Wanasiasa hawa wapime kama bado wanatufaa!

Wanasiasa hawa wapime kama bado wanatufaa!

sulphadoxine

JF-Expert Member
Joined
Nov 1, 2010
Posts
2,257
Reaction score
649
Waziri wa Uchukuzi na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe...JPG Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka.JPG Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela.JPG Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.JPG


WIKI hii Rais wa Marekani, Barack Obama alifanya ziara ya wiki moja barani Afrika, akizulu nchi tatu ikiwamo nchi yetu, Tanzania. Obama alianzia ziara yake nchini Senegal, kisha akaelekea ‘bondeni' kwa Mzee Madiba kabla ya kuhitimisha ziara hiyo Tanzania, ambako alipiga kambi kwa siku mbili kabla ya kukwea ‘pipa' lake kurejea Marekani.


Akiwa nchini, Rais Obama alizungumza na watu mbalimbali, lakini kubwa zaidi alizindua mradi mkubwa wa umeme ambao unadaiwa kuwa utapunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la nishati hiyo nchini na bara la Afrika kwa ujumla. Uzinduzi wa mradi huo ulifanyikia maeneo ya Ubungo, ambapo pia Rais Obama alitembelea mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya Symbion Power iliyopo katika eneo hilo. Kumbukumbu zangu zinaonesha kuwa Kampuni ya Symbion Power ndiyo iliyonunua ile mitambo ya kufua umeme wa dharura iliyokuwa ikimilikiwa na kampuni ya Richmond.

Kampuni ya Richmond ndiyo ambayo mwaka 2007 ilizua tafrani kubwa nchini na kusababisha aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Ngoyai Lowassa kubwaga manyanga na kutoa fursa kwa Rais Jakaya Kikwete kulivunja Baraza la Mawaziri na kulisuka upya. Hatua ya Waziri Mkuu kujiuzulu ilitokana na ripoti ya uchunguzi wa Kamati ya Bunge, iliyokuwa ikiongozwa na Waziri wa sasa wa Uchukuzi na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe.

Akisoma ripoti hiyo bungeni, Dk. Mwakyembe alilithibitishia Bunge kuwa kampuni ya Richmond ilikuwa ni kampuni feki, tena ya mfukoni, isiyokuwa na uwezo hata wa kufunga hata bulb ya umeme kwenye soketi yake! Aidha katika ripoti hiyo Dk. Mwakyembe alisema kuwa kampuni licha ya kushindwa kuzalisha hata unit moja ya umeme lakini ilikuwa ikilipwa fedha za walipakodi zaidi ya shilingi milioni 152 kwa siku bila ya kufanya kazi. Ripoti ya Dk. Mwakyembe ilitoa mapendekezo 21 yakiwemo ya kutaka baadhi ya vigogo serikalini waliohusika na utoaji wa zabuni kwa kampuni ya Richmond kuwajibishwa, huku pia ikimtaka Waziri Mkuu, Lowassa ajipime mwenyewe kama kweli anastahili kuendelea na wadhifa huo.

Nayakumbuka vema maneno ya Lowasa aliyoyatoa bungeni muda mfupi kabla ya kutangaza kujiuzulu, na hapa nayanukuu "Mhe. Spika nimefadhaika sana, nimeonewa sana, nimedhalilishwa sana katika hili, tunahutubia nchi nzima na kusema waziri mkuu amefanya hiki amefanya hiki bila kumsikiliza, mimi nadhani there is a wish, wish I'm going to grant, ni Uwaziri Mkuu, Nadhani tatizo ni uwaziri Mkuu kwamba ionekane Waziri Mkuu ndiye amefanya haya, tumuondolee heshma au tumwajibishe, nimetafakari sana kwa niaba ya chama changu, kwa niaba ya Serikali yangu nimeamua kumwandikia Rais barua ya kumwomba niachie ngazi…" Mwisho wa kumnukuu. Baada ya Waziri Mkuu kujiuzulu na baraza lake kuvunjwa na kusukwa upya, sasa likafuata suala la mitambo yenyewe ya kufua umeme ambayo ilidaiwa kuwa mkataba wake ulihamishiwa kwa kampuni ya Dowans. Sitaki kuingia ndani zaidi juu ya kampuni hiyo, kwa vile watanzania wengi tulikuwa tukifuatilia sakata hilo nap engine hata hayo niliyoyakumbusha hapo juu wengi wetu tunayafahamu vizuri zaidi.

Kampuni ya Dowans baada ya kuona wanasiasa ‘wameziba' mianya yote ya kufanya biashara ya kufua umeme nchini kwa kutumia mitambo hiyo, hatimaye ilitangaza kuiuza mitambo yake. Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zuberi Zitto Kabwe ambaye kwa wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma, aliishauri Serikali kupitia Shirika la Ugavi wa Umeme nchini Tanesco kuinunua mitambo hiyo ili itumike kuzalisha umeme na kupunguza tatizo sugu la nishati hiyo nchini. Ushauri huo ulionekana kutowapendeza baadhi ya wanasiasa ambao walikuwa msitari wa mbele kupambana na sakata la Richmond, wakidai kuwa mitambo hiyo ilikuwa ni chakavu, isiyo na uwezo wa kuzalisha umeme nchini.

Wanasiasa hao ambao baadhi yao kwa sasa ni mawaziri maarufu kwenye Serikali ya Dk. Kikwete, walisimamia kwenye sheria ya Manunuzi ambayo wakati ule ilikuwa ikipinga Serikali kununua vitu vilivyokwisha tumika, maarufu kwa jina la mitumba. Kampuni ya Dowans ilipoona mianya yote ya kupata riziki kutoka serikalini imezibwa na wanasiasa hao, ilitangaza kuiuza mitambo hiyo kwa kampuni yoyote yenye uwezo wa kuinunua na ndipo ilipoibuka Symbion Power na kuichukua. Sitaki kuamini kuwa katika ujio wake, Obama alikuja nchini na mitambo mingine mipya, bali ninao uhakika kuwa ni mitambo hiyo hiyo ambayo ilikaguliwa na juzi na Rais Obama na kutamka kuwa kwa kutumia mitambo hiyo hiyo sasa Tanzania itanufaika na mradi wa mkubwa wa umeme ambao utasambazwa hadi vijijini, huku wanasiasa wale wale waliokuwa msitari wa mbele kupinga isinunuliwe na serikali wakipiga makofi! Leo ni siku ya tatu tangu Rais Obama aondoke nchini, wanasiasa wetu machachari wapo kimya kabisa kuhusiana na mitambo hiyo waliyoipinga kwa nguvu zao zote, lakini sasa inaonekana kuwa ndiyo matumaini mapya ya tatizo la umeme nchini.

Kuna msemo wa lugha ya kingereza unaosemam kuwa ‘the time will tell' ukimaanisha kwamba yapo mambo ambayo yanaweza kukosa ufumbuzi kwa sasa lakini baada ya wakati fulani muda utazungumza. Hapa nina maswali machache kwa wanasiasa hao ambao naamini kuwa wanajitambua ipasavyo, kwanza je, wanakubali kwamba maneno ya aliyekuwa Waziri Mkuu Lowassa kuwa alionewa na kudhalilishwa yalikuwa ya kweli? Lakini pia ni vema wakatoa ufafanuzi kwa umma wa watanzania sababu za wao kupinga mitambo ile isinunuliwe na Tanesco zilikuwa ni kwa maslahi ya taifa au maslahi yao ya kisiasa? Ikiwa mitambo hiyo itaweza kufua umeme na kupunguza kama sio kumaliza kabisa tatizo la umeme nchini, watakuwa tayari kukiri kwamba kwa kuipinga na kuifanya isizalishe umeme kwa zaidi ya miaka saba tangu ilipoingizwa nchini na wao wamechangia watanzania kupata shida ya uhaba wa umeme na kukwamisha shughuli za kimaendeleo nchini? Nadhani umefika wakati ambao wanasiasa wetu badala ya kuangalia zaidi maslahi yao, waanze kufikiria kuweka uzalendo mbele ili kuepusha taifa kutumbukia kwenye matatizo na kukwamisha maendeleo.

Pengine mashabiki wa wanasiasa hao wanaweza wasifurahishwe sana na makala hii, lakini ifahamike kwamba sina nia ya kumchafua mtu wala kumjenga mtu isipokuwa ni jambo jema kukumbuka tulikotoka, tulipo na tuendako ili kuepuka kurudia makosa ambayo pengine yanaligharimu taifa. Inawezekana kabisa wanasiasa hao kwa sasa wakawa na upeo mkubwa zaidi juu ya suala hili na pengine kwa makala hii walazimika kutoa matamko ambayo yanifungua mimi na watanzania wenzangu kuhusiana na mambo yaliyo numa ya pazia juu ya ujio wa Rais Obama nchini na lengo la rais huyo kwenda kuzindua mitambo ambayo sisi tulielewa kuwa ni ya kifisadi! Ni kwa mantiki hiyo ndiyo sababu nikaandika makala hii, nikiwaomba wanasiasa wetu machachari kama vile Samwel Sitta, Dk. Mwakyembe, Anne Kilango Malecela, Christopher Ole Sendeka na wengine wengi waliokuwa msitari wa mbele kuipinga mitambo hiyo sasa watoke hadharani na kutoa ufafanuzi wa kina kwa watanzania ambao utawapima kama kweli bado wanafaa kuwa wapiganaji wa ufisadi kwa niaba yetu au wakati ule walikuwa na ajenda zao ambazo sasa zinaelekea kufichuka!


Source Gazeti la kulikoni.
 
Watanzania ni wasaulifu sana eti siku izi baadhi utawasikia wakisema lowa ni jembe eti anafaa! Sasa sijui ndo tushachanganyikiwa?
 
Back
Top Bottom