Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya "Tuwaambie kabla hawajaharibiwa" iliyofanyika Septemba 25, 2024 katika uwanja wa Ruanda Nzovwe Jijini Mbeya, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe Beno Malisa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Mhe Juma Homera amewataka wanafunzi kutosita kutoa taarifa za ukatili ili ziweze kufanyiwa kazi.
Aliongeza kuwa, kampeni hii inakwenda kuwakumbusha wazazi na walezi wajibu wao kwa watoto wao wa kutoa malezi bora ikiwa ni pamoja na kufuatilia mienendo na tabia za watoto wao ili kubaini mabadiliko mbalimbali wanayopitia na endapo kama kuna vitendo vibaya wanavyofanyiwa waweze kubaini na kuchukua hatua.
"Kampeni hii imelenga kutoa elimu ya kupinga ukatili kwa Wanafunzi wa Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo vikuu na vya kati ili kuwajengea uwezo na uelewa wa kujitambua na kujua thamani yao katika jamii" alisema Malisa.
Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mbeya Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Veronica Ponera amewataka wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari kushirikiana na Jeshi la Polisi, Wazazi na Walimu kwa kutoa taarifa za viashiria vya ukatili bila kuogopa ili wasiharibiwe na kupelekea kutofikia ndoto zao za kimaisha.
Kampeni ya Tuwaambie kabla hawajaharibiwa kitaifa ilizinduliwa Agosti 29, 2024 Mkoani Njombe na Mkuu wa Mkoa huo Mhe Anthony Mtaka ikilenga kutoa elimu ya kujitambua kwa Wanafunzi ili kuwaepusha dhidi ya uharibifu unaosababishwa na utandawazi na kuiga matendo mabaya kama vile ulevi, matumizi ya dawa za kulevya na mapenzi ya jinsia moja (ushoga).