Leo asubuhi katika makazi yangu mapya Dar es Salaam walikuja wadada wawili kudai kilichoitwa hela ya taka na mazungumzo yetu yalikua kama ifuatavyo;
Wadada: Kaka mambo
Mimi: poa
Mdada 1: Kaka hela ya taka
Mimi: wenyewe hawapo
Mdada 1: wewe si muhusika pia inabidi utoe hela ya taka
Mimi: Dada mimi sipiki wala sifagii...nitoe hela ya taka kwani nazalisha taka gani? Mana hata kushinda nashinda job
Mdada 2: huyu atatoa tu hela
Jirani: wewe dada huyo mkaka mgeni kahamia hana hata mwezi.
Kesi ikaisha hivyo ila nadhani watarudi tena. Asa mimi naomba kufahamishwa kuhusu hii hela ya taka, nalipia taka au kitu gani?
Sishindi home Sifagii Alafu wanakuja wadada tu wanavijora hawasemi wao wakika nani wanataka hela ya taka. Kweli ndo mnavyoishi hivyo?
Pole sana ndugu meneja.
Kosa lipo upande wa hao wanaokuja kuchukua hela ya taka bila kujitambulisha na kukuelimisha na kukupa nafasi uulize maswali kwa ufahamu zaidi lakini kwa ufupi ngoja nikuelezee kidogo juu ya utaratibu unavyopaswa kuwa japo mimi swishing Dar naishi mkoani;
Kwanza suala la usafi wa mazingira ni moja wapo ya majukumu ya msingi ya Halmashauri zetu za majiji/manispaa/miji na wilaya.
Hivyo utaratibu unaosimamia zoezi la ukusanyaji, usafirishaji, uchambuzi na uteketezaji wa taka unatungwa na kila Halmashauri husika kulingana na mazingira yake yalivyo. Maana yake utaratibu wa Halmashauri A unaweza kutofautiana na utaratibu wa Halmashauri B ikiwemo kiwango kinachotozwa kama Ada ya huduma ya uzoaji taka. Baadhi ya Halmashauri zinatoza 3,000/ kwa kaya kwa mwezi na Halmashauri nyingine zinatoza 5,000/ kwa kaya kwa mwezi.
Kwanza lazima uelewe kuwa wajibu wa kulipia huduma ya uzoaji taka uko kisheria na kushindwa kulipa ada hiyo ni kukiuka amri halali ya serikali hivyo unaweza kushtakiwa mahakamani.
Pia upande wa pili unaeleza juu ya haki zako kama mteja ikiwa ni pamoja na kuelimishwa juu ya umuhimu wa kutunza mazingira na kupata huduma stahiki kwa siku mliyokubaliana na mtoa huduma wenu. Pia sheria hiyo huwa inatoa nafasi kwa mteja/mwananchi kumshtaki mahakamani mtoa huduma kama atakiuka makubaliano mfano kama hazoi taka kwa wakati au hazoi kabisa na mambo kama hayo.
Ushauri wangu kwako ni kumuuliza jirani yako ili upate mawasiliano ya mtoa huduma katika eneo lako au namba ya Afisa Mtendaji wa Mtaa wako ili ujue ratiba na utaratibu mzima ikiwemo kiwango unachopaswa kulipa kwa mwezi.
Mwisho, nikuelimishe kidogo na kwa faida ya wengine ni kuwa hakuna mtu hai anayeweza kukaa mahali hata kama hapiki asizalishe taka maana kuzalisha taka ni sifa mojawapo ya msingi kwa kila kiumbe hai. Hivyo wote tunaathiri mazingira tunamoishi kwa namna moja au nyingine hivyo tunawajibika kulipia ada ya uzoaji taka ili mazingira yetu yaendelee kubaki safi na salama kwetu kuishi na vizazi vijavyo.
Kama kuna mwenye swali aulize tutaelekezana na kuelimishana.