Hits: 497
SERIKALI imesema ajira za walimu wapya
zitaanza rasmi Mei Mosi, mwaka huu huku
ikiweka wazi kuwa walimu hao wasitegemee
kupangiwa katika maeneo ya majiji,
manispaa na miji.
Walimu hao wametakiwa kutotegemea
kupangiwa katika maeneo hayo kutokana na
idadi ya walimu waliopo ni kubwa na inakidhi
mahitaji, huku maeneo yaliyopewa
kipaumbele ni vijijini na halmashauri ambazo
zina mahitaji na upungufu mkubwa wa
walimu.
Idadi ya walimu wapya watakaoanza ajira
zao mwezi ujao ni 31,056 ambapo kwa
walimu wa ngazi ya Cheti ni 11,795,
Stashahada (Diploma) 6,596 na wenye
Shahada (Degree) 12,665.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
ajira mpya za walimu kwa mwaka
2014/2015.
Alisema kwa mwaka huu ajira hizo
zimechelewa kutokana na TAMISEMI pamoja
na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
kufanya ufuatiliaji wa kina hadi katika ngazi
ya shule ili kubaini kwa uhakika mahitaji
halisi ya walimu kwa kila halmahauri na
shule.
Ufuatiliaji huo umebaini kuwepo kwa
halmashauri na shule hasa za mjini zenye
walimu wa ziada na zingine hasa za vijijini
zina upungufu mkubwa wa walimu, alisema
Sagini.
Alisema taarifa hizo zimesaidia kuwapanga
walimu wapya kwa usawa ili kuondoa
uwiano usioridhisha kwenye maeneo mengi
ya vijijini. Alisema kwa sasa wanakamilisha
taratibu za kupata kibali kwa ajili ya ajira za
walimu na fedha za kuwalipa stahili zao ili
waanze ajira zao rasmi mwezi ujao.
Aidha, alisema orodha ya walimu na vituo
watakavyopangiwa vitawekwa katika tovuti
ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI ambayo
ni
www.pmoralg.com na ya Wizara ya Elimu
www.moe. go.tz ifikapo Aprili 24, mwaka
huu.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa
TAMISEMI, Zuberi Samataba alisema, pia
ufuatiliaji huo ulikuwa ni kuhakikisha
wanakuwa na taarifa sahihi za walimu
wanaoajiri wote ni wapya ambao hawajawahi
kuajiriwa ili kuepuka usumbufu kwa walimu
ambao hawatoi taarifa.
Alisema baadhi ya walimu ambao
wameshaajiriwa wanapoenda kusoma,
hupangiwa upya vituo na hawatoi taarifa
hivyo kuleta usumbufu wa kuchelewa
kutopata mishahara yao.
Kuna baadhi ya walimu wameshaajiriwa
kwa hiyo jina linapoingizwa katika taratibu
za malipo, linagoma kuingia ndipo ukifuatilia
unajua alikuwa ameajiriwa, inabidi
umwambie arudi kwa mwajiri wake.
Kwa hiyo kwa hawa walimu wapya
nawashauri waende kuripoti katika vituo
walivyopangiwa na wakubali kufanya kazi
katika maeneo hayo, sio waripoti halafu
waondoke, alisema.
Wakati huohuo, Serikali imewataka Makatibu
Tawala wa Mikoa ambayo shule zake
zimefungwa kwa madai ya ukosefu wa
chakula, kuwachukulia hatua wakuu wa
shule hizo, kwa kile kilichoelezwa kuwa
wamekiuka utaratibu kutangaza hivyo ilhali
serikali ilishatuma fedha kwa ajili ya chakula
cha wanafunzi katika shule mbalimbali
nchini.
Shule zilizofungwa kwa tatizo hilo na mikoa
yake kwenye mabano ni Rugambwa,
Kahororo, Nyakato na Ihungo (Kagera),
Lyamungo (Kilimanjaro), Mpwapwa na Abeid
Karume (Dodoma), Kazima, Milambo,
Wavulana Tabora na Wasichana Tabora
(Tabora).
Uamuzi huo umetangazwa na Katibu Mkuu
wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne
Sagini aliyesema serikali imeshatoa asilimia
66.7 ambazo ni Sh bilioni 28.1 zilizotengwa
kwa mwaka 2014/2015.
Alisema serikali imetoa fedha hizo katika
kipindi cha mwezi Julai mwaka jana hadi
Machi mwaka huu kwa ajili ya chakula cha
wanafunzi wa shule za sekondari,
zinazomilikiwa na serikali. Sagini alisema
serikali ilitenga Sh bilioni 42.1 kwa mwaka
2014/2015, ambapo kati ya fedha hizo kiasi
kilichobaki ni Sh bilioni 13.9, sawa na
asilimia 33.23 ya fedha zilizotengwa.
Kwa ufupi, serikali haijafunga shule na
wakuu wa shule waliotangaza kufunga shule
hizo chache wamefanya makosa kwa kuwa
hawakuwasiliana na mamlaka husika ili
kupata kibali kama kungekuwa na sababu ya
kufanya hivyo, naamini mamlaka husika
zitawachukulia hatua, alisema Sagini.
Alisema wamiliki wa shule ni Mamlaka za
Serikali za Mitaa, ambazo watendaji wake ni
wakurugenzi na wakuu wa shule ni viongozi
wasimamizi wa shule hizo, hivyo hawana
mamlaka ya kutangaza kufunga shule kwa
sababu yoyote bila kibali cha mwenye shule.
Kwa mujibu wa Sagini, kuna utaratibu wa
kufunga shule ambapo katika kipindi hiki,
shule nyingi zilikuwa zimefungwa kwa
mapumziko mafupi kati ya Machi 28 hadi
Aprili 12, ambapo katika shule hizo
zilizofungwa wanafunzi walilazimika kurudi
makwao kutokana na kutangaziwa na wakuu
wao wa shule.