Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,771
- 41,027
Na. M. M. Mwanakijiji (Tanzania Daima)
MIONGONI mwa hesabu rahisi kabisa kujifunza ni hesabu za seti. Ni miongoni mwa mambo ya msingi kabisa ambayo mtoto anajifunza katika kuhusisha mafungu mbalimbali ya vitu na idadi.
Hata hivyo lengo kubwa la kujifunza hesabu za seti si kujua hasa idadi ya vitu bali kujua vitu vinahusiana vipi na kuweza kupima kipi kikubwa chenye kuhusisha vitu vingi zaidi. Hivyo, kama umesahau hesabu hizi usiwe na shaka nitakukumbusha kwa haraka haraka (hivyo usitimke!).
Hesabu za seti zinahusu makundi ya vitu mbalimbali. Zinahusu kuhusisha kundi kubwa na makundi madogo madogo na kuona jinsi gani makundi madogo yanahusiana na kundi kubwa na jinsi gani yenyewe yanahusiana au kutohusiana.
Kwa mfano, katika kundi kubwa (Seti kubwa) ya "Vyombo vya usafiri" vimo vyombo vyote vinavyotumiwa na wanadamu kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ukiondoa miguu yao.Ndani ya hii seti kubwa kuna makundi madogomadogo (seti ndogo) za "vyombo vya majini", "vyombo vya anga" na vyombo vya "ardhini".
Na seti hizo ndogo ndogo nazo zinaweza kugawanywa ndani yake na kukuta kwa mfano kwenye vyombo vya majini kuna "mitumbwi, ngalawa, merikebu, nyambizi" na kwenye vyombo vya ardhini kuna "pikipiki, treni, mabasi, magari madogo madogo, punda, ngamia n.k."
Sasa mtu anaweza kuendelea kugawanya seti hizo ndogo ndogo hata kwa aina ya nishati inayotumika, watengenezaji, nchi vinakotoka vyombo hiyo n.k
Lakini mwisho wa siku, vitu hivyo vyote hata uviweke kwenye seti ndogo kiasi gani bado vinabakia kuwa kwenye seti kubwa ya "vyombo vya usafiri."
Sasa mtu ambaye ujuzi wake au uzoefu wake ni kutumia usafiri wa punda mnaweza kubishana milele ukijaribu kumfafanulia faida ya kusafiri na ngamia au ubora wa ngamia, kama vile mtu ambaye hajawahi kupanda ndege na amezoea mabasi, ukimuambia raha na uharaka wa kupanda ndege.
Sasa, bila ya kuzama sana kwenye seti za vyombo vya usafiri, niseme kwamba tuna seti moja kubwa inaitwa "Watanzania". Seti hii inajumuisha watu wote ambao wana uraia wa Tanzania.
Seti hii haingalii usomi, dini, rangi, kabila au kitu kingine chochote, yenyewe inaangalia kitu kimoja tu nacho ni "je wewe ni Mtanzania". Kama wewe ni Mtanzania basi umo ndani ya seti yetu. Hivyo, mtu yeyote ambaye ni Mtanzania anaingia kwenye seti hii bila hata ya kubisha hodi.
Hata hivyo, seti yetu hii ndani yake yenyewe kuna seti nyingine ndogo ndogo ambazo hao Watanzania wamegawanyika ndani yake.
Nitatumia seti ndogo tatu nazo ni "Makabila", "Imani/Dini" na "Vyama vya Siasa."
Kwenye seti ndogo ya "Makabila" kuna seti ndogo za "Wakurya, Wanyiramba, Wamatengo n.k", na kwenye seti ndogo ya "Imani/Dini" ndani yake kuna "Waislamu, Wakristu, Wapagani, Wabudha n.k" hali kadhalika kwenye seti ndogo ya "Vyama vya Siasa" kuna "Wana CCM, Wana CHADEMA, Wana CUF, n.k."
Wakati mwingine, utakuta mtu ni mwanachama wa seti hizo ndogo zote tatu, kwamba yuko kwenye kabila la Mnyaturu, ni Muislamu na vile vile ni mwanachama wa CHADEMA. Lakini bado ni Mtanzania (seti kubwa).
Utakutana na mtu mwingine ambaye yuko ndani ya Ukristu lakini hajitambulishi na kabila moja la Tanzania, lakini bado ni Mtanzania (mfano mzungu aliyehamia toka Uingereza na kuupata uraia wa Tanzania.)
Vile vile unaweza kukutana na mtu ambaye ni mwanachama wa chama siasa lakini haamini dini yoyote ile na tena yawezekana haamini hata uwepo wa Mungu. Huyu naye ni Mtanzania.
Hivyo, sisi sote katika vijiseti vyetu vidogo vidogo tuna tofauti. Tena wakati mwingine tofauti hizo ni kubwa mno na zinaweza kusababisha hata watu watoane ngeu. Lakini tukijiangalia katika picha kubwa tunajikuta kuwa sisi ni Watanzania, SISI TUKO KWENYE SETI MOJA.
Malumbano na migongano ya maneno ya hivi karibuni katika mjadala wa Kadhi, mjadala wa OIC, mjadala wa Ilani ya Wakatoliki (Waraka), na mijadala ya kisiasa Bungeni imenithibitishia kuwa sisi sote kwa namna tofauti tofauti tumepigwa upofu wa kutoona nje ya seti zetu.
Hapa nazungumzia seti ndogo ya Dini/Imani. Karibu sisi sote tumejikuta tukigawanyika kwa misingi ya dini zetu na dini za wale tunaowaunga mkono katika mijadala hii.
Waislamu wamejikuta wakiunganishwa pamoja kutetea Mahakama ya Kadhi na Tanzania kujiunga OIC. Wakristu wamejikuta wakijiunga pamoja kupinga Mahakama ya Kadhi na Tanzania kujiunga OIC.
Na Wanasiasa wamefuata misingi ya dini zao kutetea Bungeni yale wanayokubaliana na imani zao; Wakristu wanaonekana kuunga mkono viongozi wao Wakristu, na Waislamu wanaonekana kuunga mkono yale viongozi wa Kiislamu wanataka. Kila mmoja hataki kutoka nje ya seti yake.
Inasikitisha na inatisha.
Inasikitisha kwa sababu inathibitisha kile nilichokisema miaka karibu miwili iliyopita; kwamba "wameshindwa kuongoza, sasa wanatuburuza."
Ndio maana yangu ya kuwabambikia hawa tunaowaita viongozi kuwa ni "watawala wetu." Neno hilo nililitunga nikimaanisha kuwa hawa siyo viongozi tena, bali ni mabingwa wa kutawala na katika kututawala hivyo badala ya kutushawishi ili tukubaliane nao, wamebakia kutuburuza.
Lakini sasa bahati mbaya, wakati wanatuburuza sisi wengine, wao wenyewe wamebakia kushikana mashati. Kwenda mbele hawendi, kurudi nyuma aibu, kukubali kushindwa hawawezi; imebakia kupigana mikwara.
Inatisha kwa sababu kwa kadiri wanavyoendelea kushikana mashati kitakachofuatia, mmoja atampiga ngumi mwingine, na mara mwingine ataingilia kati akaambulia kisukusuku, matokeo yake wanapigana na wale Watanzania wenye kufuata seti zao ndogo ndogo watajipanga kuunga mkono upande mmoja au upande mwingine.
Ninachosema ni kuwa, kiuzembe uzembe na kijinga kijinga, sisi wenyewe tunatengeneza mazingira ya kuleta machafuko ambayo kwa mtu yeyote mwenye akili timamu hayana A wala Z.
Lakini hizi seti ziko vipi? Je mtu anaweza kutoka nje ya seti yake na kujaribu kuangalia kile kilichoko kwenye seti nyingine ili akielewe? Je, kwa vile wote tuko kwenye seti moja, tunaweza kukaa chini pamoja na kusema ni nini kilichobora kwa seti yetu nzima.
Hadi hivi sasa sijaona kiongozi ambaye anafikiria nje ya seti yake. Wengine (kama kina Kingunge) wanajaribu kutokuwa na upande, lakini wanapofanya hivyo wanaonekana wamechagua upande! Hivyo wanaongeza kukorogana.
Kikwete, amekaa pembeni anamtuma Pinda na kumuweka mahali pagumu; kabla hawajatulia, Membe naye anakuja na jambo jingine; wote wawili ni Wakatoliki wanatolea misimamo ya serikali masuala ya Waislamu.
Waislamu wanajiuliza "kulikoni". Mufti na wenzake na wenyewe wanakuja juu wanataka kile ambacho wanaamini ni haki yao. Mohammed Said anasema Waislamu wameonewa; Mara Hizibu nyingine imeibuka inasema utawala bora ni dola ya Kiislamu; Kilaini naye anakuja na hoja zake na kabla hatujatulia, Mokiwa naye ndani na hatujavuta pumzi Khalifa Khamisi. Mtanzania wa kawaida anakodoa macho anajiuliza "kaugonjwa gani kamewakumba hawa?"
Hebu tuziangalie hizi seti ndogo ndogo, tuangalie kama mtu ambaye yuko nje ya seti hizo:
Wakatoliki/Wakristu
Hawa ndugu zetu wamekuja na Ilani pamoja na mwongozo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010. Kwa mujibu wa utangulizi wa Ilani hiyo Wakatoliki wametoa mapendekezo yao kwani ni "muhimu kupendekeza vipaumbele vyetu kama jamii tukiwaambia viongozi wetu wajao yale ambayo tungependa yafanyike kwa ajili ya jamii yetu.
Katika uchaguzi, hatupigi kura tu, tunapaswa kueleza makusudio yetu kwa yale tunayofikiri kuwa muhimu sana kwa Taifa."
Ukisoma Ilani nzima utakutana na mambo mengi mazuri na ya kuvutia ambayo hata watu wa seti nyingine wakiyasoma (ukiondoa machache) wanaweza kuyakubali tu. Tatizo ni kuwa, Wakatoliki wametoa mapendekezo yao kutoka kati seti yao lakini wanataka yakubalike na watu wa seti nyingine pia! Wanaamini kuwa ni mambo mazuri kwa "jamii" lakini wakati huo huo wanapendekeza mambo mengine yasifanyike ambayo watu wa seti nyingine wanaona ni muhimu kwa jamii vile vile.
Matokeo yake, wanawavutia watu wa seti moja (Wakristu wenzao) na wakati huo huo kuwatenga mbali watu wa seti nyingine (Waislamu).
Kwa vile Ilani yao na Mwongozo wao vyote vimetoka katika mtazamo wa seti ya Wakatoliki/Wakristu hata kama kuna mazuri 1001, Waislamu wanajikuta siyo tu wametengwa lakini wanaonekana wamelengwa na nyaraka hizo. Hivyo, Waislamu wanakunja nyuso zao, seti yao inatishiwa.
Wakatoliki wanasema hizi nyaraka zinawatishia mafisadi; wanadai kuwa mafisadi ndio wanaziogopa. Hawajali hisia na fikra za ndugu zao Waislamu. Wanapuuza madai ya Waislamu, wanayaona hayana msingi, hawako tayari kukaa chini kuyaelewa.
Inanikumbusha matukio ya Mwembe Chai na yale ya Pemba. Jinsi dola ilivyotumia nguvu chini ya kiongozi Mkatoliki (Benjamin Mkapa) dhidi ya raia wasio na silaha kali.
Nilitarajia viongozi wa Kanisa wangetoa msimamo mkali wakati ule, lakini kinyume chake walionekana kutoa baraka za vitendo vile. Hawakutaka kuungana na ndugu zao Waislamu kutaka uchunguzi huru ufanyike. Hawakufanya hivyo, kwa sababu watu walioshambuliwa si watu wa seti yao, na bahati mbaya kiongozi aliyeruhusu mambo hayo ni mtu wa seti yao!
Sasa leo serikali ikiwa chini ya kiongozi Muislamu, Wakatoliki wanaonekana wana ujasiri wa kuzungumza sana na hata kuinyoshea kidole serikali. Sitashangaa muda si mrefu ujao majina ya viongozi wa kisiasa yataanza kutajwa hadharani kuwa hawafai. Fikra za seti zinadumishwa.
Waislamu
Ndugu zetu Waislamu nao wako kwenye seti yao. Katika seti hii kila mtu anachosema kinachogusa Waislamu bora afikilie mara mbili kwani vinginevyo atanyoshewa kidole kuwa ni "adui wa Uislamu." Hivyo imefikia mahali watu wanaamua kufunga vinywa vyao kwa sababu hata kama wanaujua ukweli au wanataka kuchangia jambo fulani lenye manufaa wanaogopa kunyoshewa kidole.
Matokeo yake ndani ya seti hiyo hiyo kuna kugawanyika. Wapo wale wanaoounga mkono BAKWATA na wamsikiliza Mufti na pia wapo wale ambao ukiwatajia neno ‘BAKWATA' wanaona umewatajia kitu kutoka sayari nyingine. Kwa hilo kundi la pili, BAKWATA ni chombo cha serikali.
Hivyo, wanaikataa kuwakilisha maslahi yao. Wakati huo huo, watu wa Bakwata wanajua kuwa wao wanawakilisha waislamu wengi zaidi nchini na hivyo wanazungumza kwa niaba ya waislamu wengi (japo si wote).
Sasa, katika seti hii kuna watu ambao wao hakuna lolote ambalo serikali inaweza kufanya likawa zuri isipokuwa lenye maslahi kwa Waislamu kwanza. Na kama kuna kitu ambacho kimenishtua, ni pale kundi fulani lilipojitokeza na kudai kuwa kama Mahakama ya Kadhi haitaundwa, basi Waislamu wasiichague CCM mwaka 2010.
Yaani, kati ya vitu vyote ambavyo vinaweza kusababisha watu wasiichague CCM, kwao suala la Mahakama ya Kadhi ndiyo msumari wa mwisho! Lakini vile vile wanaposikia Wakatoliki wamekuja na mwongozo wa kupiga kura na wao wanakuja juu kwanini Kanisa linaingilia siasa. Lakini hawakusimama kuwapinga watu wa seti yao waliposema Waislamu wasiichague CCM.
Naweza kuendelea na kuchambua seti hizi na kuonyesha ni jinsi gani zimefungwa katika seti zao na matokeo yake sisi wengine tunaburuzwa tu.
Ni mpaka pale viongozi wa Kiislamu na viongozi wa Kikristu na hata wasio na dini watakapotoka nje ya seti zao na kujiangalia kama watu wa seti moja kubwa (Watanzania) ndipo baadhi ya matatizo yanaweza kuonekana vizuri na masuluhisho yaliyo bora kwa wote yanaweza kupatikana.
Kwa mtindo wa sasa, kila seti inasababisha matatizo yake na hivyo kusababisha matatizo kwa seti kubwa na suluhisho, yote yanatolewa yakiwa na misingi ya fikra za seti.
Vipi nao Wapagani?
Ukisikiliza mijadala ya kidini inayoendelea unaweza kuamini kabisa kuwa Tanzania ina Waislamu na Wakristu tu! Imefika mahali wanazungumza kana kwamba wanawakilisha Watanzania wote. Tena ukiangalia vizuri utagundua kuwa wote hawa wanajivunia dini za kigeni kila mmoja akitaka kujionyesha anaishika dini yake zaidi na imefika mahali, wanazungumza kana kwamba dini hizo zina haki miliki ya dini Tanzania.
Sasa ni nani anatetea maslahi ya wale wanaoabudu mizimu na wenye imani za jadi? Je hawa imani zao ni za chini kulinganisha na za Wakristu na Waislamu na hivyo siyo Watanzania kamili?
Je, hawa nao wana nafasi gani katika mijadala inayoendelea? Kwa mfano itakapoanzishwa mahakama ya Kadhi, je Mpagani au mtu asiye na imani ambaye ameoa Muislamu au Kuolewa na Muislamu ana haki gani?
Je wale wasio na imani na wenyewe wachague viongozi wajao kwa misingi ipi au ni nani atakayetoa muongozo ukasikika? Ni kwa sababu hiyo sitaki kuamini kuwa serikali inawasikiliza Wakristu na Waislamu zaidi kana kwamba seti ya imani ina makundi hayo mawili tu!
Hoja yangu kubwa ni kuwa, tujifunze kukaa pamoja kama watu wa seti moja. Tofauti zetu ziwe msingi wa sisi kukaa pamoja kuzungumza na kujaribu kutafuta utatuzi wa migogoro yetu.
Tusijikite katika seti zetu hizi kiasi kwamba mtu mwingine wa seti nyingine akisema jambo, hata kama ni bora, basi tunalipinga alimradi hatutaki kuonekana tunamuunga mkono hata kama ukweli wa jambo hilo.
Ndugu zangu, kama kichaa anakupigia kelele utoke barabarani kwa sababu kuna gari linakuja kwa kasi, utamdharau na hautaungalia upande anaoelekeza kwa sababu yeye ni kichaa? Kama adui yako akikuambia ‘angalia mwiba huo,' utaendelea kukanyaga na kuvumilia maumivu kwa sababu hukutaka kumsikiliza adui yako? Kufanya hivyo ni kujificha katika seti.
Napendekeza kabla hatujazama katika ubovu wa seti zetu na kiburi cha seti zetu, tukae pamoja tuzungumze. Ningependa kweli kuona muongozo wa kuelekea uchaguzi mkuu unatolewa kwa pamoja na viongozi wote wa dini baada ya kukaa pamoja.
Muongozo ambao utatufaa watu wa seti zote. Muongozo ambao kweli mafisadi wataogopa kwani hakuna mtu wa seti yao atakayesimama kuubeza kwa vile umetolewa na seti moja kubwa; ya WATANZANIA.
mwanakijiji@jamiiforums.com