SoC01 Walimwengu, mwiba wa malimwengu na Afya ya Akili

SoC01 Walimwengu, mwiba wa malimwengu na Afya ya Akili

Stories of Change - 2021 Competition

ally sultan

Member
Joined
Sep 8, 2021
Posts
5
Reaction score
2
inbound1200541546476695373.jpg

Hivi tumewahi kuchukua sekunde zetu chache kutafakari namna watu wanayaishi maisha ya hatari na ya kutisha siku hizi?
Namna watu wanavyouana kinyama kwa sababu ya mapenzi, mali za urithi, kutapeliana na ahadi za hapa na pale?

Tumewahi kufikiri namna malimwengu tunavyoyapa nafasi kubwa kutawala matendo yetu, hisia zetu pamoja na fikra zetu katika Dunia ya sasa?
Hiyo sasa ndiyo maana halisi ya ujenzi au ubomoaji wa afya zetu za akili.

Dunia ya sasa tumezongwa sana na huzuni, hofu, mawazo pamoja na fikra potofu ambazo ni chanzo cha maisha tunayoyapitia kama changamoto za kazi, familia, hali za kiuchumi pamoja na mahusiano.

Waswahili wamethubutu kusema “Chizi si lazima aokote makopo (katika hali ya mzaha)” lakini katu si mzaha, namna ambavyo tunazipa nafasi hali zetu za maisha na changamoto kwa sasa ndizo zinapelekea kuzorotesha afya zetu za akili.

Matendo yanayotokea siku hizi ni kwa sababu tu tuliruhusu hisia, fikra na vitendo vyetu vizidi akili zetu. Tutizame namna jamii inavyoharibika kwa kuongezeka matendo ya ubakaji na ulawiti tena kwa watoto wadogo mno, maadili yanavyomomonyoka tukishuhudia, ugomvi unaopelekea visasi na vifo vya kikatili, kujihusisha katika kazi hatarishi kama kuuza utu na miili yetu pamoja na ujambazi kwa sababu tu ya kukosa kazi kutokana na wimbi kubwa la kukosa ajira nchini kwetu na sababu nyinginezo. Yote haya ni kwa sababu ya kuruhusu fikra hasi zitutawale na sababu nyingi ambazo nitapenda tuzizungumze kama namna ya kupunguza ama kumaliza tatizo hili.

Yote yanayotokea ni kwa sababu ya hofu zetu kusema yanayoendelea mioyoni mwetu kwa kuhofia aibu na fedheha, unyanyapaa na visa vya hapa na pale, kutokushirika jamii zetu wala kujichanganya na jamii zetu, milo dhaifu, mazoezi duni pamoja na elimu finyu juu ya umuhimu wa saikolojia na afya ya akili kwa jamii.

Haya yote ndiyo yanayochangia wimbi la mauaji na kujiua kuongezeka, ubakaji, ulawiti, dhulma, wizi na ujambazi, ugaidi, unyanyapaa ambayo yote yanachangiwa na sababu ndogo ndogo zinazoweza kuzuilika kama kufeli masomo, migogoro ya mapenzi na ndoa, mali, umaskini, maradhi na changamoto nyingine za kimaisha.

Tufanyaje???

1. Eleza hisia zako kwa mtu unayemuamini.
Kueleza hisia na misukosuko unayopitia si dhambi wala aibu, tafuta mtu wako wa karibu zaidi umueleze. Kusema si sawa na kuficha. Kusema hutoa ahueni moyoni na kupunguza uzito wa jambo ambalo mwisho wake unaweza kuwa kujinyonga ama maamuzi hasi mengine.

2. Fanya mazoezi.
Mazoezi ya viungo si huimarisha mwili tu, bali hukomaza na kuboresha afya ya akili kwa kukufanya ufanye maamuzi chanya yenye tija.

3. Kula mlo kamili.
Mlo una mchango mkubwa katika kuboresha afya zetu za akili na hivyo husaidia kuamua ipasavyo. Ikiwa hujajaaliwa mlo mzuri, kula ulichopata huku ukiwa na imani ya kufikia kesho yako yenye amani na nuru.

4. Jichanganye na jamii.
Epuka kukaa mwenyewe kwani kukaa peke yako hupelekea fikra potofu na mawazo mgando. Jichanganye, shiriki katika jamii na pata muda mwingi wa kubadilishana mawazo na jamii inayokuzunguka.

5. Jikubali na ujithamini.
Wengi huzorotesha afya zao kwa sababu ya kuiga watu katika mitandao, ndugu ama jamii wanazotoka hali inayowapelekea kuwaza vitu visivyo na msingi. Ishi namna ulivyo, jikubali, jithamini. Wako watu wanatamani wawe ulivyo, usijishushe thamani!

Zaidi ya yote tuwatumie wanasaikolojia katika kuhakikisha afya zetu za akili tunaziimarisha na kupiga vita mashaka na changamoto za Dunia ambazo haziishi.

Serikali na jamii kwa ujumla ina haja ya kuhakikisha watu wake wanakuwa na afya njema za akili na miili kwa kuwatumia viongozi, wasanii na watu wenye ushawishi wakishirikiana na wanasaikolojia katika kufikisha ujumbe na hamasa dhidi ya afya ya akili. Kama tutiavyo juhudi katika mambo ya kiserikali kama ukusanyaji wa kodi na utoaji huduma za kijamii kwa jamii, hili pia linahitaji kipaumbele, Tunateketea!

Kufanya hivi hakutaimarisha afya zetu tu bali itahakikisha ubora wa fikra na mawazo chanya dhidi ya ustawi wa Taifa lenye uchumi, jamii na siasa yenye nuru.

View attachment inbound6167501961367513769.jpg
Okoa Maisha, Okoa Taifa!
Kesho njema inaanza na wewe. Jamii yetu inakumbwa na mengi ambayo ni vigumu kuyatatua lakini si afya zetu za akili, tulishinde!

Chukua hatua!!!
 
Upvote 1
Back
Top Bottom