SoC02 Wananchi: Tusiwaogope vigogo kama Ney Wamitego

SoC02 Wananchi: Tusiwaogope vigogo kama Ney Wamitego

Stories of Change - 2022 Competition

Mwanakapaya

New Member
Joined
Oct 3, 2021
Posts
2
Reaction score
1
"Niliyesimama mbele yenu siyo mbunge ni msanii
Natumia sanaa kuitetea jamii
Naongea nikiwa Bongo sitakimbia kama Roma
Mkiniteka mkinifunga bado dunia itasonga"
(Ney Wamitego, 2021)​

‘Ney Wamitego –True boy’ ni Mwanamuziki wa kizazi kipya ambaye ukiachana na jina lake hilo la kisanii, jina lake ni Emmanuel Elibariki. Huyu ni msanii maarufu nchini Tanzania anayeimba nyimbo zenye mahadhi ya kufokafoka (Hip Pop). Moja ya mambo yanayompa umaarufu zaidi na kumfanya aendelee kuwa gumzo katika tasnia yamuziki wa bongo fleva ni uwezo wake wa kuandika maishairi yenye ujumbe unaokosoa vigogo.

Wataalamu wa Fasihi wanakubaliana kuwa bongo fleva ni sehemu ya mashairi kwahiyo mashairi ya bongo fleva kama hayo ya Ney wa Mitego ni moja ya kazi za fasihi. Aidha, inafahamika kwamba kazi ya fasihi, mbali na kuburudisha, huelimisha, huonya na kuadabisha. Hata hivyo wasanii wa kazi za fasihi hukubwa na rungu la mdhibiti kiasi kwamba kazi zao huweza kufungiwa au wao wenyewe kutiwa nguvuni.

Ni kwa sababu hii, wasanii wengi huamua kutunga tungo zinazoangukia kwenye moja ya makundi yafuatayo:

Mosi, tungo zenye maudhui yanayo sifia hao wadhibiti. Hizi ni tungo za kikasuku ambazo hufumbia macho maovu yanayotendwa na wenye mamlaka na kupongeza kila kinachofanywa. Maranyingi tungo za aina hii hupendwa sana na watawala.

Kundi la pili ni tungo pendwa. Hizi ni tungo zisizo na maudhui mazito bali huwa na lengo la kuburudisha zaidi ya kuelimisha jamii. Hutawaliwa na fani inayoibuwa hisia na kukonga nyoyo za hadhira. Agharabu huwa na maudhui yanayohusu starehe kama vile pombe na mapenzi.

Kundi lingine ni tungo zenye mafumbo magumu. Baadhi ya wasanii huamua kutunga nyimbo zenye mafumbo magumu kuyafumbua ambapo huwa hazielezi wazi wazi maudhui. Hizi ni tungo zitumiazo mtindo wa kistiari jambo ambalo hufanya hadhira kushindwa kuupata ujumbe uliokusudia kirahisi. Mrisho Mpoto ni mfano mzuri wa msanii anayependa kutunga tungo za namna hii.

Aidha kutokana na sababu za kibiashara, wasanii wengi huchagua kutunga tungo zinazoangukia katika kundi la pili. Hali hii inathibitika ukichunguza nyimbo za bongo fleva zinazotoka kila siku. Utabaini kuwa nyimbo nyingi ni za mapenzi. Hizi ndizo nyimbo zinazopendwa na watu wengi hususan vijana.

Kwa upande wa Ney wa Mitego hali ni tofauti kidogo. Katika siku za hivi karibuni amejipambanua kama msanii ambaye haogopi ‘vigogo’(viongozi wa serikali, viongozi wa dini na hata vyombo vya dola). Vigogo ndiyo wenye rungu la udhibiti (BASATA), hawa ndiyo hulifanya rungu hilo kuwakung’uta wasanii wanaojitia ujasiri wa kukosoa mwenendo wa mambo.

Mnamo mwezi machi mwaka 2017, Ney wa Mitego alikamatwa na jeshi la polisi la Tanzania kwa madai ya kufanya kosa la kuimba wimbo uitwao “Wapo” unaokashifu serikali. Wimbo huo ulifungiwa na BASATA kwa madai ya kukiuka maadili na baadae rais wa wakati ule hayati Dkt John Pombe Magufuli aliagiza ufunguliwe kwa kuwa hakuona ubaya wake.

Ubeti mojawapo wa wimbo huo una maneno yafuatayo:

"Kuna viongozi na TV naona zimeshapoteza CV
Hakuna uhuru wa habari wala taarifa ya habari
Wanapindisha pindisha tu kuiogopa serikali
Siamini nchi inaendeshwa na kiki
Siasa inafunika muziki
Wanagombea front page wauze kwenye gazeti
Nasikia kuna viongozi wamefoji vyeti
Katika unbeti mwingine kuna maneno haya:
Samahani mheshimiwa hivi unamjua Bashite
Hili ni jipu jipya toka koromije"…​

Hapa tunaona Ney wa Mitego bila woga anaamua kusema kwa uwazi yale ambayo yalikuwa yakitokea katika jamii wakati huo. Pasi kumuogopa yoyote anaeleza namna ambavyo uhuru wa vyombo vya habari ulivyominywa. Ikumbukwe wakati huo kulikuwa na malalamiko miongoni mwa jamii hususan wanaharakati na wanasiasa wa upinzani kuwa demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari vilitoweka. Pengine hii ndiyo dosari kubwa iliyokuwa ikitajwa kuwa ya rais Magufuli. Aidha, kulikuwa na kiongozi mmoja wa umma aliyedaiwa kufoji vyeti. Kiongozi huyo kwa mujibu wa Askofu Gwajima katika mahubiri yake kanisani alikuwa ni RC wa wakati huo wa mkoa wa Dar es Salaam ndungu Paul Makonda. Ney wa mitego hakumuogopa akamuimba kwenye wimbo wake.

Mapema baada ya rais Samia kushika kijiti cha urasi alichoachiwa na mwendazake rais Magufuli aliyefariki mnamo machi mwaka huu, Ney wa Mitego alitunga wimbo mwingine ambao kwa ujumla ulilenga kumtahadharisha rais mpya. Wimbo huo pia ulikumbana na rungu la BASATA. Msanii kama kawaida yake katika wimbo huo unaojulikana kwa jina Mama anawasilisha maudhui yake kwa uwazi pasipo kuogopa vigogo. Kwa mfano ubeti mmoja wapo una maneno yafuatayo:

Baba alikuwa mkali mama mwenyewe unajua
Yaani tuliishi kwa taabu japo kuwa ni wa kishua
Siyo sisi tu mpaka wageni walikimbia
Kuhusu kaka yangu ibra natumai ulisikia​

Hapa tunaona Ney Wamitego ana mweleza ‘mama’, ambaye bila shaka ni rais Samia mwenyewe kuwa ‘baba’ yaani rais aliyemtangulia alikuwa mkali jambo lililopelekea watu kuishi kwa tabu na wengine kufikia hatua ya kukimbia nchi. Ukali anaozungumzia Ney Wamitego huenda ni ile hali kuminya uhuru wa kujieleza. Anamrejelea ‘Ibra’ ambaye yawezekana anamaanisha msanii mwezake Roma yaani Ibrahim Musa ambaye anadaiwa kwenda nchini Marekani baada ya kukabiliana na matukio hatari ikiwemo la kutekwa na kupigwa. Ney Wamitego anamkumbusha rais madhira yote ili labda asaidie kuyaondoa. Msanii haogopi kusema yale anayoyaamini.

Katika hatua nyingine, Ney Wamitego anazungumzia sakata la wabunge wa viti maalum 19 wanaodaiwa kufukuzwa na chama chao cha CHADEMA katika ubeti ufuatao.

"Lakini shangazi Halima na wenzake
Mbona bado nawaona kwenye vikao vya ukoo?
Na walishatengwa na familia yao?
Sema kitu kuhusu hili mama"​

Ni wazi kuwa msanii anaongelea wabunge hao. Anataja jina la mmoja wao, ‘Halima’ yaani Mheshimiwa Halima Mdee bila kuogopa. Msanii anaona kuwa wabunge hao hawana uhalali wa kuendelea kushiriki vikao vya bunge (vikao vya ukoo) kwa sababu walishatengwa na chama chao (familia yao). Suala hili limeshasemwa sana na wanasiasa hasa wa upinzani wakidai kuwa bunge linakiuka sheria kwa kuendelea kuwatambua wabunge hao ilhali wameshafukuzwa chama. Msanii naye anaamua kulisema bila woga.

Hivi karibuni msanii huyo ametoa wimbo mwingine ujulikanao ‘Rais wa Kitaa’. Wimbo huo vilevile unazungumzia masuala mbalimbali hususani changamoto za wananchi wa kawaida na maovu ya viongozi. Msanii anawasilisha maudhui yake kwa uwazi bila woga. Mathalani, katika ubeti mojawapo anasema:

Nani kamwambia mheshimiwa eti tumekubali tozo
Hapana sio Tanzania labda Zambia au Congo
Makato ni makubwa wananchi wanaumia
Hivi ni kwamba hamsikii au ndo mnapuuzia?​

Msanii anahoji aliyemwambia mhehimiwa, bila shaka mheshimiwa Rais Samia kwamba wananchi wamekubali tozo. Ikumbukwe katika moja ya hotuba zake, Rais alikaririwa akisema watanzania wamekubali tozo za miamala zilizoanzishwa na serikali yake kwa lengo la kukusanya mapato yatakayotumika katika shughuli za maendeleo. Tozo hizo zimekuwa zikilalamikiwa na baadhi ya wananchi wakiwemo wanasiasa kuwa zinamkadamiza mnyonge. Msanii anasema makato ni makubwa wananchi wanaumia. Pengine sauti yake na zile za wananchi wengine zilisikika ndiyo maana tozo hizo zimepunguzwa. Hata hivyo bado baadhi ya watu wanalalamika wakidai kuwa tozo hizo zinapaswa kufutwa siyo kupunguzwa.

Zaidi ya hayo, Ney Wamitego katika wimbo huo analalamika kuhusu kupanda kwa bei ya bidhaa hasa sukari na mafuta. Anasema:

"Sukari imepanda bei luku,
Tozo pesa wapi nikakope
Sheri buku mbili yangu
wameikataa chombo niikokote
Nani atusemee semee sisi wanyonge
Nani atusemee semee sisi wanyonge"​

Hali hii inadokeza namna wananchi wanavyopata tabu kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu. Wenye mamlaka ya kurekebisha hali ya mambo wanakumbushwa kutimiza wajibu wao ili kuhakikisha hakuna mfumuko wa bei. Msanii ameweza kuueleza ukweli ulivyo bila kuogopa kile kinachoitwa rungu la mdhibiti.

Wakati rais Samia ameingia madarakani hususani ndani ya siku mia moja watu wengi walimpongeza kwa kurekebisha hali ya mambo. Wengi walimsifu kuwa aliweza kurejesha uhuru wa kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari, demokrasia, kurejesha uhuru wa mahakama na kadhalika. Hata hivyo, hivi sasa kumeanza kuibuka malalamiko kuwa jahazi limeanza kwenda mlama tena. Hali hii ndiyo inayosababisha Msanii Ney Wamitego kusema yafuatayo:

Mi ni mmoja kati waliosema unaupiga mwingi
Nahisi una makocha wengi watakukosesha vingi
Nilikwambia hawakupendi wameshakuingiza kingi
Wanakitaka hicho kiti wana tamaa hao madingi​

Yaelekea msanii anaamini kwamba rais anashauriwa vibaya na kwamba washauri hao wanafanya hivyo kwa makusudi kwa lengo la kumwangusha ili baadae wao wakalie hicho kiti. Msaani amemwambia raisi kile anachokiamini bila kuwaogopa hao washauri wake wala yeye mwenyewe Rais. Kazi kwake. Kimsingi Ney Wamitego ni msanii aliyejipambanua kuwa mtetezi na msemaji wa wananchi wenye mawazo kama yake. Pamoja na kuwa baadhi ya nyimbo zake zimekuwa zikifungiwa, zimekuwa zikisambaa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii na ujumbe kuwafikia wananchi wengi.

Nafikiri wasanii wengine pia wanapaswa kuuvaa ujasiri wa Ney Wamitego. Aidha, ujasiri wa aina hii haupaswi kuwa wa mwananchi mmoja au wasanii pekee tu bali wananchi wote tunawiwa kuwa na ujasiri wa kuwaambia viongozi wetu pale tunapoona wanafanya ndivyo sivyo. Ni muhimu wananchi tuwe huru kutoa maoni yetu na hao vigogo wawe tayari kusikiliza maoni yetu. Hii itasaidia kuwa na utawala bora. Wananchi tusiwaogope vigogo kama Ney Wamitego.

Ndimi,
Mwanagenzi.
Mawasiliano: manyukakapaya@gmail.com
 
Upvote 1
Back
Top Bottom