KAMA maji ya bahari ya hindi yangekuwa na hisia, basi yangejisiskia fahari sana kwa kupata fursa nyingine ya kuiburudisha miili ya viumbe hawa wawili ambao walikuwa wakiogelea kandokando ya ufuko huku wakicheza na kucheka.
Walifanya picha ya kuvutia sana, hasa sura zao nzuri zilipoibuka na kutoka majini na kumezwa na tabasamu lililosababishwa na mzaha waliokuwa wakifanyiana chini ya maji. Baada ya kuogelea kwa muda walirejea nchi kavu ambako walijibwaga juu ya mchanga ulioruhusu joto likaushe maji miilini mwao.
Ufuko pia ungekuwa na kila sababu ya kusherehekea johari ya kulaliwa na viumbe kama hawa kwani walioana kimaumbile kama pacha, ingawa hawakuwa mtu na dada yake.
Walikuwa kama jozi ya kiatu cha kiume kwa cha kike. Mwanamume hakuwa mwingine zaidi ya yule kijana mwenye umbo refu, kakamavu, lililokaa kiriadhariadha na sura nzuri, yenye dalili zote za hekima, ushujaa na ucheshi. Kwa jina anaitwa Joram Kiango.