Pili ambaye alianza harakati za Siasa Mwaka 2020 akiwa Mwanachama hai wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye aligombea nafasi ya udiwani mara mbili, Mwaka 2020 na 2015 ndipo aliposhinda na kuwa diwani.
“Sikukata tamaa, niligombea mara mbili nafasi ya udiwani, Mwaka 2015 bahati ilikuwa upande wangu nilifanikiwa kuupata Udiwani,” amesema Pili.
Mwanasiasa huyo ambaye ni Mkulima na mama wa nyumbani pia, amesema ushiriki mdogo wa Wanawake katika nafasi za uongozi zinawanyima fursa za kushika nafasi za juu za uongozi na vyombo vya maamuzi.
“Niliingia katika Siasa kuongoza kama kielelezo. Kuhakikisha hakuna Mwanamke anayeachwa nyuma. Kwa miaka yote katika Baraza letu la Madiwani, nimehakikisha masuala ya Wanawake na watoto yanapewa uzito na umuhimu sawa.”
Anasema kuwa, licha ya uhaba wao katika nafasi za uongozi lakini wakipata nafasi hizo, wanafanya vizuri ikiwemo kutetea haki za Wanawake na Watoto na kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo katika wadi zao.
Kupata taarifa na matukio kuelekea uchaguzi mkuu 2025 kwa kila mkoa ingia hapa: Special Thread: Mijadala na Matukio ya Uchaguzi Mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
“Nilijiunga na Siasa kwa sababu nilitaka kufanya mambo mengi zaidi kwa ajili ya Wasichana na Wanawake ambao huku kwetu vijijini tuko nyuma kimaendeleo, katika kuwawezesha Wanawake kiuchumi wachukuwe mikopo wajiendeleze kimaendeleo.”
Amesema kuwa, masuala mengi yanayohusu Wanawake hayaingizwi katika sera, mipango na bajeti za Halmashauri kwani wengi wanaoshikilia nafasi za juu za upatikanaji wa maji, uwezeshaji kiuchumi kwa Wanawake zinashikiliwa na Wanaume, hivyo ni vyema kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, Wanawake wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi za uongozi ili kuongeza ushiriki wao.
Soma Pia kwa taarifa zaidi zinazowahusu wanawake kipindi hichi cha uchaguzi: Kipindi hiki cha Uchaguzi wanawake wanapata nafasi ya kutosha kushiriki kwenye masuala ya uchaguzi?
Maryam Ali Mussa, Diwani wa Viti maalum katika Baraza la Manispaa Wilaya ya Mjini Unguja anasema ushiriki wa Wanawake katika nafasi za uongozi bado ni mdogo, na kuwataka kuongeza ushiriki wao katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Amesema kuwa, ni vyema Wanawake wanaotaka kugombea nafasi za uongozi kujitathimini kabla ya kugombea nafasi wanayoitaka kugombea ili iwe rahisi kuipata.
Anashauri “Nawashauri Wanawake wenzangu wanaotaka kugombea ni vyema kuangalia kwa makini na kujitathimini nafasi wanazotaka kugombea ili iwe rahisi kwako kuwahudumia wananchi watakapo chaguliwa.”
Amesema kuwa, huu ndio wakati wa Wanawake kushirikiana kuelekea katika uchaguzi mkuu ili kupeana uzoefu wa kugombea, na kushika majimbo mengi ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Tume ya Uchaguzi – ZEC ya Mwaka 2020 idadi ya madiwani ni 110, Wanaume wakiwa 85 sawa na asilimia 77% na Wanawake 25 sawa na asilimia 23, huku wawakilishi Wanawake wa kuchaguliwa ni wanane kati ya 50 sawa na asilimia 16.
Upande wa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaoiwakilisha Zanzibar kwenye majimbo 50 ya uchaguzi ni wanne tu, sawa na asilimia nane.
Hali hiyo inaonesha, haja ya Wanawake kuongezeka katika nafasi za uwakilishi katika majimbo ya uchaguzi ifikapo Mwaka 2025, kwani idadi ya wawakilishi Wanawake ni kidogo.
Dk Mzuri Issa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ) ambao kwa kushirikiana na Taasisi ya Kidemokrasia (NDI), walifanya utafiti juu ya kujua hali ya wanawake viongozi kwenye vyama vya siasa.
“Ushiriki hai wa Wanawake katika siasa mara nyingi husababisha kuimarika kwa hali ya kijamii na kiuchumi, kwani Wanawake wana uwezo wa kukabiliana na kupunguza umasikini ukilinganisha na wenzao wanaume,” amemaliza Dk Mzuri akiwa Ofisini kwake Tunguu Zanzibar.
Amesema kuwa ipo haja kwa Serikali, asasi za kiraia na vyama vya siasa kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuondoa vikwazo kwa Wanawake ili iwe rahisi kwao kugombeea nafasi za uongozi, huku akiona utekelezaji wa mikataba na matamko mbali mbali ya kikanda na kimataifa ya kuhamasisha usawa wa kijinsia bado utekelezaji wake haujafikiwa.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi ya Tanzania ya Mwaka 2022, inaonesha kuwa Zanzibar ina wakazi wapao milioni 1.8 kati ya hao Wanaume ni 915,492 na Wanawake ni 974, 281.
Hii ina maana kwamba, Wanawake ni asilimia 51.6 ya wakaazi wote wa Zanzibar, lakini wingi wao huo hauonekani katika nafasi za uongozi.
Abdulrazak Said Ali, Mwanasheria kutoka Ofisi ya Msajii wa Vyama vya Siasa Zanzibar amesema “Kuongezwa kwa Kifungu cha 10 C katika Sheria ya Vyama vya Siasa nchini itasaidia kuongeza kwa ushiriki wa Wanawake kwani Sheria hiyo inavitaka vyama vya siasa kuwa na Sheria ya Jinsia kwa muda wote.
“Lengo la kuongeza kwa kifungu hicho katika sheria ya vyama vya siasa nchini ni kuongeza ushiriki wa wanawake kwa kuwa na sera ya jinsia kwa muda wote” amesema mwanasheria huyo.”
NA MARYAM NASSOR