Wasifu wa Julius Nyerere: Katiba ya TANU na bendera ya Muingereza

Wasifu wa Julius Nyerere: Katiba ya TANU na bendera ya Muingereza

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
WASIFU WA JULIUS NYERERE: SUALA LA KATIBA YA TANU NA BENDERA YA UINGEREZA KUPEPEA TANGANYIKA

Katika kitabu cha maisha ya Mwalimu Nyerere nimekutana na suala la bendera ya Muingereza, Union Jack kupepea Tanganyika.

Waandishi wamelieleza kuwa ni moja ya masuala yaliyojadiliwa katika mkutano wa kuasisi TANU mwaka wa 1954.

Mimi nilikutana na suala hili mwaka wa 1952 katika Nyaraka za Sykes kupitia Tanganyika African Government Association (TAGSA) chama cha watumishi wa serikali Waafrika.

Mtu unaweza kusema mwanzo wa mwaka wa 1950 kwa wazalendo wa Tanganyika huu ulikuwa mwaka wao mzuri kwa sababu walifanya mambo mengi ya kutajika.

Huu ndiyo mwaka ambao vijana, Dr. Vedasto Kyaruzi na Abdul Sykes walishika nafasi ya rais na katibu katika TAA baada ya kuwaondoa madarakani, rais na katibu wake Thomas Saudtz Plantan na Clement Mohamed Mtamila.

Huu pia ndiyo mwaka Abdul Sykes alikutana na Jomo Kenyatta Nairobi na kufanya mkutano wa siri vipi waunganishe nguvu za TAA na KAU dhidi ya Waingereza.

Huu ndiyo mwaka pia ambao TAA iliunda TAA Political Subcommitee kazi yake ikiwa kushughulika na mambo yote ya siasa ndani ya chama.

Muhimu hapa kueleza ni kuwa walikuwa ndani ya kamati hii na mwanasheria Earle Seaton ambae alisaidia sana katika kuishauri TAA katika mambo yote ya sheria yanayohusu nchi zilizo chini ya udhamini wa UNO.

Bahati mbaya sana hii kamati haijapata kuelezwa hata na waandishi walioandika historia ya TANU kabla yangu na katika kitabu hiki cha Mwalimu pia sioni ikipewa umuhimu.

Dr. Kyaruzi katika mswada wake, ‘’Muhaya Doctor,’’ hakuitaja popote ingawa yeye mwenyewe alikuwa mwanakamati.

Dr. Kyaruzi kama Mwalimu Nyerere inapobidi watajwe wazee wa Dar es Salaam wote watatiwa kwenye kikapu cha wazee ambao majina yao hayatajwi.

Cranford Pratt peke yake ndiye aliyeitaja hii kamati katika kitabu chake, ‘’Crirical Phase in Tanzania,’’ pale alipoisifia kwa kutoa mapendekezo yake kwenye kamati ya katiba ya Gavana Edward Francis Twining kwa kusema kuwa katika mapendendekezo yote Tanganyika nzima haya ya TAA Political Subcommitte ndiyo yalishinda yote.

Wajumbe wa kamati hii walikuwa Dr. Vedasto Kyaruzi, Abdulwahid Sykes, Hamza Mwapachu, Steven Mhando, Mufti Sheikh Hassan bin Ameir, Sheikh Said Chaurembo na John Rupia.

Kamati hii labda kama si kuwepo katika Nyaraka za Sykes nami nikaitaja katika kitabu cha Abdul Sykes isingejulikana kama ilikuwapo.

Hili lingetokea baadhi ya wajumbe wa kamati hii kama Mufti wa Tanganyika Sheikh Hassan bin Ameir na Said Chaurembo wasingekuwa sehemu ya historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika.

Sasa turejee katika suala la Union Jack, bendera ya Muingereza kupepea katika ardhi ya Tanganyika.

Suala hili katika kitabu cha Mwalimu limeunganishwa na suala la katiba ya TANU na limeegemezwa kwa Nyerere.

Lakini ukweli ni kuwa lilishashughulikiwa huko nyuma miaka mingi kabla haya Nyerere hajafika Dar es Salaam.

Mimi nimekutana na suala hili mwaka wa 1952 katika memorandum ya TAGSA uliowasilishwa kwa kamati ya UNO ya nchi chini ya udhamini wake iliyotembelea Tanganyika.

Wakati ule Rais wa TAGSA alikuwa Dr. Wilbard Mwanjisi na Katibu wake Ally Sykes na katika wanakamati alikuwamo Rashid Mfaume Kawawa na Dr. Michael Lugazia.

Katika viongozi wa walioshika nafasi ya urais wa TAGSA kuanzia mwaka wa 1951 walikuwa Thomas Marealle na Steven Mhando lakini nafasi ya katibu haikubadili Ally Sykes alichaguliwa mara nne kama katibu.

Sasa kamati ya UNO ya udhamini ilipofika Tanganyika TAGSA ikawapa memorandum yake na zaidi ilikuwa kuhusu ajira na mishahara iliyokuwa inatolewa kwa ubaguzi wa rangi.

Hii kamati ya UNO haikufanya lolote la maana katika malalamiko ya TAGSA na Ally Sykes kama katibu barua zote alizokuwa anamwandikia Chief Secretary Bruce Hutt, alizipuuza kwani alikuwa hazijibu.

Hapo ndipo Ally Sykes akamwandikia barua Chief Secretary kumwambia kuwa Uingereza ijitoe katika kama mdhamini wa Tanganyika na Union Jack, bendera ya Muingereza ishushwe haina haki kupepea kwenya ardhi ya Tanganyika kwani Tanganyika si koloni la Uingereza (Ally Sykes, TAGSA Honorary Secretary, to The Honourable Chief Secretary to the Government; Ref. No.1/52/3 10th January 1952).

Nilikuwa nikisoma hizi barua za Ally Sykes nikimuuliza kwa nini yeye alikuwa hana lugha ya stahamala na yeye akinijibu akisema, ‘’Mwanangu Mohamed mimi nina bahati kuzaliwa Tanganyika, Waingereza ni watu waungwana kama nilingezaliwa Mozambique, Wareno wangeshaniua mimi.’’

Dossa Aziz alipata kuniambia kuwa wao walikuwa wakimpa Ally Sykes kazi zote za hatari na alikuwa hazikatai.

Babu yake Ally Sykes , Sykes Mbuwane alitokea Mozambique.

Kuna mahali niliandika kuhusu Ally Sykes na Dr. Mwanjisi baada ya kuwajua vyema nikasema hawa watu wawili kwa ile misimamo yao ilivyokuwa mikali si watu wa kuwaachia chama chochote cha siasa peke yao bila kuwa mgongoni kwao kuangalia maamuzi yao vinginevyo wanaweza kukuponzeni nyote mkaangamizwa na serikali.

Baada ya barua hii ya Ally Sykes kuhoji mamlaka ya Uingereza Tangayika, serikali ilighadhibika sana na viongozi wote wa TAGSA akiwemo Ally Sykes, Rashid Kawawa, Dr. Mwanjisi wakahamishwa Dar es Salaam na kupelekwa majimboni.

Ally Sykes alikataa uhamisho.

Bila shaka katika barua ile ulikuwako mkono wa Dr. Mwanjisi na pengine Steven Mhando kwani hizo ndizo zilikuwa lugha zao, watu wa misimamo mikali.

Steven Mhando yeye anasomesha historia darasani Shule ya Kitchwele anawaeleza wanafunzi wake kuwa Waingereza ni wezi wa fadhila.

Kisa cha maneno haya ni kwa wanahistoria wa Kiingereza kuwaandika Susi na Chuma kuwa walikuwa watumishi wa David Livingstone na akifika hapo anawauliza wanafunzi wake ni mfanyakazi gani atabeba maiti ya muajiri wake kichwani zaidi ya maili 1000 kutoka Chiponda Zambia hadi Bagamoyo ili ukazikwe kwao Uingereza na kwa ujira gan
Steven Mhando anamalizia uchambuzi wake kwa kusema kuwa Susi na Chuma wale walikuwa ndugu zake David Livingstone hawakuwa wapagazi wake.

Dr. Mwanjisi alipata kuwaita Waingereza, ‘’washenzi,’’ yaani hawajastaarabika kwa kudhani rangi ya ngozi ya mtu ndiyo inayojenga akili yake, kwa maana ukiwa mweupe una akili na ukiwa mweusi hamna kitu.

Hawa viongozi wa wawili wa TAGSA baada ya uhuru wote walisuguana na Nyerere na wakanuniana hadi wote wanaingia ndani ya makaburi yao.

Kuhusu katiba ya TANU inayosemwa ukweli ni kuwa hakuna watu waliokaa kuandika katiba mpya.

Katiba ya TANU ilinakiliwa kutoka katiba ya Convetion People’s Party (CPP) ya Kwame Nkrumah wa Ghana.

Mwandishi yeyote yule anaetaka kumtembeza Julius Nyerere kwenye barabara ya TANU akiwa peke yake njia nzima kuna mengi sana muhimu yatampita.

Dr. Michael Lugazia katika miaka yake ya mwisho akifanyakazi Ocean Road Hospital alikuwa akisema kuwa historia ya TANU jinsi inavyoelezwa na kuandikwa utadhani kama vile Julius Nyerere alikuwa peke yake katika kupigania uhuru wa Tanganyika.

Picha: Gavana Edward Twining, Baraza la Wazee wa TANU lililotoa tarifa mbele ya ujumbe wa UNO, August 1957, Saadan Abdu Kandoro mbele ya Ujumbe wa UNO (Picha kutoka kitabu cha Saadan Abdu Kandoro, ''Mwito wa Uhuru,'' 1961).
Picha ya sanamu ya David Livingstone, katika Kumbukumbu yake Blantyre, Glasgow, Scotland 1991.

BARAZA LA WAZEE WA TANU KANDORO.jpg


EDWARD TWINING.jpg


SAADAN ABDU KANDORO NA UJUMBE WA UNO 1957.jpg


DAVID LIVINSTONE AND ME.jpg
 
Back
Top Bottom