Mphamvu
JF-Expert Member
- Jan 28, 2011
- 10,702
- 3,319
Algeria 7 - 0 Tanzania, hivyo ndivyo ulivyosomeka ubao wa matangazo uwanjani Blida, baada ya mechi ya marudiano ya Kufuzu Kombe la Dunia 2018 kuisha Ok. 17 mwaka huu.
Tukubaliane jambo moja, kila mtu ambaye ni mdau wa timu ya Taifa ya soka, kwa namna yake alidhalilika na kipigo kile cha kihistoria, ambacho wetu hatujawahi kushuhudia kwenye maisha yetu yote.
Baada ya mechi ya kwanza nilipanga kuja na makala ya kuwalaumu washabiki ambao tulikuwa nao Uwanja wa Taifa kwenye sare ya 2-2.
Baada ya Stars kuwa mbele kwa goli mbili, walishangilia kwa mizuka yote, ila wakati Slimani Islam anarejesha goli la pili, kundi la kutosha la washabiki lilianza kutoka nje ya uwanja, wakiashiria kuwa kuendelea kuwatazama Stars ni kupoteza muda.
Bila kumung'unya maneno, washabiki kama hawa ni kikwazo kikubwa kwa timu, kwani timu huwa inahitaji 'kuungwa mkono' tu kutoka kwa hawa watu.
Tupo kwenye zama za fedha fedha, washabiki hawatakiwi tena kujitoa kwa 'hali' na 'mali', kwani mamlaka zinazohusika zilishamaliza suala la 'mali', kwa maana ya usaidizi wa kifedha kwa timu ya taifa.
Sapoti ya mashabiki wakati mgumu, timu inapokuwa imezidiwa kiufundi si jambo doo, ndio maana kuamriwa kucheza bila mashabiki ni adhabu kubwa sana kwenye ligi ambazo wamerasimishiwa mfumo wao wa viwanja na washabiki.
Sasa turejee kwenye kisanga cha fedheha ya 7 - 0, ambapo mara tu baada ya hapo kila mtu aligeuka mkosoaji, mtaalamu, mshauri na mbobezi wa kila kitu kwenye soka, kuanzia ufundi, utawala na uwekezaji kwenye soka la vijana.
Sifa ya kwanza ya kuwa mkosoaji mzuri ni kutambua juhudi na hatua ambazo tayari zilishafanyika. Ajabu wakosoaji wetu walishauri tuwe na soka la vijana, wakasahau kuwa Thomas Ulimwengu wanayejigamba nae ni zao la shule ya TSA iliyokuwa inaendeshwa kwa ubia kati ya TFF na Bolton Wanderers FC ya Uingereza.
Wakosoaji wetu wakasahau kuwa mwaka huu pekee, nchi ilipata Shule mbili za Soka la Watoto na Vijana, ile ya NSSF/Real Madrid na Kituo cha Soka cha Kidongo chekundu, miradi ya kisasa kabisa inayosimamiwa kitaalamu, kwa sasa.
Kundi lingine la wakosoaji likadai kuwa na ligi imara, na kukomesha ubabe wa Simba na Yanga. Nadhani washabiki wetu wanatumia mfumo wa kumbukumbu uliopitwa na wakati kwani hawaoni kuwa sasa hivi Ligi zetu za ndani zina makampuni kadhaa yanayodhamini, jambo ambalo miaka kadhaa nyuma halikuwepo.
Mgawanyo wa fedha na uwekezaji kwenye vilabu si wa kukatisha tamaa sana, timu kadhaa leo hii zina wadhamini binafsi, mipango ya maendeleo na vilabu kama Azam na Mwadui vina viwanja vya kisasa vya mechi na mazoezi, haya ni mambo ya kubeza?
Wakosoaji wetu wameshindwa, au wamejifanya hawaoni juhudi ambazo TFF, vilabu, Wizara ya Michezo, makampuni binafsi na watu mmoja mmoja wamefanya kwa ajili ya kusogeza soka letu mbele, na bila unafiki tunaona limesogea.
Hawa ni aina ya watu ambao ukifanikiwa wanajigamba pamoja na wewe, ila ukipoteza wanakumbusha kuwa ulishaitwa Kichwa cha Mwendawazimu na mwanasiasa mkongwe ambae sidhani kama amewahi kucheza soka.
Watu hawa hatuwahitaji, sio wao wala ushauri wao kwani wanaonekana hawajui matatizo ya timu zetu, hawajui juhudi ambazo tumefanya, hawapo kwa ajili ya kutupa moyo na hawatusaidii lolote.
Makundi ya hawa watu yanataka kushauri mambo ya kitaifa yanayohusu Soka, huku wakiwa hawajawahi kushauri hata timu za mtaani kwao.
Yupo mchambuzi mmoja mahiri ambaye aliongoza safu ya kukosoa na kumponda mwalimu wa timu tangu mechi ya kwanza, na bahati ameshiriki matukio mengi ya mpira ya kimataifa. Waja wakahoji, kwenye ziara zake za Ulaya na kwingineko, alishawahi kumuunganisha mbongo mwenzake hata mmoja?
Nikomee hapa, nikisisitiza tuwajue wapiga kelele wetu, wanaodhani wanafahamu suluhu ya matatizo yetu, huku wakishindwa kuwa msaada wowote, hata wa makelele tu.
Makala iliyohaririwa imechapishwa kwenye Mwananchi la 23 Novemba 2015.