Habari, naomba Kusaidiwa katika hili hizi ajira wanasema 30,000 ya malazi ni za kweli Maana walioomba Ni wengi sana
- Tunachokijua
- Lake Oil Limited ni kampuni inayojihusisha na uuzaji wa nishati ya mafuta yanayotumiwa na vyombo vya usafiri pamoja na shughuli nyingine zinazotegemea nishati hiyo.
Mbali na huduma ya mafuta vituo hivyo piavinatoa huduma mbalimbali kama bidhaa za maduka ya rejareja, sehemu za kuosha magari, migahawa ya vyakula vya haraka, huduma za matengenezo ya magari, huduma za umeme wa LUKU, pamoja na huduma za ATM. huduma za kampuni hiyo hupatikana jijini Dar es Salaam na karibu kila mkoa nchini Tanzania.
Kumekuwapo na barua ambayo inaonesha kuitwa kwenye usaili wa maombi ya kazi katika kampuni ya Lake Oil Limited huku kukiwa na utata juu ya uhalisia wake.
Je, ni upi uhalisia wa barua hiyo?
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck umebaini kuwa barua hiyo si kweli na hata madai ya kuitwa kwenye usaili si ya kweli kwani Kampuni ya Lake Oil haikutangaza nafasi za kazi na kuita waombaji katika usaili.
Tovuti na kurasa za mitandao ya kijamii ya Kampuni hiyo hazichapisha kuhusu uwepo wa nafasi za kazi wa kuitwa katika usaili kwa waombaji wa nafasi za kazi. Vile vile tovuti ambazo huchapisha matangazo ya nafasi za kazi kutoka taasisi mbalimbali hazikuchapisha juu ya tangazo la nafasi za kazi kutoka kampuni ya Lake Oil hivi karibuni.
Aidha JamiiCheck imebaini mapungufu kadha katika barua pamoja na ujumbe wa barua pepe uliotumiwa kufikisha taarifa ya usaili huo, sehemu ya mapungufu hayo ni pamoja na kutofautiana kwa namba ya sanduku la posta ambapo Kampuni hutumia S.L.P 5055 Dar es salaam, Tanzania, tofauti na iliyotumiwa katika barua hiyo 45445 Dar es salaam. Uwepo wa barua pepe (mhasibuolake@gmail.com ) ambayo haitumiwi na kampuni hiyo katika maombi ya kazi badala yake tovuti rasmi inaonesha barua pepe rasmi zinazotumika ni admin@lakeoilgroup.com na hr@lakeoilgroup.com kadhalika ujumbe wa barua pepe neno energies katika ‘O - Lake energies’ limekosewa kwa kukosekana kwa herufi ‘r’
Kampuni ya Lake Oil Energies katika tovuti yake ina sehemu maalumu inayomwezesha mtu yeyote anayetuma maombi ya kazi, kuyatuma kupitia tovuti hiyo.
Ujumbe wa barua hiyo hauna ukweli wowote bali umetengenezwa na watu wenye nia ovu ya kutaka kuwaibia watu wenye uhitaji wa kazi. Mara nyingi maombi ya kazi pamoja na usaili huwa ni bure katika taasisi mbalimbali zinazotangaza nafasi za kazi, hivyo ni vema kuwa makini na maombi yanayohitaji malipo ya fedha katika michakato hiyo.