SoC01 Wasomi wetu wamekosa mvuto, nini kafanyike?

SoC01 Wasomi wetu wamekosa mvuto, nini kafanyike?

Stories of Change - 2021 Competition

Gnyaisa

Member
Joined
Jul 13, 2021
Posts
23
Reaction score
24
Zaidi ya miaka 15 iliyopita wakati nikiwa ningali mwanafunzi wa shule ya msingi, ndoto yangu kubwa ilikuwa kufikia elimu ya Chuo Kikuu. Wakati huo sikuwa na matamanio ya kuwa daktari bingwa, mwandishi nguli au mwanasheria aliyebobea kwa sababu niliamini nikifika Chuo Kikuu nitayafikia matamanio hayo. Mwalimu wangu darasani alikuwa akifundisha na kuacha baadhi ya mambo bila kuyafafanua kwa kina kwa maelezo kwamba tukifika Chuo Kikuu tutaelewa zaidi na hivyo kuniongezea hamasa ya kusoma kwa bidii mpaka Chuo Kikuu.

Nyumbani pia wazazi walinihimiza mara kwa mara kusoma kwa bidii ili nifanikiwe kufika Chuo Kikuu. Wahitimu wa vyuo vikuu mtaani walikuwa wanahesabika na kufahamika kuwa wewe ni msomi wa Chuo Kikuu ilikuwa sifa kubwa katika jamii. Niliamini (bado naamini mpaka sasa) kuwa msomi wa Chuo Kikuu ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kupambanua mambo mbalimbali na kupambana na kila aina ya changamoto katika jamii.

Idadi ya Vyuo Vikuu ilikuwa ndogo nchini lakini viliweza kutoa mazao bora ya wataalamu katika fani mbalimbali walioweza kupambana na wenzao wa mataifa ya nje na kuwapiku. Familia yenye msomi wa Chuo Kikuu ilikuwa na kila sababu ya kujivunia na kujitapa dhidi ya familia nyingine.

Miaka ya hivi karibuni mambo yameanza kubadilika kwa kasi ya kutisha! Idadi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanaotamani kufikia kiwango cha elimu ya juu inaporomoka kila kukicha! Vijana hawa kwa sasa wanatamani kuwa wasanii wa Bongo Fleva na Bongo Muvi kuliko wanavyotamani kuwa wahadhiri wa Vyuo Vikuu. Utaanzia wapi kumshawishi awe Profesa wa Chuo Kikuu ilhali anawaona Diamond Platinumz na msanii Nandi wakichekelea mamilioni kwa shoo ya siku moja! Utaanzia wapi kumshauri awe mtaalamu wa masuala ya kompyuta na teknolojia kisha aanze kuzurura mtaani kusaka ajira ilhali anamuona rafiki (mentor) yake Joti akijikusanyia mamilioni kwa kuchekesha watu!

Lengo la makala haya si kukosoa kazi nzuri zinazofanywa na vijana wenzetu kupitia matumizi sahihi ya vipaji vyao licha ya wengi wao kutokuwa na elimu kubwa ya Vyuo Vikuu bali kujadili sababu ya hawa tunaowaita “wasomi” kukosa mvuto katika jamii. Shauku ya familia mbalimbali kuwa na angalau msomi mmoja inazidi kupungua kutokana na wasomi hao kugeuka mizigo katika jamii na tanuru la lawama dhidi ya serikali, ndugu na jamaa zao.

Msomi huyu aliyesotea shahada ya Chuo Kikuu kwa zaidi ya muongo mmoja kwa maana ya miaka 7 ya shule ya msingi, miaka 6 ya sekondari na miaka mingine 3 hadi mitano ya Chuo Kikuu, anategemewa kuwa moto wa kuotea mbali katika kupambana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii na kisha kuzibadili changamoto hizo kuwa fursa za kujipatia kipato na kuzalisha ajira kwa wengine. Jamii haitarajii kumuona msomi huyu akilalamikia kukosekana kwa mtaji fedha kama sababu kuu ya kumfanya ashindwe kujiajiri na kuajiri wenzao.

Jamii inaamini msomi ni kama askari aliyepelekwa ughaibuni kupata mafunzo makali ya ukomandoo kwa lengo la kurudi na kupambana na “vibaka” wanaovamia kijijini mara kwa mara na kupora mali zao kwa kutumia silaha za jadi lakini baadae inashangaza kumuona “komandoo” huyu akiwakimbia vibaka hao kwa maelezo kwamba hawezi kupambana kwakuwa kijijini hakuna mabomu ya machozi wala silaha nzito za kupambana na vibaka hao!

Muziki wa Tanzania unapendwa na unaongoza kwa kusikilizwa katika nchi zote za Afrika Mashariki! Msomi uliebobea katika fani ya sheria unaanzia wapi kulalamikia ukosefu wa ajira ilhali wasanii wetu wa Bongo Fleva wanalalamikia kuzulumiwa kazi zao na hata kutapeliwa katika shoo mbalimbali kutokana na kutojua jinsi ya kuingia makubaliano mazuri ya kimikataba? Si fursa hii kwa wasomi hawa kujiajiri badala ya kusubiri ajira kutoka Utumishi? Kama komandoo wa vita anatupwa msituni akiwa na begi dogo la kumsaidia kufika katika kambi ya adui iliyojaa silaha, komandoo huyu wa elimu anashindwa vipi kuwa msaada katika jamii?

Tasnia ya filamu Tanzania inaongoza kwa kupendwa katika nchi zote za Afrika Mashariki na kati! Msomi uliehitimu shahada ya utawala katika biashara unaanzia wapi kuilalamikia serikali kutokuzalisha ajira ilhali wasanii hawa hawajui mbinu bora za kusambaza kazi zao katika mataifa ya Kenya, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo? Si fursa hii kwa wasomi hawa kuandaa maandiko bora ya miradi ya jinsi ya kuwasaidia wasanii wetu na hatimaye kuwa fursa mpya ya ajira?

Wasomi tuamke, tujitambua na tuwe chachu ya mabadiliko katika jamii ili jamii hiyo ituheshimu. Haisaidii kitu tukiendelea kulalamika na kudhani pengine serikali mpya ikiingia madarakani itabadili hali ya mambo bila sisi kubadili fikra na mitazamo yetu kuhusu maisha. Tuache kubweteka vijiweni kwakuwa msomi ni askari kamili aliyepewa mafunzo muhimu ya jinsi ya kupambana na maadui ujinga, umaskini na maradhi.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom