JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 2,780
- 6,607
Tangu zamani inajulikana ndani ya daladala ni sehemu ya vituko vingi, kuna matukio mengi kwa kuwa asilimia kubwa wanaotumia ni wale wenzangu na mimi wenye ipato cha chini na kipato cha kati.
Nasema hivyo kuwa kuwa ni watu wachache sana ambao wana kipato cha juu wanatumia usafiri huo, japo inapotokea kwa asilimia ndogo.
Hiyo inatokana na hadha zilizopo katika usafiri huo wa umma, kwanza ni wa shida hasa mida ya asubuhi na jioni ambapo kunakuwa na mzunguko mkubwa wa watu wengi kutoka na kurejea nyumbani au kwenda vibaruani.
Ugomvi, lugha kali, dharau, kubanana, kuibiana, kutomasana, kupapasana, lugha za kukera, ni baadhi ya mambo ambayo sisi wapanda daladala, mwendokasi, Bajaj tunakutana nayo.
Ndiyo maana wanasema ukitaka kupata au kuona vituko vingi wewe banda daladala au mwendokasi hasa mida niliyotaja jioni au asubuhi.
Changamoto niliyoiona ni kuwa kuna watu wengi sijui ni stress au tabia zimebadilika, au maisha magumu au ni nini hasa! Kuna ugomvi mwingi unatokea bila sababu za msingi na unaweza kukwepeka lakini bado inatokea.
Wiki iliyopita nikiwa kituoni, ilikuja daladala watu wakiwa wengi, wakaanza kugombania, mbaba mmoja (miaka 35-40) akaweka begi lake kwenye siti yeye akiwa nje.
Alipoenda kugombania akafanikiwa kuingia, kufika kwenye ile siti akamkuta mdada amekaa, akaanza kulumbana naye atoke mdada akagoma, wakati hayo yakitokea kulikuwa bado kuna siti kama sita hivi zipo wazi nyuma ya hiyo siti wanayoigombania.
Sasa bahati nzuri gari ikawa haijajaa kumbe abiria wengi hawakuwa wakienda ‘route’ hiyo, hivyo siti zikawa nyingi, lakini yule ‘mwamba’ akakomaa na dada wa watu mpaka wakaanza kuvutana, ikawa mbinde kwelikweli.
Jamaa anamvuta mdada wa watu kama ile siti ni mali yake vile, wakati nyuma kuna siti kibao zipo wazi, tuliokuwa pembeni tukajiuliza huku mwamba ni stress au ameweka nini kwenye hiyo siti.
Niishie hapo siku mbili baadaye likatokea tukio kama hilo katika daladala nyingine nikilishuhudiA.
Juzi kati tena nikiwa kwenye basi la kwenda mkoani ikatokea sekeseke kama hilo, jamaa kakaa kwenye siti ambayo siyo namba ya tiketi yake, akaja mwenye siti yake ambaye ni mdada, mzee baba akagoma kutoka.
Yaani inachekesha lakini inashangaza, ilibidi wahudumu wa basi watumie nguvu kubwa kumtaka jamaa aondoke kwenye siti, akawa anagoma, ikabidi wafikie hatua ya kutishia kumshusha kwenye basi kwa kuwa ndio kwanza lilikuwa kituoni likijiandaa kutoka, ndipo akakubali kishingo upande.
Sasa hivyo ni mifano michache tu, njua hata wewe unayo mingine mingi, hivi najiuliza, sisi Watanzania ni nini hasa kinatusumbua kichwani, ni stress za maisha au basi tu watu wameamua kujitoa akili?
Naamini wengi mmekutana na matukio ya aina hii au mengine yanayoonesha wazi vichwa vya Wabongo vipo lesi.
========================
MWANASAIKOLOJIA ASEMA WANA MSONGO WA MAWAZO
Mwanasaikolojia Sylvia Sostenes ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Thamani Yangu Initiative inayotoa huduma za kisaikolojia kutoka Ubungo Jijini Dar es Salaam anazungumzia sababu za kutokea mivutano katika usafiri wa umma:
“Imekuwa ni kawaida kutoka matukio hayo hasa katika miaka ya hivi karibuni, asilimia kubwa hiyo inatokea kwa kuwa wahusika wana matatizo ya kisaikolojia.
“Wapo wanaofanya hivyo kwa kuwa wanakuwa wameshindwa kumaliza tofauti zao za walipotoka, hivyo wanakwenda kulipuka sehemu ambzo wanazimudu, na sehemu hizo wanajua ugomvi hautakuwa wa watu wawili.
“Wanajua akifanya ugomvi kwenye umma atapata sapoti ya watu au watu kuingilia na hautakuwa mkubwa.
“Unakuta mtu ameambiwa sogea kidogo au amechelewa kukupa nauli, mtu anakuja juu kwa kuwa ana hasira zake ambazo alishindwa kuzitoa huko alikotoka.
“Hali hii siyo tu kwenye usafiri, bali sehemu nyingi zenye msongamano wa watu kama sokoni, shuleni, hospitali na kwingineko.
“Nashauri wanaokuwa na msongo wa mawazo au wenye kawaida ya kufanya hivyo ni vema mtu akajifunza kutafuta utatuzi wa matatizo yake na siyo kutegemea kutoa msongo wake wa mawazo kwenye maeneo ya watu wengi.”