SoC01 Wanafunzi wafundishwe sanaa shuleni

SoC01 Wanafunzi wafundishwe sanaa shuleni

Stories of Change - 2021 Competition

MTEGULE

Member
Joined
Jul 16, 2021
Posts
15
Reaction score
22
WANAFUNZI WAFUNDISHWE SANAA SHULENI.

Sanaa ni ufundi au ujuzi ambao unatokana na fikra za mwanadamu na kuwasilisha kwa wengine. Sanaa imebaba matawi mbalimbali kama vile ushonaji, muziki, uhunzi, Ufinyanzi, uchoraji,fasihi,maonyesho na utarizi.

Ufundishwaji wa sanaa shuleni kutokea ngazi ya chini ya shule ya msingi hadi ngazi ya sekondari ni jambo muhimu sana na yapaswa lipewe kipaombele kwa kiasi kikubwa ili kuwa na maendeleo yenye tija kwenye jamii yetu ya sasa na hasa hichi kizazi tulichonacho.

ZIFUATAZO NI FAIDA TANO (5) MUHIMU AMBAZO ZITAPATIKANA KAMA SANAA IKAFUNDISHWA NA KUTILIWA MKAZO SHULENI.

Mosi: Kukosekana kwa wimbi la watu wengi wasiokuwa na ajira: Hivi sasa kuna uwepo wa watu wengi ambao wamehitimu masomo yao katika vyuo vya kati na vyuo vikuu. Wengi wao wanasubiri kuajiriwa kwenye serikali au hata mashirika na makampuni binafsi ili waweze kukidhi mahitaji yao.Ama kweli mchumia juani hulia kivulini lakini methali hiyo kwao wao haina maana kwani wanafunzi wengi waliohitimu masomo yao bado wanasota mtaani na hakuna ajira rasmi ambazo wengi wao walizitarajia. Lakini ingalikuwa wamefundishwa na kutiliwa mkazo ufundishwaji wa sanaa basi wangejiajiri katika sanaa mbalimbali kama vile muziki,ushonaji na uchoraji.

Pili: Itasaidia watu kupata mahitaji muhimu na kukidhi haja ya maisha yao: ikiwa mwanafunzi atafundishwa ipasavyo sanaa basi itakua ni chachu ya maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa zima kwa ujumla mfano kama uchoraji na muziki ambapo hapa tunaweza kupata wanamuziki na wachoraji mahiri.Watu wengi wanajipatia pesa za kuendesha maisha yao na kulipa kodi katika nchi kutokana na shughuli za sanaa wazifanyazo.

Tatu: Kukuza na kuongeza pato la taifa: hili lipo wazi kabisa kupitia kufungua mashirika,makampuni na taasisi mbalimbali ambazo zitajishughulisha na masuala ya sanaa na ikumbukwe kwamba ulipaji wa kodi utafanyika na kusababishwa uboreshaji wenye tija na ulio mzuri katika huduma mbalimbali za kijamii kama vile umeme, maji na miundombinu kama vile barabara. Hivyo vyote vitaboresha kutokana na ulipaji kodi unaotokana na vijana au watu waliotumia sanaa kama fursa.Mfano uliowazi kabisa ni wa msanii Nasibu Abdul "Diamond" ameweza kutumia sanaa ya muziki kuongeza kipato chake binafsi na taifa zima kwa ujumla lakini pia kuwafungulia fursa vijana wengine.

Nne: Upatikanaji wa huduma na bidhaa hapa hapa ndani ya nchi bila ya kuwategemea mabepari: ikiwa kama sanaa kama vile sanaa ya utarizi, sanaa ya uhunzi, sanaa ya ushonaji ikasimamiwa vizuri na kupewa kipaombele shuleni itasaidia watu katika jamii kutokua tegemezi na sisi tukazalisha bidhaa zetu hapa hapa ndani kama vile nguo, viatu, vifaa vya kilimo na bidhaa nyingine mbalimbali.

Tano: Kulinda na kuthamini mila na tamaduni zetu kama watanzania: Sanaa hajawacha nyuma suala la kulinda na kuthamini kule tulikotokea mathalani kupitia sanaa ya uhunzi na sanaa ya uchoraji hizi ni sanaa ambazo zilikuwapo tokea hapo mwanzo lakini pia sanaa ya muziki ambapo makabila mengi hapa nchini Tanzania hutafsiriwa kwa kuwa namna mbalimbali za ngoma ambazo huwaburudisha wao.

Ningependa kushauri wizara husika kulisimamia hili kwa mapana yake na kulishikilia kwa magego ili tuweze kupata faida mbalimbali. Ni Kweli kwamba zipo baadhi ya shule hufundisha lakini ni kwa kiwango kidogo mnoo na huchukuliwa kama ni jambo la ziada, kumbe ni jambo ambalo inabidi lipewe kipaombele kuliko masomo mengine.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom