoka kwa kondoo wakati wa sherehe ya Mt. Anyesi ambayo huadhimishwa Januari 21 kila mwaka. Jina Anyesi (au Agnes) limetokana na neno la Kilatin “Agnus” lenye maana ya “Mwanakondoo”. Kwa nini hutengenezwa kutokana na sufu ya kondoo? Kwenye Agano Jipya Kristo anatambulishwa kama “Mwanakondoo wa Mungu” (rejea Yn. 1:29, 36). Kama ambavyo kondoo wanatoa sufu kwa ajili ya kutengeneza Pallium, hivyo hivyo Kristo aliye “mwanakondoo wa Mungu” anajitoa sadaka kwa ajili ya dhambi za ulimwengu. Kadhalika, kitendo cha kuvaa shingoni Pallium iliyotengenezwa kutokana na sufu ya kondoo kinaonesha kuwa Askofu ni Mchungaji Mwema kwani amewabeba kondoo zake (waamini) mabegani. Pallium inapovaliwa shingoni mwa Askofu inamaanisha pia “nira ya Kristo” kwani Kristo alisema “Jitieni nira yangu… Kwa maana nira yangu ni laini…” (Mt. 11:29, 30). Pallium zikishatengenezwa huweka chini ya altare ya Basilica la Mt. Petro karibu kabisa na kaburi la Mtume Petro. Kila tarehe 29 June ambayo ni Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, Maaskofu Wakuu wapya walioteuliwa mwaka huo huenda Roma na kupatiwa Pallium hizo kama zawadi maalumu kutoka kwa Baba Mtakatifu. Kwa nini Pallium huwekwa karibu na kaburi la Mtume Petro? Na kwa nini Papa pekee ndiye huwapatia Pallium Maaskofu Wakuu? Hii ni kuonesha kuwa Maaskofu Wakuu wanapaswa kuwa na ushirika wa kipekee kabisa na Baba Mtakatifu ambaye ni halifa wa Mtume Petro. Wanapaswa kuonesha muungano na utii kwa Baba Mtakatifu ambaye ni halifa wa Mtume Petro. Pallium ni nyeupe ili kuonesha kuwa Askofu husika anapaswa kuwa na usafi wa maisha (innocence of life).

Maelezo Haya ni Kwa Mujibu wa Padre Kelvin Onesmo Mkama, Jimbo Kuu la Mwanza (Mimi Nimeyaandika tu)

ALFRED
 
Kilemba cha Sister kina umuhimu gani

don't invest in a woman
 
Back
Top Bottom