Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
NANI ANAWAKUMBUKA BANTU GROUP WAHAMASISHAJI WA TANU NA WALINZI WA MWALIMU NYERERE?
Bantu Group lilikuwa kundi la vijana wanachama wa TANU waliokuwa wahamasishaji wa TANU na walinzi wa viongozi na Mwalimu Nyerere.
Silaha zao za ulinzi zilikuwa silaha za jadi, mashoka mapanga na mikuki.
Vijana hawa walikuwa na vibweka vingi katika mikutano ya TANU.
Watafika mapema viwanja vya Mnazi Mmoja wakitokea ofisi ya TANU New Street wamevaa kaniki na malubega na wengine magunia huku wamejipaka masinzi.
Njia nzima wakiimba nyimbo za kuhamsisha uzalendo na ukombozi wa Tanganyika.
Uwanjani BANTU GROUP watatimua vumbi jingi hapo kwa kucheza ngoma hasa Mganda, ngoma ya Kizaramo.
Katika kufanya hivi wanachama wengine wa TANU wataingia uwanjani kuwaunga mkono.
Wakipumzika BANTU GROUP inaingia Kwaya ya TANU ikiongozwa na kijana Rajab Matimbwa na wenzake akina Katumbwele.
Wakimaliza hawa gramaphone inapiga santuri ya Frank Humplink akiimba, "Nasikia king'weng'we..."
Ukisikia nyimbo hiyo watu wanajua karibu Sheikh Suleiman Takadir atapanda jukwaani kusoma dua na kufungua mkutano Nyerere ahutubie.
Mikutano ya TANU ikipambika hasa.
Katika picha kulia ni Julius Nyerere Territorial President wa TANU, John Rupia Vice-President na Sheikh Suleiman Takadir Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU na nyuma ni walinzi wa TANU Bantu Group.
Huu ulikuwa wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika katika miaka ya 1950.