Wakili anayemtetea Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni ya Uchaguzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Pambalu, Hekima Mwasipu amekanusha madai yaliyotolewa na Mjumbe wa Baraza Kuu la CHADEMA kupitia Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), Hilda Newton kwamba kurejea kwa mteja wake nchini na kutoa maelezo kwa Jeshi la Polisi kunahusiana na madai ya kutekwa kwa mwanaharakati na mwanachama wa chama hicho, Twaha Mwaipaya, jijini Nairobi nchini Kenya.
Sintofahamu hiyo imeibuka katikati ya madai ya kutekwa kwa Twaha Mwaipaya nchini Kenya na kushikiliwa kwa Pambalu nchini Tanzania kufuatia kufunguliwa kwa mashtaka ya uhaini yanayohusiana na matukio ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Mnamo Novemba 1, 2026, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Hilda Newton alichapisha maelezo akimshutumu Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Godbless Lema, kwa kumshawishi Pambalu kurejea nchini Tanzania na kutoa ushirikiano kamili kwa Jeshi la Polisi. Katika chapisho hilo, Hilda alidai kuwa Lema alimhakikishia Pambalu usalama wake akisema alizungumza na afisa wa polisi na kwamba kila kitu kilikuwa sawa, jambo lililompa Pambalu ujasiri wa kurejea nchini.
“Pambalu kwa maelekezo yake wakati anazungumza na watu walioenda kumuona gerezani hivi karibuni anasema, wakati polisi wanamhoji alizungumza ukweli wake wote ambao anaujua kuhusu watu waliopo Nairobi. Siku kadhaa baada ya Pambalu kusema ukweli wake wote, Twaha Mwaipaya akatekwa na watu wasiojulikana mpaka leo imetimia siku nane hatujui Twaha yupo wapi”, aliandika Hilda katika sehemu ya chapisho lake.
Kufuatia chapisho la Hilda, Wakili Mwasipu alijibu kupitia mitandao yake ya kijamii ili kuweka wazi masuala yote ambayo mteja wake alihojiwa mbele yake wakati akiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi.
Wakili Mwasipu alitaja mambo ambayo Pambalu alihojiwa mbele yake ikiwamo majukumu aliyopangiwa na Kamati Kuu ya CHADEMA katika Hoteli za Desderia na Bagamoyo, kama alihusika kuandaa filamu ya kumbukumbu ya mauaji ya tarehe 29 Oktoba 2025 kabla akiwa na John Kitoka, uhusika wake na Dkt. Slaa na Mchungaji Mwamakula kwenda nchini Uganda na Kenya kuhamasisha maandaman