SoC04 Walimu wapewe posho ya katikati ya mwezi shilingi laki moja kuwapa motisha na kuwapunguzia ugumu wa maisha

SoC04 Walimu wapewe posho ya katikati ya mwezi shilingi laki moja kuwapa motisha na kuwapunguzia ugumu wa maisha

Tanzania Tuitakayo competition threads

Xpertz

Member
Joined
May 3, 2024
Posts
13
Reaction score
10
UTANGULIZI

Kwa miaka mingi toka nchi ipate uhuru walimu wamekua ndio kiwanda cha kuzalisha maarifa kwa ajili ya uendeshaji wa nchi kwa kuwatoa watu ujinga na kuzalisha Wataalamu ila maslahi yao yameachwa nyuma, hawana motisha. Mfumuko wa bei kwa miaka mingi umeendelea kuwa sio rafiki kulinganisha na viwango vya mishahara yao na kuwalazimu kuwa wahanga wakuu wa mikopo umiza maarufu kama KAUSHA DAMU. Walimu wengine wengi hususani maeneo ya mijini wamejikuta wakijiingiza kwenye ajira za ziada zisizo rafiki kwa taaluma zao ikiwemo uendeshaji wa bodaboda ili tu kujiongezea kipato kuweza kujikimu kulingana na gharama kubwa za maisha na kipato chao kidogo.

Kundi hili la walimu ni nyeti sana kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla katika nyanja zote, hivyo kuendelea kulipuuza ni kutishia mustakabali mpana wa maendeleo ya taifa letu, hawana motisha ya kazi mshahara wanaopewa hautoshi kulingana na gharama halisi za maisha kwa sasa HUO NDIO UKWELI MCHUNGU.

Walimu wengi wanaishi maisha ya unyonge, hawana la kujivunia kwenye kazi yao maana ajira yao ilipaswa kichangia maendeleo ya maisha yao ila imebaki kuwa ajira ambayo kipato chake hata kujikimu hakitoshi kutokana na kutofanyiwa mabadiliko kuendana na gharama za Mfumuko wa bei nchini kwa miaka mingi mfululizo.

Nini kifanyike kuokoa kundi hili nyeti kwenye nchi yetu?

Nashauri kama ilivyofanyika kwa vyombo vya ulinzi na usalama ambao wanapokea 300,000/= kama posho ya katikati ya mwezi, madaktari ambao mishahara yao imeboreshwa kuendana na gharama za maisha, WALIMU NAO WAKUMBUKWE. Kwa wingi wao, hata kama kuwaongezea mishahara kwa ujumla wao inakua ngumu kibajeti nashauri angalau wapewe shilingi laki moja(100,000/=) katikati ya mwezi kama posho ili kuwapunguzia ukali wa maisha. Hii itasaidia kuwapunguzia ugumu wa maisha na maumivu dhidi ya mikopo umiza na kausha damu wanayolazimika kuchukua kwa sasa ili kutatua changamoto zao ndogo ndogo za kifedha kutokana na mshahara kuwa kidogo usioendana na gharama za maisha.

Posho ya katikati ya mwezi itasaidia mno kuwapa morali na motisha ya kazi yao, itaondoa msongo wa mawazo na kuimarisha utendaji wao ambao matokeo yake watoto wetu watapata elimu bora zaidi na kuunda taifa lililostaarabika na lenye maarifa ya kutosha.

Kitendo cha kuendelea kuwapuuza walimu ni kuchezea Sekta nyeti kwa mustakabali wa taifa letu kulingana na maendeleo ya sayansi na teknolojia na UTANDAWAZI ambapo kwa sasa elimu inahitajika kwa UFANISI mkubwa kuliko wakati wowote katika historia ya nchi na dunia.

Dunia inaenda kasi sana, tunapaswa kujenga taifa kwa kuhakikisha maeneo ya vipaumbele tunayapa umuhimu wake ili kuongeza tija.

Walimu ndio waasisi wa maarifa na maadili kwa Wataalamu wa kada zote ikiwemo viongozi, wanasiasa, madaktari, mainjinia nk ila cha kusikitisha hao wote wana maslahi bora kuliko walimu. Walimu wamekua kama magreda(mitambo ya kuchimbia barabara) wanachimba barabara ila wao hawaruhusiwi kuitumia. Wanazalisha Wataalamu nyeti wanaopata maslahi bora ya kazi zao ila walimu wao maslahi ni hafifu hayakidhi hata mahitaji yao.

Ugumu wa maisha kwa Walimu kutokana na kipato hafifu umepelekea baadhi ya walimu kupata matatizo ya afya ya akili kwa kuingia mikopo umiza /nyonya damu ambayo imekua ikiwaumiza mno matokeo yake ufundishaji wao umeporomoka wengine wamefikia kutoa adhabu kali kwa wanafunzi mashuleni na hata kupelekea vifo kwa watoto. Matukio hayo yamekua yakiripotiwa mara kwa mara nchini ila tumeendelea kupuuza kuangalia chanzo ambacho ni KIPATO HAFIFU.

Sambamba na posho ya katikati ya mwezi ya shilingi laki moja nashauri pia walimu wapewe pikipiki kama wanavyopewa Maafisa kilimo na pikipiki hizo baada ya miaka miwili ziwe zao ili kuwaongezea motisha ya kazi.

Ualimu ni kazi inayohitaji unadhifu, katika bajeti ya wizara ya elimu nashauri pia kuwe na fungu la sare kwa ajili ya walimu kama ilivyo kwa manesi ili kuongeza tija. Walimu wawe na sare maalumu kuchochea maadili mashuleni ambapo kwa sasa kuna baadhi ya walimu wanavaa kinyume na maadili. Sare hizo walipiwe na Serikali kila mwaka wa bajeti ili kuongeza tija kwenye suala la maadili mashuleni na uvaaji kwa ujumla.

Serikali iangalie uwezekano wa kutumia miundombinu ya baadhi ya shule za kimkakati kibiashara kuongeza mapato ya Ziada yatakayosaidia kufanikisha uboreshaji wa maslahi ya walimu. Kwa mfano shule zilizoko mijini zina kuta za uzio, kuta hizo zijengwe fremu za biashara wafanyabiashara wakodishwe na kulipia kodi kwa mfano shule ya sekondari Uhuru iliyopo manispaa ya Shinyanga, pia kuna shule zina mashamba makubwa ziajiri Wataalamu wasimamizi kufanyike miradi yenye tija kubwa ya uzalishaji pia yatumike kufundishia UJASIRIAMALI wanafunzi wetu.

ELIMU BORA BILA MASLAHI BORA YA WALIMU HAIWEZEKANI,

MASLAHI BORA YA WALIMU NDIO MSINGI WA ELIMU BORA NCHINI.

NAWASILISHA
 
Upvote 1
Back
Top Bottom