Wanaoharibu elimu yetu wasifumbiwe macho

Wanaoharibu elimu yetu wasifumbiwe macho

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363
Katuni(22).jpg

Katuni


Katika toleo letu la jana Julai 25 ukurasa wa tano tulichapisha habari iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Wizara ya Elimu yahofia uchakachuaji kidato cha tatu.

Katika habari hiyo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilikuwa ikiwaagiza Waratibu Elimu Kata kufanya ukaguzi katika shule zote za sekondari nchini ili kubaini kama wanafunzi wanaosoma kidato cha tatu ni wale ambao walifaulu mtihani wa taifa wa kidato cha pili uliofanyika mwaka jana.

Agizo hilo lilitolewa juzi na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Phillipo Mulugo, wakati akifungua mafunzo ya waratibu elimu kata kitaifa yanayoendeshwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) na kufanyika mjini Bagamoyo, mkoani Pwani.

Mafunzo hayo yanayowashirikisha waratibu elimu kata 1,762 ni ya awamu ya pili na yanalenga kuwawezesha waratibu hao kuleta matokeo chanya katika usimamizi na ufuatiliaji wa utoaji wa elimu ya sekondari nchini baada ya serikali kuwakabidhi jukumu hilo.

Mulugo alibainisha kuwa, mwaka jana katika shule ambazo kulikuwa na matatizo kwa wakuu wa shule kutafuna ada za mtihani wa kidato cha pili baadhi ya wakuu wa shule hizo waliwaruhusu wanafunzi kuendelea na masomo ya kidato cha pili hata kabla ya matokeo ya mtihani wa kidato cha pili kutolewa.

Aliwataka Waratibu Elimu Kata hao baada ya kumaliza mafunzo hayo wafuatilie katika shule zote za sekondari kuona kama wanafunzi wanasoma kidato cha tatu walifaulu mtihani wa kidato cha pili mwaka jana na kisha kupewa taarifa.

Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinaonyesha kuwa wanafunzi zaidi ya 136,000 walishindwa kuendelea kidato cha tatu kutokana na kupata alama chini ya asilimia 30 zilizowekwa na serikali na hivyo kulazimika kurudia kidato cha pili mwaka huu.

Tunaunga mkono agizo hili la Mulugo la kuwataka Waratibu Elimu Kata kufuatilia suala hilo kwani litasaidia kuzuia mapema wanafunzi wasio na sifa zinazostahili kuendelea na masomo.

Jambo hili likiachwa kuwa mazoea litaleta athari kubwa huko mbele kwa kuwa na taifa la wasomi mbumbumbu ambao wataliangamiza taifa hili badala ya kulisaidia kupiga hatua za maendeleo.

Tunasema hivyo, kwa sababu umeibuka mtindo mbaya wa baadhi ya wakuu wa shule wakati mwingine kwa kushirikiana na wazazi wasiojielewa kuwasaidia wanafunzi wakati wa mitihani ili wafaulu hali ambayo inaliweka taifa njia panda kuja kupata wataalamu wasio na sifa siku za usoni.

Ni ukweli usiopingika kuwa sekta ya elimu kwa sasa nchini kwetu imegubikwa na utapeli na ufisadi mkubwa kwa wahusika kuweka zaidi mbele maslahi binafsi kuliko kutoa elimu bora itakayowezesha watakaohitimu kuja kuwa wataalamu wazuri katika sekta mbalimbali hivyo kusaidia kusukuma mbele gurudumu letu la maendeleo.

Hivyo, tunaunga mkono agizo la Mulugo la kutaka kufanyika ukaguzi katika shule zote za sekondari nchini ili kubaini kama wanafunzi wanaosoma kidato cha tatu ni wale ambao walifaulu mtihani wa taifa wa kidato cha pili uliofanyika mwaka jana.

Endapo itabainika kuwa kuna walimu wakuu wamefanya utapeli wa kula ada za wanafunzi wa kidato cha pili na kisha kuwaruhusu waendelee na kidato cha tatu hata kabla matokeo ya mtihani hayajatangazwa, serikali ichukue hatua kali dhidi ya walimu hao ili iwe fundisho kwa wengine wanaofikiria kufanya hivyo.

Hii itasaidia kuondoa mazongazonga ya udanganyifu katika shule zetu na kuhakikisha wanafunzi wanaoendelea na masomo na kuhitimu ni wale tu wenye sifa ili kuliokoa taifa letu kupata wasomi feki.




CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom