Mahakama ya Kadhi
Mheshimiwa Mufti;
Kuhusu mchakato wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi, nimeyasikia maoni yenu kwamba kumekuwa na kulegalega kwa upande wa Serikali jambo linalowafanya muingiwe na wasiwasi kuhusu nia njema ya Serikali katika mchakato huu. Napenda kuwatoa hofu kuwa hakuna kulegalega wala kubadilika kwa dhamira ya Serikali. Msimamo wa Serikali upo pale pale. Huu ni uamuzi uliofanywa na Chama chetu na Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya uongozi wa Rais Benjamin Mkapa wa kutaka kulitafutia ufumbuzi suala la Mahakama ya Kadhi na kuachiwa Serikali ya Awamu ya Nne kutekeleza.
Na sisi katika kufuatilia utekelezaji wa jambo hili tulikabidhi Tume ya Kurekebisha Sheria kuishauri Serikali. Ushauri wa Tume hiyo ulikuwa kwamba Serikali haiwezi kuunda Mahakama ya kushughulikia masuala ya kidini ya dini fulani. Jambo hilo liachiwe Waislamu wenyewe kufanya.
Serikali imekubali ushauri huo na ndipo mchakato ukaanza na tukaunda Kamati ya pamoja iliyojumuisha Serikali na BAKWATA. Nia ya Serikali ni kujihakikishia kuwa hicho kitakachoundwa hakiendi nje ya masuala ya kidini yaani ndoa, takala, mirathi na wakfu kwa mujibu wa dini ya Kiislamu. Katu si Mahakama ya kushughulikia masuala ya jinai au madai. Haitajihusisha na masuala ya wizi na kutoa adhabu kama vile za kukatwa mikono. Haitahusika na kesi za fumanizi na hivyo kutoa hukumu ya kuuawa mkosaji kwa kupigwa mawe. La hasha !! Narudia kuwa mamlaka yake yatahusu ndoa, takala, mirathi na wakfu. Isitoshe Muislamu hatazuiliwa kuamua kutumia sheria za nchi kwa masuala hayo akipenda kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mufti, Waheshimiwa Masheikh, Ndugu Zangu Waislamu;
Napenda kuwatoa hofu pia kwamba hakuna mkono wa mtu wapo mnadhania hivyo. Maana, tunajuana. Si ajabu kuna hisia kuwa huenda Kanisa limeingilia kati kuzuia au kuchelewesha. Siyo hivyo hata kidogo. Tarehe 22 Julai, 2011 nilipoalikwa kuzungumza na Maaskofu katika kikao chao cha Jukwaa la Wakristo katika risala yao kwangu kuhusu suala la Mahakama ya Kadhi walitoa ushauri ufuatao kuwa:
"Kuanzisha Mahakama ya Kadhi nchini na jambo zuri linalowahusu Waislamu. Kwa kuwa ni jambo la kidini waachiwe Waislamu wenyewe walifanye ndani ya Uislamu, pasipo kutumia hazina ya Serikali ambayo ni fedha ya walipa kodi wote nchini"
Hiyo ni nukuu kutoka ibara ya 6 ya Risala yao kuhusu Uhuru wa Kuabudu na dhana ya Udini.
Katika maelezo yangu kwao, niliwahakikishia kuwa mawazo yao yanawiana na yale ya Serikali kama ilivyoshauriwa na Tume ya Kurekebisha Sheria ambayo Mwenyekiti wake ni Profesa Ibrahim Juma. Mahakama hii itaundwa na Waislamu wenyewe ndani ya Uislamu wao na wataiendesha wenyewe na haitagharamiwa na Serikali.
JK